Rais tuondolee kero ya usafiri Dar

14Feb 2016
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
NAWAZA KWA SAUTI
Rais tuondolee kero ya usafiri Dar

RAIS Dk. John Magufuli, ametimiza siku 100 za kuwa madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, alipopata ridhaa ya wananchi wengi kupitia sanduku la kura.

Ndani ya siku 100 tangu aapishwe Novemba 5, mambo mengi mazuri yamefanyika ambayo kwa kiasi kikubwa yanagusa maisha ya watanzania wa kawaida na kuondoa dhana ya kuwapo ongezeko la idadi ya walionacho kwa kutumia jasho la maskini; ambaye kila uchao anaishi kwa matumani kwa kukosa huduma muhimu za kijamii.

Kwa sasa tumaini limeanza kurejea kuwa inawezekana kabisa rasilimali za nchi zikatumika kunufaisha wote na siyo kundi fulani la watu, kwa kuwa kunufaika kwa mwananchi wa kawaida siyo kugawiwa fedha bali huduma muhimu kama hospitali kuwa na dawa na vifaa tiba, huduma za maji safi ya uhakika, miundombinu thabiti na kukoma kwa kero na manyanyaso kutoka kwa viongozi.

Hakika haikukosewa Dk. Magufuli kuwa rais wa tano kwani anagusa maeneo ambayo yaliogopwa, anagusa waliogeuka miungu watu, anagusa maisha ya mwananchi ambaye anaishi kwa kusindikiza wengine kwa kuwa hana hakika ya mlo mmoja kwa siku, ambaye hospitalini hana hakika ya huduma muhimu za matibabu na akishatibiwa anaelekezwa duka la kununua dawa.

Kipimo cha kuwa wananchi walishachoka na kuhitaji mabadailiko kilionekana wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa kuwa asilimia kubwa ya wananchi waliunga mkono upinzani na kueleza waziwazi kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewachosha kwa kuwa mambo yake ni yale yale, na waliamini kiongozi ajaye naye ataendeleza yale yale ya kuwasahau wananchi waliokosa huduma muhimu.

Mwandishi wa riwaya ya 'Beautful are not yet born' wa nchini Ghana alieleza kinagaubaga kile alichokiona katika nchi yake kama kukithiri kwa rushwa, unyanyasaji wa maskini, viongozi kujilimbikizia mali, ufisadi uliopitiliza huku huduma muhimu za kijamii zikiendelea kudorora.

Mwandishi wa riwaya hiyo hakuficha uhalisia wa ujumbe aliotaka kufikisha kwani alieleza kwa muundo ambao msomaji anajua inayozungumziwa ni nchi ya Ghana, ambayo ilipata Uhuru siku nyingi na ina viongozi wakongwe lakini bado ni maskini kutokana na ufisadi uliokithiri na kuweka daraja kubwa kati ya walionacho na maskini.

Yaliyomo katika riwaya hiyo inayotumiwa na wanafunzi wa kidato cha tano na sita nchini, ndiyo yaliyokuwa yanaendelea nchini, na mwandishi ni kama alilenga ujumbe wake kwa Tanzania ambayo ilifika hatua ya mambo kwenda alimradi huku kila aliye kwenye nafasi akiishi maisha ya beba chako mapema.

Kwa sasa Rais Magufuli anarejesha nidhamu na uwajibikaji wa utumishi wa umma na uwajibikaji maeneo yote, na serikalini kwa sasa siyo kijiwe au kichaka cha kujifanyia mambo ya ovyo, na tumaini lipo kuwa Tanzania mpya inawezekana.

Na kama mwandishi wa riwaya ya 'Beautful are not yet born' alivyosema, viongozi wazuri bado hawajazaliwa.
Lakini kwa nchi yetu tunao uthubutu wa kusema kiongozi mzuri amezaliwa.

Mwezi uliopita nilitembelea Afrika Kusini ambako nilikutana na waandishi na wahariri kutoka nchi za Zimbabwe, Botswana, Malawi, Kenya na Zambia ambao walifahamu habari za rais wetu na kila mmoja alisema Tanzania imepata kiongozi ambaye wanatamani wamuazime kwa muda, ili anayoyafanya nchini yakafanyike nchini mwao kwa kuwa nchi za Afrika zinafanana kwa mengi hasa ya ulafi na kutojali maslahi ya umma.

Lakini niliona jinsi Afrika Kusini ilivyojengwa kwa mpangilio huku miundombinu ikiwa ni mingi, mizuri na imara ambayo imejengwa kwa malengo ya miaka mingi ijayo. Nilijikuta naikumbuka nchi yangu na kujaribu kuhamisha miundombinu ile kwa Jiji la Dar es Salaam na kujiambia tungekuwa na barabara kama hizi kumi, foleni ingekuwa kitendawili na muda wa uzalishaji mali ungeongezeka.

Dar es Salaam ni kitovu cha nchi kiuchumi, ndiyo Jiji kubwa lenye watu wengi na shughuli nyingi za maendeleo zipo humo, ofisi zote muhimu na mapato yake ni makubwa lakini kero kubwa ni foleni isiyokwisha kwani ni kawaida mtu kukaa barabarani saa mbili hadi tatu umbali wa kusafiri kwa dakika 30.

Hivyo Rais wangu katika siku za mbeleni ambazo natarajia makubwa na mazuri, naomba ingilia kati kero hii na anza mipango ya kiutekelezaji ya kuongeza miundombinu na kuiboresha iliyopo ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kwa wakandarasi wote ambao wanajenga barabara nchini ya viwango na inaponyesha mvua kwa muda mfupi tu zinaharibika.

Ni kawaida sana kukuta barabara iliyojegwa miezi miwili iliyopita kuanza kumeguka na kuwa na mashimo, jambo ambalo linatufanya tujiulize kwanini mkandarasi huyo kafanya hivyo, ni Mtanzania na mzalendo kwa nchi yake au anajitengenezea mazingira ya kupata fedha za mara kwa mara kwa ajili ya ukarabati wa barabara husika?

Kufanya hivi ni kuitia umaskini nchi, ni sawa na nyumbani kwako uwe unanunua bidhaa zisizodumu ambazo kila baada ya miezi sita unalazimika kununua nyingine. Hii ni kujitia umaskini lakini ukinunua kitu imara utatumia kwa muda mrefu na fedha kutumika kwa shughuli nyingine za maendeleo.

Rais, pamoja na majukumu mengi uliyonayo lakini inasue Dar es Salaam kutoka kwenye dhahama hii ya ubovu wa miundombinu, mathalani barabara za mitaani ambazo zinaweza kusaidia kupunguza foleni nyingi ni mbovu sana na kipindi cha mvua ndiyo hali huwa mbaya zaidi.

Jijini mvua ikinyesha ni kawaida kusota kwenye foleni kwa saa nne hadi tano, kwa uliyetoka kazini eneo la Mwenge saa 12 na unaishi Mbagala ni lazima ufike nyumbani saa sita usiku, mahali ambako ungetumia saa moja tu kufika.

Ndiyo maana nakuomba Rais utuondolee kero hii ili uchumi uzidi kupaa kwani huwezi kuzungumzia maendeleo ya uchumi wakati kuna kikwazo kikubwa cha miundombinu inayosababisha foleni hivyo watu kuchelewa kufika katika shughuli za uzalishaji.

Mungu mbariki Rais wetu, Mungu Ibariki Tanzania.

Kwa mawasiliano; [email protected]