Polisi mnalea jipu uchaguzi wa meya Dar

04Mar 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Polisi mnalea jipu uchaguzi wa meya Dar

KWANZA kabisa nilipongeze Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa ambayo limekuwa likifanya ili kuhakikisha raia wa Tanzania na mali zao wanakuwa salama, hasa kutokana na ukweli kwamba kazi ya msingi ya polisi ni kulinda raia na mali zao.

Wamekuwa wakifanyakazi kuhakikisha kwamba wanaweka mambo sawa pale wanapogundua kuna viashiria vya uvunjifu wa amani ndani ya jamii ama kwenye mkusanyiko wa watu.

Mfano wa jinsi Polisi wanavyofanya kazi ili kuhakikisha watu wanakuwa salama ni mkutano wa uchaguzi wa Meya wa jijini Dar es Salaam, ambao ulikumbwa na vurugu ndipo polisi wakalazimika kuingilia kati ili kuleta amani.

Uchaguzi huo ambao ulikuwa ufanyike Jumamosi ya Februari 27, uliahirishwa baada ya kuwapo kwa taarifa kwamba kuna zuio kutoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliahirishwa baada ya Kaimu Mkurugenzi wa Jiji aliyekuwa Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Theresia Mmbando, kusoma kile alichodai ni zuio la Mahakama ya Kisutu lililokuwa linalenga kusitisha uchaguzi huo.

Hatua hiyo ya Mmbando ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, ilizua sintofahamu iliyosababisha wajumbe wa pande mbili wa wa CCM, CUF na Chadema kurushiana maneno, hali iliyolazimu polisi kuingilia kati kumtoa kiongozi huyo wa serikali chini ya ulinzi baada ya kupata misukosuko kutoka kwa baadhi ya wajumbe.

Lakini ajabu ni kwamba siku moja tu baada ya kuahirishwa kwa uchaguzi kwa madai ya kuwapo kwa zuio kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Warialwande Lema, alikanusha zuio hilo na kusema kuwa ni uongo; kwamba mahakama yake haijatoa zuio lolote.

Kwa kauli yake akasema: "Mahakama ilitoa amri ya zuio la muda Februari 5, mwaka huu la kuzuia uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 8, mwaka huu, ilipanga kusikiliza maombi hayo Februari 15 lakini walalamikaji hawakufika mahakamani,” akasema na kuongeza: "Mahakama ilipanga tena maombi hayo kusikilizwa Februari 23, mwaka huu lakini pia hawakutokea mahakamani.”

Akaongeza kuwa baada ya walalamikaji kushindwa kufika mahakamani kusikiliza maombi yao, mahakama hiyo ililiondoa maombi ya zuio yaliyokuwa yamewasilishwa na walalamikaji Susan Massawe na Saad Khimji, dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.

Hakimu huyo akasema kuwa madai kwamba ilitoa zuio la uchaguzi huo ni ya uongo na kwamba, zuio lake lilikuwa la uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 8, mwaka huu, ambalo baadaye lilifutwa baada ya walalamikaji kutoonekana mahakamani.

Baada ya kueleza kwa kirefu jinsi hali halisi ilivyo, nije kwenye hoja ya msingi kutokana na kile kinachoendelea sasa baada ya uchaguzi huo kuahirishwa kwa zuio ambalo kimsingi halipo hasa kufuatia mahakama kulikataa.

Hadi sasa wapo baadhi ya wajumbe ambao wamekamatwa na Jeshi la Polisi baada ya kutokea vurugu kufuatiwa kutolewa kwa tangazo la zuio la uchaguzi huo na aliyekuwa akiusimamia.

Kwanza ieleweke kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi ilizushiwa uongo na kwa mujibu wa wataalam wa sheria, kusema uongo ni kosa la jinai, hivyo waliozusha uongo huo wanapaswa kushughulikiwa.

Vile vile msimamizi wa uchaguzi huo anaonekana hakuwa makini ama aliamua kukubaliana na uongo huo hadi kusababisha vurugu zilizotokea katika ukumbi wa mkutano wakati wajumbe wakijiandaa kupiga kura.

Kwa mtazamo wangu ni kwamba msimamizi wa uchaguzi anapaswa kuhojiwa ni kwa nini aliwasilisha zuio la uongo na pia walioleta tangazo la zuio hilo ambalo mahakama imeliita 'feki' nao wanatakiwa kukamatwa na vyombo vya dola.

Kama nilivyosema awali, ninalipongeza Jeshi la Polisi kwa jinsi linavyojitahidi kuhakikisha usalama wa raia na mali zao na pia sishabikii vurugu zilizojitokeza baada ya kuahirishwa kwa uchaguzi wa Meya.

Ninawashauri polisi wetu kwamba ingekuwa vyema zaidi kuwakamata wale ambao walikuwa chanzo cha vurugu hizo wangeunganishwa na hao wanaotuhumiwa kuzifanya.

Kwa kawaida mtu huwa anaangilia alikojikwaa na siyo alikoangukia, kwa maana hiyo polisi wangeangalia kwanza chanzo cha vurugu hizo ni nini na kukifanyia kazi na siyo kung'ang'ania upande mmoja tu.

Ikumbukwe kwamba kilichofanyika hadi uchaguzi kuahirishwa kwa mara na nne ni kuzuia shughuli halali kwa zuio la uongo, hivyo walioleta zuio hilo hawana budi kuwa kwenye mikono ya vyombo vya dola.

Bahati nzuri Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshawarahisishia kazi polisi, kwamba haihusiki na zuio hilo, hivyo askari hao walipaswa kuwasaka waliohusika katika mchezo huo ambao kwa kweli haufai.

Haufai kwani baadhi ya wanasiasa sasa wanatupeleka pabaya na kwa mtindo huu wa kutaka kutimiza malengo yao binafsi, wanaweza kusababisha wananchi wasiziamini Mahakama.

Wataalam wa sheria wanasema kuwa kilichofanywa na wale waliozuia uchaguzi huo ni kosa la jinai na wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kusema uongo na kuzuia shughuli halali kwa uongo.

Kunani uchaguzi wa Meya Dar es Salaam kuahirishwa mara kwa mara hata kwa zuio la uongo? Hili ni jipu ambalo linahitaji kutumbuliwa mapema sana kabla halijaleta madhara makubwa.