Programu kama SAGCOT isambazwe sehemu zingine kuongeza tija

03Jan 2018
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Programu kama SAGCOT isambazwe sehemu zingine kuongeza tija

SENSA ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 inaonyesha kuwa asilimia 70 ya Watanzania wote ambao idadi yao sasa ni takribani watu milioni 50 wanaishi vijijini, huku asilimia 30 wakiwa mijini.

Aidha, takwimu kutoka vyanzo mbalimbali zinabainisha kwamba shughuli kubwa ya kiuchumi ya Watanzania wengi ni kilimo.

Kwamba kilimo ni sekta inayotoa ajira kwa takribani asilimia 70 ya wananchi, hasa walioko vijijini, wengi wakiwa ni wakulima wadogo wadogo wanaolima eneo la kati ya nusu ekari hadi ekari mbili.

Kwa takwimu hizi, Muungwana anaona kuwa hili basi ndilo kundi linalopaswa kupewa kipaumbele kikubwa katika jitihada za serikali za kuwakwamua Watanzania kutoka katika lindi la umaskini.

Na ndio maana hata wabobezi wa masuala ya uchumi wanakiri kuwa hali ya kipato ya wananchi ingeweza kutatuliwa vyema endapo uwekezaji mkubwa ungefanyika katika sekta ya kilimo.

Chapisho kuu la utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi lililotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2014, linaonyesha kuwa kiwango cha umaskini kilipungua kutoka asilimia 34 mwaka 2007 hadi asilimia 28 mwaka 2011.

Kwa maana nyingine kati ya Watanzania 100 kwa mwaka 2011, 28 miongoni mwao walikuwa ni maskini.

Hivyo basi, Muungwana anaunga mkono hili la serikali na wadau kutoa kipaumbele kwenye uwekezaji katika kilimo kwa lengo la kuwakwamua wananchi wengi kutoka kwenye lindi la umaskini.

Bado wakulima wengi wanatumia zana duni za kilimo kama jembe la mkono na matumizi ya mbolea bado yako katika kiwango cha chini katika baadhi ya mikoa.

Bado hawapati mbegu bora, hawapati dawa za kilimo na pia bado kilimo chao kinategemea mvua za masika ambazo upatikanaji wake kwa sasa umekuwa ni wa shida kutokana na janga la mabadiliko ya tabianchi.

Mavuno hafifu yaliyoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo mwaka jana, hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ni ushahidi wa jinsi kutegemea mvua za masika kunavyoathiri wakulima wengi.

Hata hivyo, Muungwana anakiri kuwa serikali ina programu au mipango mbalimbali katika baadhi ya maeneo yenye dhumuni la kukifanya kilimo kuwa cha kisasa, lengo likiwa ni kuwakwamua wakulima waendeshe kilimo chenye tija.

Na kimsingi mipango hiyo imeonyesha mafanikio makubwa kwa wakulima baada ya tija ya uzalishaji wa mazao kuwa kubwa.

Moja ya mipango hiyo ni ule wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania ama kwa jina jingine Mpango wa Ukuaji wa Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).

Madhumuni ya mpango huo ni pamoja na mengine kusaidia ukuaji wa kilimo; kutambua na kuchochea upatikanaji wa fedha kupitia sekta mpya za umma na binafsi, ili kuchochea maendeleo ya kilimo cha biashara.

Lakini pia kuongeza ushiriki wa wakulima wadogo katika kilimo cha biashara.

Mpango huu umeweza kusaidia jitihada za kunyanyua kilimo katika maeneo mengi ya ukanda huo unaoundwa na mikoa kama vile Morogoro, Iringa, Mbeya, Ruvuma na Songwe.

Umeweza kupeleka rasilimali fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali ambazo zimewezesha pamoja na mambo mengine kilimo cha umwagiliaji na miradi ya uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora katika maeneo hao.

Mpango huo kwa mfano umeongeza uzalishaji wa viazi kwa ekari kutoka gunia 20 kabla hadi kati ya gunia 60 na 80.

Ukiacha faida ya masoko na elimu ya uongezaji thamani wa mazao.

Muungwana anaona sasa wakati umefika kwa serikali kupeleka programu ama mpango kama huo wa SAGCOT kwenye maeneo yenye matatizo na upatikanaji wa mvua na hasa ya Kanda ya Ziwa ambako athari za mabadiliko ya tabianchi yamesababisha ukame.

Muungwana anaona miradi kama hiyo itasaidia kuwakwamua wakulima wa maeneo hayo kutoka katika lindi la umaskini.