Ratiba Ligi Kuu maumivu kwa wachezaji

10Feb 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ratiba Ligi Kuu maumivu kwa wachezaji

MECHI ya 'dabi' ya Mwanza kati ya Alliance dhidi ya Mbao iliisha kwa sare ya bao 1-1 Jumamosi, huku wachezaji wa timu hizo mbili wakiwa hoi.

Si kwa sababu ya mechi hiyo tu peke yake, bali pia kwa safari ndefu ya kutoka Mtwara, timu zote mbili zikiwa zimefika Mwanza na kucheza bila kupumzika.

Aliiance ilifika mchana wa siku ya kuamkia mechi, lakini wenzao Mbao waliwasili Mwanza usiku na kesho yake kujitupa dimbani kucheza dhidi ya wenzao.

Wachezaji wa timu zote mbili hawakupata muda wa kupumzika, kwani Alliance Februari Mosi ilikuwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara kupambana na Ndanda FC na baada ya mechi hiyo, ikaanza safari ya kilometa nyingi kwa basi dogo kuwahi mechi dhidi ya Mbao FC.

Februari 4, mwaka huu, Mbao FC nayo pia ikawa kwenye uwanja huo huo wa Nangwanda Sijaona kucheza dhidi ya Ndanda, na baada ya mechi ikageuza kwa basi kuiwahi mechi dhidi ya Alliance iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nyamagana Mwanza.

Makocha na viongozi wa timu zote mbili baada ya mechi walilalamikia uchovu wa wachezaji wao kuwa hawakupumzika, wala kuweka miili yao sawa na badala yake wamefika tu na kukutana na mechi, huku wakiwa wametoka umbali mrefu, wachezaji wakiwa wamejikunyata garini.

Huu ni mfano wa mechi nyingi ambazo zinachezwa baada ya siku mbili au tatu, huku timu zikisafiri umbali mrefu na kusababisha hata mechi zenyewe zisichezwe kwenye kiwango halisi kinavyotakiwa.

Cha kujiuliza hata wasafiri wa kawaida tu wanapotoka kwenda mikoa ya mbali wanapofika wanakuwa wamechoka kwa safari na kuhitaji kupumzika, vipi iwe kwa wachezaji ambao wao wanafika tu na wanatakiwa kucheza?

Kuna watakaosema kuwa mbona Ligi za Ulaya wanacheza mfululizo, timu inacheza Jumanne Ligi ya Mabingwa na Jumamosi inacheza Ligi Kuu, lakini ikumbukwe kwa wenzetu wana miundombinu mizuri, lakini wana uwezo mkubwa kipesa, kiasi cha kuweza kusafiri kwa ndege ili kutowachosha wachezaji wao.

Inatakiwa wachezaji wa Tanzania wacheze mechi nyingi, lakini si zikiwa karibu karibu, huku baadhi ya timu zikiwa zinatoka mbali kwa kusafiri umbali mrefu kwenda kucheza na timu nyingine.

Ndiyo maana kuna baadhi walipendekeza mechi ya Alliance na Mbao basi ingechezwa Nangwanda Sijaona huko huko kwa sababu zote zilikuwa huko, lakini navyojua hii haipo kwenye kanuni ya ligi.

Najua tatizo kubwa hapa ni kwamba Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) wanakimbizana na muda wa fainali za Kombe la CHAN zitakazoanza Aprili 4 hadi 25, mwaka huu nchini Cameroon, lakini inawaumiza mno wachezaji kwani ni hawa hawa ambao wanakimbizwa mchakamchaka huu, baadhi yao wanatakiwa kuingia kambini kwa ajili ya michuano hiyo, hivi kweli wanaweza kwenda kucheza kwa viwango vyao kweli huko CHAN?

Halafu hapo hapo wanatakiwa kurejea tena bila kupumzika, mwezi Mei wanaendelea kumalizia mechi za Ligi Kuu, hapa naona wachezaji hawatendewi haki.

Wanafanywa kama matrekta ambayo ni chuma na yanatumia mafuta, wakati wao ni binadamu wanatumia damu na nguvu za miili yao, wakati wanahitaji pia kupumzika ili miili irejeshe nguvu.

Sitaki kuwaingilia sana TPLB kwenye ratiba zao, lakini ukweli utabaki pale pale kuwa kwa ratiba hii jinsi ilivyo inachosha sana na kuwaumiza wachezaji na kuwafanya wasicheze kwenye viwango vya kawaida.