Rais Magufuli afanye maamuzi pamba ya wakulima inunuliwe

16Jul 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Rais Magufuli afanye maamuzi pamba ya wakulima inunuliwe

CHANGAMOTO ya kutonunuliwa kwa pamba ya wakulima nchini ilipofikia kwa hivi sasa, ni dhahiri kwa maoni ya Muungwana kwamba ni Mtanzania namba moja kwa maana ya Rais John Magufuli ndiye ambaye anaweza ‘kuokoa jahazi’ hili.

Ikiwa inaelekea kuwa takribani mwezi wa tatu sasa toka kuzinduliwa kwa msimu wa ununuzi wa zao la pamba nchini Mei 2 mwaka huu, bado kampuni zilizopitishwa kununua zao hilo kwa sehemu kubwa hazijaanza kufanya hivyo.

Taarifa kutoka maeneo mbalimbali ya mikoa kunakolimwa zao hili zinabainisha kwamba bado wakulima wanaendelea kubaki na pamba yao majumbani mwao, na kwenye maghala ya Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) ambayo ilikuwa imeshapelekwa tayari.

Hivyo wakulima hawa ambao kwa kweli ni sehemu kubwa ya Watanzania takribani milioni 55 kwa maana ya eneo linalolima zao hili wanaendelea kupaza kilio chao, wakitaka pamba yao inunuliwe.

Wanapaza sauti zao kwa sababu kuwa wengi miongoni mwao kilimo ndiyo maisha yao na pamba ndiyo chanzo chao kikuu cha mapato ya kiuchumi na hivyo ustawi wao kwa ujumla.

Hivyo kuna wale ambao walitegemea kuwa wameuza pamba yao muda mrefu, siku za mwanzo za kuzinduliwa kwa msimu wa ununuzi, lakini hawajafanya hivyo kutokana na wanunuzi kusuasua kununua zao hilo.

Muungwana amezungumzia changamoto hii kwa takribani mwezi sasa, akisisitiza jitihada za makusudi zichukuliwe ili pamba ya wakulima inunuliwe kwa lengo la kuwawezesha kujiletea maendeleo yao.

Maendeleo ambayo mbali na kugharimia mahitaji yao ya msingi kama vile ununuzi wa vyakula, kugharimia mahitaji mbalimbali ya familia zao, yanawawezesha pia kujenga ama kuboresha makazi yao na kununua vyombo vya usafiri.

Kuna sababu mbalimbali zinazoelezwa ni kwa nini ununuzi wa zao hilo unasuasua, baadhi zikiwa ni pamoja na madai kutoka kwa kampuni za ununuzi kwamba bei ya Sh. 1,200 iliyowekwa na serikali ni kubwa.

Ni kubwa kwa maana ‘haiwalipi’ kufuatana na bei ya zao hilo katika soko la dunia, kwamba bei imeporomoka sana.

Kwamba kutokana na kushuka huko kwa bei katika soko la dunia, hata benki nchini zinasita kuwakopesha wanunuzi wa zao hilo zikihofia kuwa hawataweza kurejesha mikopo na kwa maana hiyo ndiyo huo mchezo wa kusuasua kwa ununuzi wa pamba.

Na ndiyo sababu nikaanza katika Tulonge yangu leo kwamba kuna haja sasa ya Rais Magufuli kufanya kazi yake ya ‘kuokoa jahazi’ hili la wakulima wa pamba.

Nimembainisha yeye kwa sababu ana historia ya kutatua changamoto za aina hii zinazowakumba wananchi wake na hasa wanyonge kama wakulima hawa wa zao la pamba.

Kwa mfano Novemba mwaka jana, Rais Magufuli aliingilia kati sakata la korosho ambalo linaonekana kufanana na hili la pamba.

Wanunuzi wa korosho nchini walisuasua kununua korosho wakitaka wainunue kwa bei ya chini ya Sh. 3,000 kwa kilo, hali iliyosababisha Rais Magufuli kuamuru serikali inunue korosho kwa wakulima kwa bei ya Sh. 3,300 ambayo ilikuwa na tija kwa wakulima.

Aidha, Desemba mwaka jana, Rais Magufuli alifuta kikokotoo cha mafao baada ya mfanyakazi kustaafu kilichokuwa kimependekezwa katika Kanuni za Sheria ya Mifuko ya Jamii ambacho kilikuwa kinalalamikiwa na wafanyakazi.

Kikokotoo hicho kipya kilikuwa kimeleta mkanganyiko na taharuki miongoni mwa wafanyakazi na hata wengine kukata tamaa.

Hivyo Rais Magufuli akaagiza kanuni ya mafao iliyokuwa ikitumika zamani kabla ya mifuko ya hifadhi kuunganishwa iendelee kutumika.

Ni kwa historia hiyo Muungwana ana maoni kwa Rais Magufuli kuokoa jahazi hili la wakulima, ili pamba yao inunuliwe na hivyo kuboresha ustawi wao.