RC Makonda na wenzake watatue vizuizi vitambulisho vya Machinga

04Jun 2019
Moses Ismail
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
RC Makonda na wenzake watatue vizuizi vitambulisho vya Machinga

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametangaza vita dhidi ya wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama ‘Machinga’ wanaofanyabiashara katika mkoa huo bila ya kuwa na vitambulisho vilivyotolewa kwa ajili yao maarufu kama vitambulisho vya wamachinga.

Makonda alisisitiza wiki iliyopita kuwa wafanyabiashara wasio na vitambulisho wachukue jitihada za kuvipata kufikia jana (Juni 3), vinginevyo hawataruhusiwa kufanya biashara zao pamoja na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.

Hii inatokana na kile kinachoonekana kupungua kwa kasi ya Wamachinga wanaojiandikisha ili kupatiwa vitambulisho hivyo, vinavyowapa uhuru wa kufanya biashara zao katika eneo lolote la nchi hii linaloruhusiwa.

Zoezi la kutoa vitambulisho hivyo kwa malipo ya Sh. 20,000 kwa kila kitambulisho, lilizinduliwa na Rais John Magufuli kwa kugawa jumla ya vitambulisho 670,000 kwa mikoa yote ya Tanzania Bara.

Kila mkoa ulipewa vitambulisho 25,000 ili viwafikie wajasiriamali wote wenye mitaji chini ya Sh. milioni 4 na hivyo kuongeza wigo wa kukusanya mapato ya serikali.

Mbali ya lengo hilo, vitambulisho hivyo pia vilitolewa kwa nia ya dhati kabisa ya Rais Magufuli ya kuona kuwa wafanyabiashara wote wadogo nchini wanafanya shughuli zao kwa uhuru na kwa hali ya kistaarabu kinyume na ile hali ya mikikimikiki ya kukimbizana na Mgambo. 

Tofauti na mikoa mingine, Dar es Salaam ulipewa vitambulisho vingi zaidi, kiasi cha vitambulisho 175,000 kwa kuzingatia ukweli kuwa ndio mkoa wenye wamachinga wengi, ikilinganishwa na mikoa mingine.

Kinyume na matarajio ya serikali, si kwa Dar es Salaam tu, zoezi la 'ugawaji' vitambulisho hivyo linaonekana kusuasua na hilo limewafanya baadhi ya wakuu wa mikoa kubuni mbinu za kuhakikisha zoezi halikwami ndani ya himaya zao.

Iwapo kila mkuu wa mkoa atafanikiwa kugawa vitambulisho vyote 25,000, kwa malipo ya Sh. 20,000, atakuwa ameiwezesha serikali kuingiza jumla ya Sh. milioni 500, wakati mkoa wa Dar es Salaam ukitarajiwa kuingiza jumla ya Sh. bilioni 3.5 kwa vitambulisho vyake 175,000.

Ni ukweli kwa mujibu wa Muungwana kwamba wamachinga walio wengi  hawajaweza kununua vitambulisho hivyo kutokana na sababu mbalimbali.

Kuna wanaolalamikia urasimu wa upatikanaji wa vitambulisho hivyo, wakati wakuu wa mikoa wakitaka kuhakikisha wamachinga wanapata vitambulisho.

Na ndiyo maana wakuu wengine wa mikoa wamefikia hatua ya kutaka kuviuza vitambulisho hivyo hata kwa kada zisizohusika, wakiwamo waandishi wa habari.

Hii ni ishara kuwa kuna tatizo katika utekelezaji wa zoezi hilo.

Muungwana anaona kuwa njia nyepesi ya kutatua kinachokwamisha kununuliwa kwa vitambulisho hivyo ni kwa pande zinazohusika, yaani serikali na wamachinga kukaa pamoja na kujadiliana.

Lengo likiwa kubaini changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi wenye tija.

Rais alipozindua mpango huo, Desemba 10 mwaka jana, ulionekana kupokewa kwa furaha na wamachinga wengi kwani ni suluhu ya ‘dhahama’ ya kushikana mashati baina yao na Mgambo na kuirasimisha sekta yao.

Ni maoni ya Muungwana kwamba kuwachukulia wamachinga kama watu wabishi wasiotaka kufuata utaratibu bila ya kusikiliza sababu wanazotoa juu ya tatizo hilo, kunaweza kusaidie upande wowote na hivyo kufisha lengo lililokusudiwa na Rais Magufuli.

Na ndiyo maana ninasema changamoto zinazojitokeza sasa zitafutiwe mbinu za kuziondoa, badala ya ‘kutunishiana misuli.’

Ninasema hilo halitosaidia upande wowote na hasa kwa wamachinga ambao kabla ya kuingia kwa serikali ya awamu ya tano walikuwa kwenye mapambano ya ‘kudumu’ dhidi ya mamlaka zenye dhamana ya kusimamia sekta ya biashara.

Utulivu wa sasa unaoruhusu wamachinga kufanyabiashara zao kwa salama ni tunu kubwa kwa serikali ya awamu ya tano na unapaswa kulindwa kwa majadiliano na si kurudi tena katika zama za kutumia nguvu za Mgambo.