Polisi, TPSIS jipangeni kuwaunganisha walinzi binafsi

20Jun 2019
Mashaka Mgeta
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Polisi, TPSIS jipangeni kuwaunganisha walinzi binafsi

HIVI karibuni, kumezinduliwa mpango wa kuwasajili walinzi binafsi wanaofanya kazi kwenye makazi na taasisi za kijamii.

Mpango huo uliotangazwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Huduma za Kuunganisha Walinzi Binafsi (TPSIS), Dk. David Rwegoshora, unalishirikisha Jeshi la Polisi katika utoaji mafunzo na utunzaji wa taarifa za walinzi binafsi, hasa walio nje ya mfumo wa kampuni binafsi za ulinzi nchini.

Dk. Rwegoshora anasema, mpango huo hauiingizi TPSIS katika kuwaajiri walinzi, bali kuchukua na kutunza kumbukumbu zao kwa mukhtadha wa kuwawezesha kujulikana rasmi polisi, kunufaika na mafunzo na kuunganishwa na masoko ya ndani na nje ya nchi.

Hiyo ni moja ya mambo mapya ya kibunifu na yanayojenga dhana ya kuisaidia jamii, ili iendelee kuishi katika mazingira ya amani na utulivu. Hivyo, kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.

Dk. Rwegoshora alinukuliwa akisema TPSIS haihusiki katika kuwaajiri walinzi binafsi, isipokuwa kuwaunganisha kwenye mfumo wa utunzaji wa kanzidata (database) ambao polisi itakuwa na uwezo wa ‘kuupitia’ katika ngazi ya Taifa na mkoa.

Pia, Dk. Rwegoshora anasema walinzi watakaojisajili kupitia mpango huo, watapewa mafunzo yenye lengo la kutambua na kudhibiti uhalifu kabla haujatokea.

Anasema mbinu na stadi hizo zinatolewa na Jeshi la Polisi, huku TPSIS ikiwa ni mratibu wa mafunzo hayo.

Kwa muda mrefu, jamii imeshuhudia makubwa ya polisi, katika kukabiliana na wahalifu. Hiyo, haishii kuhatarishi maisha ya askari vijana raia wa taifa pekee, bali kunatumia fedha nyingi ambazo kama (uhalifu) ungedhibitiwa mapema, zingeelekezwa kwenye matumizi mengine.

Pia mpango huo unajijibu kadhia mbalimbali ambazo raia wamekuwa wakizipata pindi wanapohitaji walinzi binafsi kwenye makazi yao, taasisi kama shule ama maeneo ya kufanyia biashara.

Utaratibu uliozoeleka na unaoendelea kutumiwa na jamii ni wa kuagizia mlinzi binafsi kutoka maeneo yenye jamii, zenye historia ya uthubutu katika kuifanya kazi hiyo.

Awali, raia kutoka kabila la Wamakonde waliheshimika sana kwenye maeneo ya mijini hasa Dar es Salaam, kwamba walifaa kwa huduma ya ulinzi binafsi.

Baadaye, hali ilibadilika taratibu na sasa sehemu kubwa ya Wamasai wanaaminika kufaa katika utoaji huduma hiyo, ingawa wapo watu kutoka jamii nyinginezo wanaojishughulisha na kazi hiyo.

Lakini, katika hali ya kustaajabisha, si walinzi binafsi au waajiri wenye taarifa sahihi zitakazowasaidia hasa yanapotokea matatizo. Kwa maana upatikanaji wake na namna wanavyoingia makubaliano ni miongoni mwa mambo yanayofanyika ‘kienyeji’.

Ndio maana niliposoma kuhusu kuzinduliwa kwa mpango huo na kwamba unapatikana kwa njia ya kujisajili kupitia mtandao unaoweza kupatikana hata kupitia simu ya kiganjani, nikaona ni fursa zinazoweka mazingira bora kwa amani, usalama na utulivu.

Pengine sasa ni jukumu la waratibu wa mpango huo, TPSIS na Jeshi la Polisi kwa ujumla, kuhakikisha kwamba maeneo kadhaa yanapewa kipaumbele na kuingizwa kwenye mafunzo ama utendaji wa aina yoyote katika utekelezaji wa mradi huo.

Maeneo hayo ni pamoja na ‘kuwaivisha’ wanufaika wa huduma hiyo katika uzalendo kwa nchi na watu wake. Walinzi binafsi ni nyanja inayoajiri watu wengi wanaotekeleza wajibu unaopaswa kutekelezwa na Jeshi la Polisi, kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Hivyo, watakapowekwa kwenye kanzi data na kutambulika rasmi kwa majina, sura, alama za mwili na mienendo yao, hawana budi kutambua umuhimu wao kwa jamii. Umuhimu huo unajikita katika uzalendo kwa nchi.

Pengine, ndio maana mpango huo ukaweka bayana kwamba msisitizo mkubwa wa mafunzo kwa walinzi binafsi utawekwa katika kutambua na kudhibiti uhalifu kabla ya kutokea.

Ni wakati kwa walinzi binafsi na wengine watakaotambua umuhimu wa mpango huo, kujitokeza na kuunga mkono kwa vile hatua ya kuwekwa pamoja, inatoa nafasi ya kufahamiana, kubadilishana mawazo na pengine kutafuta namna nzuri ya kukabiliana ama kuzitatua changamoto zinazowakabili.

Lakini, kwa upande wa waratibu na Jeshi Polisi, hawapaswi kulidhika tu, kwamba wamefanikiwa kuwaunganisha walinzi binafsi kwa kuwaandalia kanzi data, la hasha!

Katika ulimwengu wa sasa ambapo uhalifu wa kwenye mtandao umeshamiri, lolote linaweza kutumika hata ikibidi kwa nia ovu.

Inabidi wakati wote wahusika wa mpango huo waendelee kuwa makini, ili hatimaye kufikia malengo wanayoyakusudia.

Mwandishi anapatikana kwa simu: (+255) 0754 691540 au baruapepe: [email protected].