Polisi Dar imekuwaje wapigadebe hawa, mbona kimya?

08Sep 2017
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Polisi Dar imekuwaje wapigadebe hawa, mbona kimya?

WAPIGADEBE kuendelea kung’ang’ania vituoni ndicho kinachowafanya wengi kuhisi kuwa huenda ilikuwa ni nguvu ya soda kutangaza kuwa wangeondolewa ili kumaliza kero zisizo na sababu vituoni.

Huenda watu wengi walifurahia uamuzi wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kutangaza kwamba wapiga debe wataondolewa kwenye vituo vya daladala.

Aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu, Lucas Mkondya, alitangaza operesheni hiyo mwanzoni mwa mwezi uliopita na kuahidi kuwa watawakamata vituoni iwapo watakaidi kuondoka wenyewe.

Pamoja na agizo hilo, hadi sasa wapiga debe wapo maeneo hayo na hii inaweza kuleta hofu miongozi mwa jamii kwamba kundi hili linaogopwa ama linalindwa kwa vile mbali na kupokonya fedha , wapiga debe ni watumia mihadarati, walaghai na wengine wanadaiwa kushambulia madereva na makondakata.

Wanadaiwa hutumia bisibisi, nyembe na hata sindano kuwachoma madereva na makonda wanoko wanaowanyima fedha.
Hali ilitulia kwa muda muda mfupi pale waliposikia kwenye vyombo vya habari kuwa, operesheni inaanza.

Kamanda wa kanda hiyo, aliyeteuliwa hivi karibuni, Lazaro Mambosasa, kati ya masuala ambayo anapaswa asiyasahau ni kuwashughulikia wapiga debe ambao wamekuwa ni kero kubwa kwenye vituo vya daladala.

Kwa kiasi kikubwa wapigadebe hawa wamedaiwa kuwa ni chanzo cha wizi katika vituo vingi hususan Mwenge, Buguruni na Mbezi ambako inaonekana ni kati ya vituo sugu na pengine wanadhani wapo juu ya sheria.

Wanapora mikoba ya wanawake, simu, pochi za wanaume na kukimbilia vichochoro, huku baadhi ya watu wakishuhudia kwa kuogopa kujeruhiwa au kuchomwa na vitu vyenye ncha kali kama bisibisi.

Wapigadebe wa Mwenge mathalani, wanafahamika hata wanakoziuzia simu mara baada ya kuwakwapulia abiria au mtu yeyote aliyepo kwenye kituo hicho, na ilifikia wakati mtu ambaye alihitaji simu ya bei chee ya aina fulani, mpigadebe humuahidi kumpatia baada ya nusu saa akitarajia kumkwapua abiria kituoni hapo.

Tandale kwa Mtogole ndio ni zaidi imepewa jina ‘mahakama ya simu’ yaani simu zinahukumiwa mchana bila hofu. Ndiyo maana watu hujiuliza wasimamizi na walinzi wa raia wako wapi?

Makondakta wa daladala wamekuwa wakipigwa mkwara iwapo watatoa siri za wapiga debe ambao wanafahamika kwamba ni wezi au ambao wanashuhudia abiria wao wakiibiwa.

Na hata baada ya mpiga debe kupigia debe gari na kondakta kama hatampatia walau Shilingi 500 ajue anaweka maisha yake rehani.

Katika karne hii ni ya 21 kwa tafsiri ya kwamba maendeleo ya wanadamu yanashika kasi, hivyo suala la kujua kusoma nakutambua gari unalopanda ni tatizo hata uhitaji kelele za Kimara Mbezi, Kariakoo, Buguruni , Tegeta….?

Kuendekeza wapiga debe Arusha, Mbeya, Mwanza na Dar es Salaam ni kizamani.

Daladala za sasa zina jina la ruti, nauli na njia inayotumika lakini pia kuna mkanda wa rangi tofauti ambazo humfanya aliye mvivu wa kusoma au kutokujua kusoma, kukariri kuwa daladala rangi fulani itakuwa inakwenda wapi.

Kwa sasa Watanzania wengi hasa wa majiji ambako usafiri huu wa umma unatumika zaidi wanajua kusoma, hivyo kuendelea kuishi kwa mazoea na kuwategemea wapiga debe wakufikishe uendako kumepitwa na wakati na ni kuendekeza vibaka.

Kupiga debe wakati watu wanajua kusoma si sahihi, na pia wapigadebe hawa wana akili na wengi wao wana viungo vilivyokamilika ni vyema wakajishughulishe na kazi nyingine na kuwaingizi kipato badala ya kugeuka ombaomba.