RC Dar azuru, abadilishe maisha Uwanja wa Fisi

29Jun 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
RC Dar azuru, abadilishe maisha Uwanja wa Fisi

DAR ES SALAAM ni miongoni mwa majiji yenye makazi ya walalahoi likiwamo la Uwanja wa Fisi, sehemu yenye watu wengi wenye maisha duni, wakila vyakula kama ngozi za wanyama na bidhaa zilizoisha muda wa matumizi.

Wakazi wake wanaishi katika umaskini, na wengi wanashindwa kumudu chakula bora na mavazi.

Mazingira hayo yanawalazimisha kutegemea vyakula vya bei nafuu na wakati mwingine huuziwa bidhaa ambazo zimeharibika baada ya kupitisha muda wa matumizi.

Ni kutokana na unafuu wake au kutoelewa athari zake kiafya.

Maduka mbalimbali na wafanyabiashara wanauza bidhaa kulingana na mahitaji na uhalisia wa maisha ya wakazi au wateja wao ili kila mmoja apate anachohitaji.

Kwa mfano, madukani sukari, chumvi, majani ya chai na unga vinapimwa na kufunganywa katika karatasi kwa kipimo tofauti ili kuuzwa kwa bei ambayo mteja anaimudu.

Hata mafuta ya kula nayo yana vipimo vidogo ili kuwapa wateja bidhaa kwa thamani ya fedha zao.

Lakini mbaya zaidi, ni kuwapo kwa biashara ya ngono muda wote wa saa 24, hali ambayo inaongeza hatari zaidi kwa wakazi wa eneo hilo.

Ni kutokana na kuambukizwa maradhi ya ngono ukiwamo UKIMWI, mimba za utotoni kwa watoto, maradhi ya kama homa ya ini yote hayo yakienea kwa njia ya kukutana kwa majimaji za mwili.

Ipo haja ya kuchukua hatua madhubuti za kuokoa jamii ya hapo kwa kuipa elimu na kuihamasisha kubadilika.

Wapo baadhi ya viongozi wa serikali na wanasiasa ambao wamewahi kufika eneo hilo na kutoa ahadi mbalimbali za kuliboresha eneo hilo lakini bado hawajazitekeleza.

Utashi wa kisiasa unahitajika ili kubadili matumizi ya eneo kama njia mojawapo ya kumaliza changamoto hizo na kubadili maisha ya Watanzania hao.

Ingekuwa ni vyema kama kutakuwa na uamuzi wa kweli wa kufanya mabadiliko ya matumizi ya eneo hilo badala ya wanasiasa kupita wakati wa kampeni za uchaguzi na kutoa ahadi ambazo hazitekelezeki.

Kwa mfano aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, aliwahi kuahidi kuwa nyumba zote za eneo hilo zitabomolewa na kujengwa viwanda vidogo.

Makonda katika ahadi yake alisema, anasubiri wafanyabiashara wapatikane ili kuanza utaratibu wa kulipa fidia kwa kaya zote za 'Uwanja wa Fisi', ili kuwe na sura mpya.

Hiyo ilikuwa ni Novemba mwaka 2016, lakini hadi sasa eneo hilo limeendelea kubaki kama lilivyo, ndiyo maana kuna haja ya awamu ya sita kulitazama upya na kufanya mambo mapya Uwanja wa Fisi.

Maana yangu ni kwamba, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wa sasa, anaweza kuendeleza mkakati huo ulioachwa na Makonda, ili ahadi hiyo itekelezwe kwa vitendo kama sehemu ya uamuzi wa mkoa.

Ni vyema mkuu wa sasa mkoa akapita eneo hilo kujionea hali ilivyo eneo hilo, ili kama itawezekana afanye kama ambavyo Makonda alikuwa amekusudia, au aangalie njia nyingine ya kunusuru wakazi wa 'Uwanja wa Fisi'.

Kwa jumla kumekuwapo na ahadi mbalimbali za kuboresha eneo hilo, lakini haijajulikana ni nini kinakwamisha utekelezaji wake, hivyo ni vyema utashi wa kisiasa utumike kumaliza changamoto iliopo eneo hilo.

Ninaamini kwamba, ni matamanio ya watu wengi wa eneo hilo kuona likiboreshwa, kwani hata Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Muungano ambao eneo hilo liko ndani yake, Joseph Mkunde, anatamani hivyo.

Kiongozi huyo anasema, anasikitika kuona matamanio hayo bado hayajazaa matunda, na kushauri kila liwezekanalo kuhakikisha wenye nyumba wa eneo hilo wanalipwa ili kupisha matumizi mengine ya Uwanja wa Fisi.

Ninaungana naye katika hilo, kwani kama kutajengwa viwanda vidogo, itakuwa ni rahisi kuongeza ajira na ikiwezekana, wale wanaofanya biashara ya ngono wapewe kipaumbele ili waachane na kazi hiyo.

Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuzua ukahaba, lakini pamoja na hayo, njia mojawapo ambayo ingesaidia, ni kubadili matumizi ya eneo hilo ikiwamo kujenga viwanda vidogo kama ambavyo Makonda alikuwa ameahidi.