Rais Magufuli mwendo wako safi, tutafika tu!

26Feb 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Rais Magufuli mwendo wako safi, tutafika tu!

Miongoni mwa mambo hayati Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alihimiza katika hotuba zake, ni umuhimu wa serikali kukusanya kodi na wananchi kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya taifa lao.

Alitamka:"Kutokusanya kodi ni sifa moja ya ‘vi-serikali corrupt’ popote pale. Popote, wala usifikiri ni Tanzania peke yake.

"Serikali ‘corrupt’ popote pale haitozi kodi. Serikali ‘corrupt’ inatumwa na wenye mali. Inawafanyia kazi wenye mali. Serikali ‘corrupt’ itamwambiaje mwenye mali kwamba utalipa, usipolipa utakiona! Atacheka tu huyu. Atakwambia ‘unaniambia hivyo wewe? kesho siji basi!

“Serikali ya wala rushwa haikusanyi kodi. Itabaki kufukuzana fukuzana na vijitu vidogo vidogo barabarani hivi basi".
Baba wa Taifa alizungumzia miiko ya uongozi na kusema:

"Zamani tulikuwa na kitu kinaitwa Miiko ya Uongozi wakati wa TANU. Zilikuwa zinaitwa Kanuni za TANU. Na kanuni moja ya TANU ambayo baadaye tukarithi katika CCM au tukairithisha CCM,inasema; Rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala sitapokea rushwa.”

"Usije ukadhani kwamba wakati wa awamu ya kwanza palikuwa hapana rushwa; ilikuwapo, lakini tulikuwa wakali sana. Siku za mwanzo kabisa, tulitaka watu wajue hivyo, tulitaka watu wajue kwamba tutakuwa wakali sana na wala rushwa ndani ya serikali na wale wanaotoa rushwa.

“Tukapitisha sheria kwamba mtu akila rushwa, eh! Kiongozi wetu anakula rushwa: anayetoa, aliyepokea, Wazanaki wanasema wote ‘manzi ga nyanza’ yaani wote wanapata msukosuko. Tunataka kiongozi anayejua hivyo ambaye atasema rushwa kwangu ni mwiko.”

Nimegusia kwa kirefu hotuba hiyo, kutokana na juhudi zinazofanywa sasa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, katika kuhakikisha kila mtu analipa kodi kwa mujibu wa sheria.

Hatua hiyo inaonyesha Rais Dk. Magufuli anatembea juu ya kauli yake katika kupambana na wafanyabiashara wakubwa wasioguswa ambao walikuwa wanakwepa kulipa kodi na kweli hilo linaonekana kutendeka.

Ninasema hivyo, kwa sababu aliahidi kufanya hivyo wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita na sasa anaendelea kufanyia kazi ahadi hiyo kwa kutambua nchi yoyote duniani huwa inaendeshwa kwa kodi.

Nakumbuka katika hotuba yake alipozindua Bunge la 11 mwaka jana, alisema ameamua kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa kodi.

Kutokana na uamuzi huo, alianza kufuta safari za nje zisizo na ulazima kwa lengo la kubana matumizi, ikiwamo kufuta sherehe mbalimbali ambazo zimekuwa zikiligharimu taifa mabilioni ya fedha.

Rais kwa kauli yake alitamka: “Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa ukusanyaji wa mapato umekuwa chini ya makadirio kwa sababu mbalimbali. Serikali ya Awamu ya Tano itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.”

Katika juhudi zake za kukabiliana na wakwepa kodi, tayari kuna waryhymiwa walioko kwenye msukosuko wa kisheria wa kuhujumu uchumi wa nchi, kupitia kodi mwaka jana.

Binafsi ninampongeza Rais Dk. Magufuli na timu yake kwa kuamua kupambana kodi zinakusanywa, kwa ajili ya maendeleo ya taifa hili na wakwepaji washughulikiwe.