RC Malima na staili yake kuinua uchumi eneo lake

03Jul 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
RC Malima na staili yake kuinua uchumi eneo lake

MARA unatajwa kuwa miongoni mwa mikoa yenye fursa nyingi za kiuchumi, kutokana na rasilimali mbalimbali zilizopo, lakini wakazi wake bado hawajanufaika na uwepo wa fursa hizo.

Miongoni mwa fursa hizo za kiuchumi ni Ziwa Victoria maliasili nyingi zikiwamo madini, vivutio vya utalii, ardhi nzuri ya kilimo na maeneo ya uvuvi, ambazo zinahitaji uwekezaji.

Hiyo ni kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima, ambaye sasa anawataka wakurugenzi watendaji wa halmashauri za Tarime, Serengeti, Bunda na Musoma kutenga maeneo kwa ajili ya wawekezaji.

Uwekezaji anaouzungumzia ni wa ndani, hasa kwa kujenga hoteli za kitalii za gharama nafuu, lakini zenye viwango na hadhi ya kitalii, kwamba hatua hiyo itasaidia kukuza uchumi wa maeneo.

Alitoa wito huo alipozindua kituo cha biashara cha kidijitali cha mkoa na kusema, hoteli za ndani ya hifadhi ni za gharama kubwa, hali inayosababisha watalii wa kipato cha kati na chini kushindwa kumudu gharama hizo.

"Hivyo, kujengwa hoteli zenye hadhi ya kitalii lakini zenye gharama nafuu nje ya hifadhi hiyo kutasaidia kuongezeka kwa watalii ndani ya hifadhi hiyo huku wakazi wa mkoa wakinufaika zaidi kiuchumi," anasema Malima.

Aidha, anawataka wafanyabiashara mkoani humo kuhakikisha wanautangaza mkoa wao pamoja na fursa zilizopo, ili zitambuliwe ndani na nje ya nchi, kwa manufaa ya wakazi wa Mara na taifa kwa ujumla.

Nikirejea hoja ni kwamba, hilo ndilo lengo kuu la serikali imekuwa ikihimiza kila wakati, kuhusu uwekezaji wenye lengo la kunufaisha wananchi wanaoishi kwenye eneo jirani, pia katika sura pana ya kitaifa.

Mkuu wa Mkoa, anahimiza uwekezaji katika mkoa wake. Hivyo waliopewa jukumu la kuandaa maeneo kwa ajili ya kazi hiyo, hawana budi kuzingatia hilo, kwa manufaa ya wana- mkoa kwa ujumla.

Vilevile, wafanyabiashara waliopewa jukumu la kuutangaza mkoa huo na fursa zake, nao wanapaswa kuufanya kuwa sehemu yao, ili lengo la kuwainua wananchi hao mkoani kiuchumi kwa kutumia rasilimali za mkoa wao, litimie.

Ni kwa kufanya hivyo kila mahali, Tanzania itaendelea kuongoza katika uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki, kama ilivyo sasa, kwa kuvutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.18.

Hiyo inatokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali kuvutia wawekezaji, hata kukapigwa hatua kukilinganishwa na nchi nyinginezo za Afrika Mashariki.

Wakati Tanzania inaongoza, Uganda inatajwa kufuatia ikiwa na uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 700, huku Kenya ikiwa na Dola za Marekani milioni 670.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika moja ya taarifa zake za Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za ofisi yake, anasema:

"Taarifa ya Uwekezaji ya Dunia (World Investment Report) ya mwaka 2018 inayotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) imebainisha kiasi hicho kikubwa cha uwekezaji. “Taarifa nyingine ya “The Africa Investment Index (AII) 2018.”

Hapo inaonyesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 13 kati ya nchi 54 za Afrika katika kutoa fursa za masoko na vivutio vya uwekezaji.

Anasema, uhamasishaji wa miradi ya kisekta ndani na nje ya nchi, umefanikisha kuvutia uwekezaji kwenye sekta mbalimbali za kimkakati na unatarajia kuwekeza mitaji ya jumla ya Dola za Marekani bilioni 1.84 na kuzalisha ajira mpya 15,491.

Kwamba hadi kufikia Februari, 2019 miradi mipya 145 ilisajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), na 104 ambayo ni sawa na asilimia 72 inamilikiwa na wawekezaji wa ndani.

Pia, kuna miradi 38 sawa na asilimia 26 inamilikiwa na wawekezaji kutoka nje na miradi mitatu sawa na asilimia 2.01 ni ya ubia.

Hii inaonyesha ni jinsi gani uwekezaji ulivyo na umuhimu kwa maendeleo ya watu wa maeneo ambayo uwekezaji unawekwa, lakini ukilenga kunufaisha pande zote ikiwamo wananchi, mwekezaji na serikali.