Pongezi Rais Samia, namna ulivyoingilia ya Machinga

23Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Pongezi Rais Samia, namna ulivyoingilia ya Machinga

MOJA ya tabia kubwa ambayo binadamu tunayo, ni kwamba kuna wakati huwa ni wepesi wa kupuuza baadhi ya mambo. Lakini, yakishakuwa makubwa au mazito, ndipo hapo tunaanza kujiuliza nini kilitokea.

Kupuuza ni hulka ya asili ambayo kila mwanadamu anayo kwa viwango tofauti na ndiyo maana, huwa kuna msemo unaoeleza kiongozi mzuri ni yule anatatua matatizo ya watu wake, lakini kiongozi bora ni yule ambaye anaona tatizo kabla halijatokea.

Mara nyingi dhana hiyo ya kutatua tatizo, ndiyo ambayo huwa inachukuliwa na wengi kwa mtazamo wa mkumbo kuwa ndiye kiongozi bora, lakini kiuhalisia yule ambaye anaona tatizo kabla halijatokea, ndiye anayestahili kupewa pongezi mama analishinda tatizo.

Kwanini nasema hivyo? Mara nyingi hasa kwenye hizi sekta kubwa au nafasi kubwa, viongozi wengi wanapenda kuwa katika upande wa wale wanaotatua matatizo kwa kuwa wanajua watapata sifa nyingi na wataonekana ndiyo wanaostahili.

Wale ambao wanatatua matatizo kabla hayajatokea huo ndiyo wa muhimu zaidi, lakini kwa kuwa tu jamii ya watu haiwaoni au haioni kile kinachofanywa na wao, basi umuhimu wao unaonekana mdogo.

Kwa sasa, kuna sakata la Wamachinga na jinsi ya kuweka utaratibu mzuri wa wao kufanya biashara. Tofauti na ilivyo sasa, asilimia kubwa wanafanya kiholela bila ya kuwa na mpangilio sahihi.

Wamachinga licha ya kuwa ni ndugu zetu, familia, marafiki na jamaa zetu, lakini ukweli ni kuwa kuna tatizo kubwa linatokana na wao kukosa utaratibu mzuri wa kufanya shughuli zao.

Suala hilo lilitakiwa kuwa limeshafanyia kazi miaka mingi nyuma ja ka ya kukua kufikia hatua ya sasa. Tatizo hilo nalo limekuwa likiendelea kila mwaka.

Ni kweli wamachinga wanahitaji kufanya biashara zao, lakini kila kiongozi anapoingilia kutaka kufanya au kuweka utaratibu mzuri wa kuwawezesha waendelee na biashara zao, bila ya kuwavuruga watu wengine. Inakuwa ngumu kuwa tayari kwa sababu nguvu ya wamachinga iko kubwa.

Kwa maisha ya Kitanzania yalivyo sasa, ni lazima kila Mtanzania awe anajihusisha kwa namna moja au nyingine katika biashara hii, iwe kwa mtu wake anashiriki kuuza au yeye mwenyewe kutegemea kununua bidhaa kutoka kwa machinga.

Kwa msingi huo, inamaanisha kuwa sakata la wamachinga ni mzizi mkubwa ambao kuudhibiti unahitaji akili kubwa. Kutumia nguvu pekee, ni kuingia katika matatizo makubwa.

Nampongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuligusia suala hilo la wamachinga. Anajua wazi kuingia kutumia nguvu pekee haitasaidia, ndiyo maana ameagiza utumike utaratibu wa mazungumzo na kueleweshana.

Kwa kawaida, kunaelezwa kuwapo baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakilazimika kutumia wamachinga katika kuuza biadhaa zao.

Niseme, kufanya hivyo kunamaanisha kuwa suala la kodi ni mtihani, serikali inakosa chake cha kuisaidia kuendesha nchi.

Kama tabia hiyo, itaendelea kuachwa na itafika hatua itaonekana ni kawaida, huku serikali iikipoteza fedha nyingi kutokana kusuasua katika kuchukua uamuzi mapema.

Nirejee maelezo ya Rais Samia ni ya msingi sana. Anatambua kuwa suala la wamachinga kwa sasa hutakiwi kuliingilia ‘kichwa kichwa’, kwani kufanya hivyo ni kutengeneza mazingira ya kukosekana kwa imani hasa kwa maeneo mengi.

Machinga wanaendesha maisha yao na familia zao katika sura oana inayofika mbali. Idadi yao ni mamilioni ya watu, hivyo kuwaondoa ghafla kwenye utaratibu wao, inamaanisha kuwa ni kuwatengeneza matatizo mengine.

Licha ya kwamba natambua nguvu ya serikali ni kubwa na inaweza kufanya au kuamua chochote kikubwa na wamachinga wakatakiwa kutii, lakini alichokifanya Rais Samia ni kuona tatizo kabla halijatokea.

Pia, mara zote binadamu unapomshirikisha katika kutua tatizo lake, ni rahisi sana kupata ufumbuzi ambao ni bora.

Muhimu ni kuwa hata wale viongozi wa mikoa na ngazi nyingine waliopewa maagizo na Rais kuhakikisha suala la wamachinga ninarejea katika mstari mzuri, wanatakiwa kufanya kwa usahii, tofauti na hapo watamtengenezea bomu kiongozi wetu na baadaye lije lilipuke.