Operesheni usafi mitaro nchini, wakati wake sasa

01Jan 2020
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Operesheni usafi mitaro nchini, wakati wake sasa

KUNA mengi ambayo serikali ya awamu ya tano inazidi kujijengea uhalali kwenye suala zima la utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazokabili wananchi katika suala zima la kujenga ustawi na maendeleo ya jamii ya Kitanzania.

Ninaweza kuzungumzia maeneo mengi kuanzia kwenye suala zima la kupambana dhidi ya rushwa na ufisadi, watumishi hewa, uhalifu hususani unyang’anyi, ujambazi na ujangili.

Lakini hata katika suala la kuboresha hali ya miundombinu ya barabara, vituo vya afya, ukarabati na ujenzi wa madarasa, maabara, maktaba, utoaji wa elimu bure kwa kutaja baadhi ya mambo.

Muungwana anaona haya yote ni katika ile dhima ya kutekeleza majukumu na wajibu wa serikali hii kwa wananchi wake.

Na hiyo ni kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo Rais na timu yake, waliinadi wakati wa kampeni za kutafuta ridhaa ya kuongoza taifa hili.

Kama nilivyosema hapo juu kuna mengi ambayo yametekelezwa na serikali hii, lakini kwa makusudi maalumu Muungwana amevutiwa zaidi kuzungumzia operesheni mbili ambazo kwa mtazamo wake zimeiongezea alama serikali ya awamu ya tano.

Zimeiongezea alama mbele ya macho ya wananchi na hasa wenye mapenzi mema kwa ustawi wa taifa na raia wake, lakini pia hata katika suala la usafi wa mazingira na uhai wa viumbe vinavyoyategemea mazingira hayo.

Operesheni ya kwanza anayoirejea Muungwana ni ile iliyochukuliwa na serikali mwaka 2017 inayofahamika hadi leo kama operesheni ‘piga marufuku viroba’ vilivyokuwa maarufu katika maeneo mbalimbali nchini.

Kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, serikali ilipiga marufuku uzalishaji, uuzaji, uingizaji na matumizi ya pombe inayofungwa kwenye pakiti za plastiki kwa jina la viroba kuanzia Machi Mosi, mwaka 2017.

Aidha, ikaweka wazi kwamba ambaye angebainika kuvitumia angewajibishwa kwa kulipa faini, kufungwa jela au vyote kwa pamoja.

Ilichukua hatua hiyo kwa nia nzuri ya kulinda afya ya Watanzania, hususani vijana ambao ndiyo nguvukazi ya taifa hili wanaotengeneza sehemu kubwa ya idadi ya Watanzania takribani milioni 55 kwa hivi sasa.

Kwa wanaokumbuka hali ilipokuwa imefikia wakati huo kiasi kwamba viroba vilienea kila kona hata kwa watoto wa shule za msingi ambao nao walianza kuvitumia kwa sababu ya urahisi wake wa kuvibeba, kwani iliwezekana hata kuviweka mfukoni na kutembea navyo.

Madhara ya viroba yalikuwa mabaya sana kwa afya na maendeleo ya Watanzania kwani mbali na ajali za barabarani zilizotokana na uendeshaji wa kizembe hasa kwa madereva wa bodaboda, pia yaliharibu mazingira kutokana na kuzagaa kwa vifungashio hivyo.

Operesheni ya pili ambayo imeendelea kuipa alama serikali hii ni iliyochukuliwa na serikali hivi karibuni ambayo imepiga marufuku uzalishaji, uingizaji, usafirishaji nje ya nchi, usambazaji, uuzaji na matumizi ya mifuko aina ya plastiki maarufu kama ‘Rambo’ iliyokuwa ikitumika kubebea bidhaa kuanzia Juni Mosi.

Katika operesheni zote mbili, serikali ilitoa maelekezo na hatua madhubuti itakazochukua kwa wote ambao wangekaidi maelekezo yake.

Kama nilivyosema hapo juu, kufanikiwa kwa operesheni hizi kunaonyesha kwamba serikali hii inapoelekeza marufuku dhidi ya dosari fulani iliyo na madhara kwa watu wake, wananchi wanaelewa na kutekeleza.

Wanafanya hivyo kwa sababu wanajua haina simile katika kuchukua hatua.

Wakati Muungwana akipongeza umadhubuti wa serikali katika kusimamia masuala yenye tija kwa wananchi, anatoa wito operesheni kama hiyo sasa ielekezwe katika usafi wa mitaro kwenye majiji na miji, hasa jiji la Dar es Salaam, lenye hali mbaya katika eneo hilo.

Muungwana ana imani kwamba serikali ikielekeza nguvu kwenye eneo hili la mitaro katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, suala la mlipuko wa magonjwa kama kipundupindu na homa ya Dengue iliyopo sasa yatakwisha.