Poleni mabinti, sheria sasa ichukue mkondo

20Jul 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Poleni mabinti, sheria sasa ichukue mkondo

JUMLA ya watoto 981, wamepata mimba katika kipindi cha miezi sita kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, katika Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, hali inayoonyesha kuwa jitihada zaidi za kupambana na unyanyanyasi watoto kingono zinahitajika.

Kwa hesabu hiyo, ni kwamba kila mwezi, watoto 163 wamepata mimba katika kipindi hicho wilayani humo, na kama ikitokea wilaya zote za mkoa zina tatizo hilo, maana yake ni kwamba idadi 'itatisha' na mabinti hawatasoma watakuwa wanalea.

Akiwa katika ziara Kibondo, yenye lengo la kukagua na kujionea utoaji wa huduma za ustawi wa jamii na masuala ya maendeleo ya jamii, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis, anaagiza watuhumiwa watafutwe na kuchukuliwa hatua.

Anataja mimba hizo kwa watoto kama kitendo cha ukatili wa kijinsi, na kwamba taarifa hizo haziwezi kufumbiwa macho, badala yake watendaji wanaohusika wafanye kila linalowezekana ili watuhumiwa wapatikane na haki inatendeka katika kipindi kifupi.

Kimsingi, jamii haiwezi kutegemea miujiza ya mafanikio ya kizazi kijacho iwapo itabaki kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kwa kuangalia watoto wao wakidhalilishwa kingono katika umri mdogo, kuambukizwa maradhi, wengine kufariki kwenye uzazi na kupata ulemavu ikiwamo fistula wakati wa kujifungua.

Hivyo kama anavyosema kiongozi huyo, ni vyema kila mzazi na mlezi kufanya sehemu yake katika malezi ya mtoto ikiwamo kumwepusha na mazingira yanayoweza kumsababishia kupata mimba za utotoni.

Wapo baadhi ya wazazi na walezi ambao hudaiwa kushirikiana na watu wanaowapa mimba mabinti kwa kumalizakana kimya kimya, inawezekana mazingira kama hayo ndiyo yamefanyika hata katika wilaya ya Kibondo, kwa kuwa  hakuna hatua zilizochukuliwa hadi serikali ilipotoa maelekezo ya kukamatwa watuhumiwa.

Hivyo ili kumaliza tatizo hilo, mabadiliko yanatakiwa kufanyika kuanzia kwa wazazi na walezi, watambue umuhimu wa elimu kwa watoto wao na kuachana na tamaa ya kutaka mali kwa njia zisizo halali.

Watoto wa kike wanatakiwa kuachwa waendelee na masomo yao bila ya usumbufu, hivyo wazazi na walezi wanaoshiriki kuwaoza, watambue kuwa wanawaharibia ndoto zao kielimu na hata afya.

Katika kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, ni vyema nguvu ziendelee kuelekezwa katika uwekezaji kwenye elimu kwa watoto wa kike, wawe shuleni, wasome bila vikwazo.

Hatua hiyo inaweza kubadilisha mitazamo kuhusu majukumu ya kijinsia na usawa wa kijinsia na kutambua kuwa mtoto wa kike ana haki ya kupata elimu kama ilivyo kwa mtoto wa kiume.

Mbali na hilo, suala la elimu ya afya ya uzazi inatiliwa mkazo kwa watoto waliofikia kuvunja umri wa ungo, ili kuzuia mimba na pia kuhimiza wazazi na walezi waweze kushiriki kikamilifu katika vita dhidi na ndoa na mimba hizo.

Kila upande ukitimiza wajibu, ni rahisi kutambua kuwa mimba za utotoni huathiri afya, elimu na haki za mtoto wa kike, kwa kuwa mtoto wa kike asiye na elimu itamuwia vigumu kupata maisha bora na kujitegemea baadaye.

Kadhalika binti anayepata mimba akiwa na umri wa miaka 14 au pungufu inaelezwa kuwa haki zake zinakiukwa, hivyo ili awe  salama, ni muhimu wadau wote kushiriki katika vita dhidi ya mimba na ndoa za utotoni.

Pamoja na mbinu na njia mbalimbali ambazo zinatumika kudhibiti mimba za utotoni tatizo limeendelea kuwapo kama hilo la Kibondo, hali inayoashiria kuwa kuna haja ya kuchukua hatua zaidi.