Pipi, biskuti hizi shuleni zifuatiliwe

05Jul 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Pipi, biskuti hizi shuleni zifuatiliwe

BAADHI ya walimu katika shule za jijini Dar es Salaam, wanadai kwamba kumekuwapo na pipi na biskuti zinazouzwa karibu na maeneo ya shule, wanazodhani huenda, zinatengenezwa kwa vitu ambavyo si salama kwa afya na ustawi wa wanafunzi.

Kutokana na hali hiyo, walimu hao wanaiomba serikali kufuatilia kwa karibu viwanda vinavyozalisha pipi hizo na biskuti ili kuhakikisha kama zinafaa kutumiwa na wanafunzi au ni hatari kwa afya zao.

 

Maombi hayo waliyatoa hivi karibuni kwenye warsha ya kutoa taarifa ya utendaji kazi wa kamati za kuzuia ukatili dhidi ya watoto shuleni ilioandaliwa na asasi ya kiraia ya Ekama Development Tanzania.

Walimu hao wanasema karibu maeneo yote ya shule kuna vibanda vinauza vitu mbalimbali zikiwamo pipi na biskuti ambazo nyingine zina harufu ya kahawa  au sigara, hali ambayo wanadhani siyo salama kwa watoto.

Warsha hiyo ilishirikisha wadau zaidi ya 150 wakiwamo maofisa wa ustawi wa jamii, polisi walimu, wanafunzi, wazazi na viongozi wa dini, ambao kila upande ulitoa maoni kuhusu mambo mbalimbali.

"Inawezekana hata wauzaji wakawa hawajui kuhusu pipi na biskuti hizo, lakini kuna haja serikali kufuatilia ili kubaini kama zina madhara au hazina ili watoto wetu wawe salama," anasema mmoja wa walimu.

Anaeleza kuwa anajua watoto wanakumbana na changamoto nyingi zikiwamo za kuingia katika vibanda vya video mitaani, ambavyo vinachangia ukatili kwao, lakini pia suala la biashara katika maeneo ya shule ni la kufuatiliwa kwa karibu.

Mwalimu huyo anataka biashara holela kwenye maeneo ya shule idhibitiwe ili kulinda afya za wanafunzi kuliko kuacha kila mtu akifanya anavyotaka na mwisho wa siku wanaweza kusababisha madhara.

Vilevile anawashauri wazazi kuwa makini kwa kuwapa watoto wao maelekezo ya kutambua ni vitu gani vya kununua wawapo shuleni kuliko kununua kila wanachotaka, kwa vile wanaweza kujikuta wakinunua visivyofaa.

Anataka ikiwezekana, mtoto apewe chakula kutoka nyumbani kuliko pesa ambazo anajikuta ananunua hata vitu visivyofaa na kwamba anajua watoto wanapenda pipi na biskuti, lakini pia ni muhimu wakaelezwa madhara yake.

Kutokana na ushauri wa mwalimu huyo ni vyema mamlaka husika zikafuatilia biashara hiyo na pia wazazi kuwa makini wanapowapa watoto wao pesa za kutumia shuleni ili kuepuka kuwaingiza kwenye hatari.

Wakati mwalimu huyo akisema hayo, bado pia kuna haja ya kufuatilia maji yanayofungwa kwenye mifuko myeupe ya nailoni, ambayo ni maarufu kwa jina la 'Kandoro', nayo yanadaiwa kuwa hatari.

Maji hayo yamekuwa yakiuzwa mitaani na hata kwenye maeneo ya shule yatakuwa yanapatikana, kwani huchangamkiwa sana na watoto kutokana na kuuzwa kwa bei nafuu.

Jambo la kuzingatia ni kwamba maji hayo huwa hayachemshwi, hivyo si salama kwa wanywaji, ndio maana nikasema kuwa biashara hiyo nayo ifuatiliwe na kupigwa marufuku ili kulinda afya za watu.

Ni muhimu wanaofanya biashara hiyo wakawa makini ili kubaini taarifa ambazo zinalalamikiwa na walimu ili kulinda afya za wanafunzi kuliko kufanya kiholela na kusababisha wasiwe salama.

Waswahili wana msemo usemao; lisemwalo lipo, kama halipo, laja, hivyo inawezekana kinacholalamikiwa na walimu kina ukweli na kama hakipo, basi kinaweza kujitokeza baadaye.

Hii inatokana na ukweli kwamba hata baadhi ya wabunge walishawahi kulalamika kwamba kuna baadhi ya pipi zenye dawa za kulevya zilizokuwa zikiuzwa kwenye maeneo ya shule huku wanafunzi wakitumia bila kujua.

Kwa hali kama hiyo ni wazi kwamba inawezekana hata wauzaji nao wasijue kwamba wanauza pipi au biskuti zenye dawa za kulevya, hivyo ni vyema wakawa makini wanapochukua bidhaa za kuuza.

Bila kufanya hivyo, wataendelea kuweka rehani afya za wanafunzi kwa kutojua au kwa kujua ili mradi tu wapate pesa hata kwa njia ambayo inahatarisha afya za wengine.