Raia anaweza kuhoji, kukataa kukamatwa

05Oct 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Raia anaweza kuhoji, kukataa kukamatwa

SIKU zote wananchi wamekuwa wakililalamikia jeshi la polisi kwa namna linavyoendesha shughuli zake hasa wakati wa ukamataji wa raia.

Matumizi ya nguvu, ubabe na kutofuata sheria na taratibu maalum limekuwa ndiyo tatizo kubwa kwa wananchi dhidi ya askari.
Sio siri askari wamekuwa wakitumia nguvu na ubabe mno katika kuwakamata raia.

Hata pale pasipo na haja yoyote ya kutumia nguvu bado wao wamekuwa wakilazimisha nguvu nyingi hali ambayo hupelekea vurugu , kuumizana na hata mauaji.

Mara nyingi unapochunguza matukio mbalimbali ya vurugu ambayo huwahusisha raia na polisi utagundua kwa haraka kuwa ubabe wa askari ndio uliopelekea vurugu.

Basi leo nitaeleza nini ufanye askari anapokiuka taratibu hasa wakati wa kukamata au kukuweka chini ya ulinzi.

KUKAMATWA NI NINI?

Sura ya 20 Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 ndiyo sheria inayotoa mwongozo wa namna na jinsi ya kumkamata mtu.

Pamoja na hayo sheria hii haikueleza moja kwa moja nini maana ya kukamata. Hata hivyo kutokana na miongozo mbalimbali ya kimahakama ambayo hutumika kutafsiri, sheria hii tunaweza kupata tafsiri ya neno kukamatwa kwa kusema kuwa ni tendo la kumzuia kwa muda raia ambaye inatuhumiwa kwa kosa fulani, ambalo hufanywa na mamlaka husika.

Kwa tafsiri hiyo tendo la kuzuia lazima liwe la muda, raia anayekamatwa lazima awe ametuhumiwa, na pia ukamataji lazima ufanywe na mamlaka. Huo ndio utakuwa ukamataji..

MWENYE MAMLAKA

Kwanza kifungu cha 14 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinampa mamlaka askari polisi kumkamata au kumweka chini ya ulinzi raia mtuhumiwa . Hii ni kusema kuwa mamlaka ya kukamata aliyonayo askari yeyote ameyapata kutoka kifungu hiki.

Pili kifungu cha 18 cha sheria hiyohiyo kinampa hakimu yeyote mamlaka ya kumkamata raia mtuhumiwa.

Mahakimu wamegawanyika, wapo mahakimu wa mahakama za mwanzo, mahakimu mahakama za wilaya na mahakimu mahakama za hakimu mkazi.

Hawa wote ni mahakimu na wanayo mamlaka ya kumkamata mtuhumiwa kwa mujibu wa kifungu hiki.

Tatu kifungu cha 16 cha sheria hiyohiyo kinatoa mamlaka kwa raia yeyote kumkamata mtu anayetenda kosa.

Hapa tofauti ni kuwa mamlaka ya raia kumkamata raia mwenzake ni madogo na huwezekana pale tu ambapo mtuhumiwa ametenda kosa kubwa na pengine kuna wasiwasi kuwa anaweza kutoroka asipozuiliwa haraka na kwa muda huo.

Lakini, kama mazingira si haya basi raia anatakiwa kutoa taarifa polisi ili wao wenyewe ndiyo wafanye kazi hiyo.

MATUMIZI YA NGUVU

Kifungu cha 21 cha sheria hiyo kinakataza kabisa matumizi ya nguvu wakati wa kumkamata raia.

Matumizi ya nguvu ni pamoja na kumpiga mtuhumiwa , kumfunga pingu, kumshika suruali kwa kumning’iza, kumtukana au matumizi yoyote ya lugha chafu na kila kitu kinachofanana na hayo.
KUKATAA KUKAMATWA

Sheria inaruhusu raia kukataa kukamatwa askari anapokiuka taratibu.

Katika kesi ya Nzige Juma dhidi ya Jamhuri ya mwaka 1964, mahakama ilisema kuwa ikiwa mtu atakamatwa bila kufuata utaratibu basi mtu huyo anaruhusiwa kugomea ukamataji huo.

Huu ndio uamuzi wa mahakama na kwa mujibu wa sheria uamuzi wa mahakama ni sheria na hivyo maamuzi hayo ni sheria. Kwa sheria hii nitoe mwito kwa raia kutowaonea aibu askari polisi wanaokiuka taratibu ikiwa ni pamoja na matumizi ya nguvu katika ukamataji kwa kuwagomea. Ieleweke kuwa kugoma katika hili si kuvunja sheria bali ni kutekeleza sheria.

Ni haki yako kama zilivyo haki zako nyingine. Na kugoma katika hili hakuwezi kukuletea shida yoyote na hivyo huna haja ya kuwa muoga.

Kumbuka kama wewe mwenyewe hautaweza kulinda haki zako hakuna atakayelinda haki hizo kwa niaba yako. Wewe ndio unatakiwa kuwa wa kwanza kulinda na kusimamia haki zako kwa msimamo usioyumba tena bila woga huku ukiamini kuwa uko salama mbele ya sheria.

Chukua hatua sasa kwa kukataa na kugomea ukamataji uliokiuka taratibu na maelekezo ya kisheria.