RC Malima ‘komaa nao’ tu hadi waziteme

06Dec 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
RC Malima ‘komaa nao’ tu hadi waziteme

MKUU wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amewapa siku saba viongozi wa vyama zaidi ya 85 vya ushirika, wanaotuhumiwa kufuja fedha zaidi ya Sh. milioni 105 kuzirejesha mara moja.

Alitoa agizo hilo baada ya kupokea ripoti kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu kuwapo ufujaji wa fedha zaidi ya Sh 105 milioni katika Amcos, zaidi ya 85 mkoani mwake na kumfanya acharuke na kuagiza wahusika wazirejeshe.

Malima anasema, vitendo hivyo vya ubadhirifu na ufujaji wa fedha za ushirika vinavyofanywa na viongozi vinarudisha nyuma juhudi za serikali, katika kumkomboa kiuchumi mwananchi wa kawaida.

Anasema, ushirika ukitumika vizuri utakuwa ni mkombozi mkubwa wa wakulima, na kwamba serikali haiwezi kuwavumilia viongozi wa aina hiyo, ambao wanatumia jasho la wananchi kwa manufaa yao.

"Lengo kuu la ushirika ni kuwasaidia na kuwainua wanachama kupitia kwenye ushirika baada ya mauzo ya mazao na bidhaa zao na michango mbalimbali kwa mujibu wa makubaliano yao," anasema Malima.

Mkuu huyo anasema, anafanya jitihada za kuimarisha sekta ya ushirika, ili iwe mojawapo ya zile zitakazosaidia kuleta mapinduzi ya kiuchumi, akianzia kuimarisha kilimo cha pamba na kahawa, kisha uvuvi na madini.

Hivyo, anasema hawezi kukubali kuona kuna watu wanamkwamisha wakiwamo hao wanaotuhumiwa kufuja kiasi hicho cha fedha, amewapa siku saba kuhakikisha kwamba wanakirejesha mara moja.

Mkuu huyo wa mkoa amechukua hatua hiyo huku tayari kukiwa na wito wa kuimarisha udhibiti wa ndani katika vyama vya ushirika, ili kuondoa wizi unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji wa vyama hivyo.

Wito huo ulitolewa Oktoba mwaka huu na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), alipowasilisha ripoti ya ukaguzi wa vyama hivyo kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Ripoti hiyo ilikabidhiwa kwa Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dk. Titus Kamani, jijini Dodoma na kisha Makamishna wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania wakaijadili.

Katika mjadala wao, nao wakashauri COASCO na TCDC kuboresha ushirikiano uliopo kwa ajili ya udhibiti katika vyama vya ushirika ili kuondoa tatizo la wizi na ufujaji wa fedha kwenye vyama hivyo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Brigedia Jenerali John Mbungo, baada ya kupokea ripoti hiyo, alitangaza vita kwa wanaotafutana fedha hizo.

Alizitaka taasisi na mashirika yote yaliyotafuna fedha za vyama vya msingi vya ushirika kuzirudisha haraka iwezekanavyo na kwamba wasipofanya hivyo, watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Baadaye aliujulisha umma wa Watanzania kupitia vyombo vya habari, kuwa viongozi 52 wa vyama vya ushirika mkoani Lindi walinaswa kwa kushindwa kuwalipa wakulima wa korosho Sh. milioni 436.

Hatua zinazochukuliwa na viongozi mbalimbali akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Mara, kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la ufujaji wa fedha za Amcos ni za kuungwa mkono na wapenda maendeleo.

Ninasema hivyo, sababu moja ya vyanzo vya migogoro katika vyama vya ushirika kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini, ni ufujaji wa fedha unaofanywa na baadhi ya viongozi wasio waaminifu.

Hivyo, RC Malima aendelee kuwakomalia hao viongozi wanaotuhumiwa kufuja fedha zaidi ya Sh. milioni 105 za vyama vya ushirika, ili hatimaye wazirejeshe mara moja kama alivyoagiza.

Ushirika hauwezi kuwa na maana kama wanachama wataendelea kuibiwa na viongozi wao, ambao kwa namna moja au nyingine wanaweza kuharibu dhana ya ushirika ambayo inalenga kumkomboa mkulima.

Kimsingi ni kwamba wanaotuhumiwa kufanya ufujaji wa fedha za vyama watambue kuwa wanavuruga umoja na mshikamano wa wanachama kwa maslahi yao binafsi, hivyo ni muhimu wakaepukwa.

Ushirika hauwezi kuwa na maana kama wanachama wataendelea kuibiwa na viongozi wao, ambao kwa namna moja au nyingine wanaweza kuharibu dhana ya ushirika, ambayo lengo lake ni kumkomboa mkulima.

Ikumbukwe kuwa ushirika ni kwa maendeleo ya wanachama, chama na hata taifa kwa ujumla, hivyo wanaouvuruga kwa njia yoyote ile, hawana budi kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.