Roho ya ujinga imewatapeli wanawake wengi

16Jul 2017
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
Maisha Ndivyo Yalivyo
Roho ya ujinga imewatapeli wanawake wengi

MPENZI msomaji, tunaendelea na shuhuda jinsi roho ya ujinga inavyotesa kinamama. Hebu wasikie wafuatao;- Mimi imenigusa sana hii roho ya ujinga. Mume wangu nilikuwa nampenda sana. Yeye alikuwa hanipendi nilikuwa naishi naye basi tu.

Mtu mwenyewe alinizalisha watoto watano.

Basi akapata mwanamke mwingine akahamia huko akaniacha na mtoto wangu wa mwisho na mali ambazo ni nguruwe nane na ng’ombe za kulima.

Sasa zile ng’ombe nikashtuka mapema nikaagiza ndugu zangu waje kuzichukua kwa sababu huyu mimi simuelewi kwani sasa hivi hata kuchunga anakataa. Wakaja kuzichukua wakaacha zile nguruwe nane.

Mimi nikawa naumwa wakanipeleka hospitalini na kulazwa nilikuwa na mimba ya miezi saba. Wakatumwa askari wakamfuata pale nyumbani walipompata wakamuuliza kwanini huyu mwanamke umemtelekeza kwa sababu ana mimba? Halafu hali yake siyo nzuri.

Basi akaja siku moja na alipokuja akanitolea damu, waliponiwekea damu ile hakurudia tena, mpaka nimejifungua kwa upasuaji mpaka sasa hivi nilipo niko peke yangu naishi na watoto wangu wote na mwenyewe yuko huko huko hajarudia tena mpaka leo. Na nguruwe zile amekula peke yake.

Mwingine anasema;- Nikiri kwamba maendeleo kidogo niliyo nayo leo ni kwa sababu ya kudanganywa na watu. Mimi nina roho ya kuamini watu hata kama akija na kuniambia kitu nakiamini. Kama ni pesa nimkopeshe na sina historia ya kumkopesha mtu pasa akanilipa yote.

Hata akinilipa ni lazima ibakie kiasi mkononi mwake hata kama ni kidogo. Nimedanganywa mara nyingi lakini namba niseme uwongo ambao umenitokea.

Wa kwanza nilidanyanywa na mpendwa. Mimi napenda kuvaa nguo za kitenge . Naweza kuvaa nguo moja leo nikaja kuirudia baada ya miezi mitatu. Sasa kuna dada mmoja tuko naye akaniambia usiwe unavaa nguo nyingi, naomba tufanye biashara ya nguo.

Aliponishawishi nikaona ni biashara nzuri. Mimi nilichofanya ni kuchukua zile nguo zangu na kuziweka kwenye mabegi yakajaa akaniambia nakwenda kuziuza Nairobi. Na tangu alipotoka hakurudi tena. Ni nguo nyingi, ikabidi nianze tena upya kununua nguo.

Uwongo mwingine umetokea kwenye mtandao. Naomba niwasihi watu wote wanaotumia facebook, whatsapp. Kuna mtu aliwasiliana nami kwenye facebook akajifanya yeye ni mzungu. Kwa hiyo nikaanza urafiki kidogo kidogo. Tukawa marafiki sana.

Sasa baadaye akaniambia yeye anafanya kazi UNHCR(Shirika la Umoja wa mataifa linalohudumia wakimbizi) na hayupo nchini hivi sasa amerudi kwao. Akawa ameniambia kwamba amenipenda ni mwanamke. Akaniuliza una watoto nikamwambia ndio ninao.

Akaniambia najisikia kuwa-adopt watoto wako, nikamwambia sasa ukiwa uko tayari niambie kwani natamani maisha ya ulaya, natamani watoto wangu siku moja waishi maisha ya ulaya. Nikakubali kwani tulikuwa marafiki sana.

Baadaye akisema hivyo kwamba yuko nje, akaniambia nataka nikukabidhi nyumba yangu ambayo nilimwacha mlinzi na mbwa wangu wawili. Nikasema sawa. Nikamuuliza mimi niko Dar nitawezaje kuisimamia nyumba yako ambayo iko Arusha?

Akasema mimi nitakuwa nakutumia pesa na wewe unamtumia mlinzi anaendelea kuitunza halafu wewe siku moja moja uwe unaenda.

Nikasema sawa. Siku moja akanipigia simu akaniambia nayo dharura nitumie fedha. Nkamuuliza dharura ya kiasi gani? Akaniambia mbwa wangu wamekosa chakula nahitaji utume hela kwa mlinzi awanunulie mbwa chakula.

Nikasema mbona hapa nilipo sina pesa. Akaniambia tafta kiasi chochote halafu nitarudisha jioni hiyo pesa. Akaniuliza hapo una shilingi ngapi, nikamwambia mimi nina shilingi 50,000/= , akaniambia itume hiyo hiyo.

Akaniambia nakupa namba ya mlinzi. Yaani tatizo langu ni kwamba mtu yoyote akiniambia nina shida, tayari hiyo shida yake itakuwa ni yangu, nitaibeba.

Akanipa namba ya simu ya mlinzi, nilipopiga ikapokelewa na mtu anayeongea sauti ya kimasai. Hajui Kiswahili kabisa. Kumbe ni yeye huyo huyo amebadilisha sauti akajifanya ni mmasai wakati siyo mmasai.

Basi nikaituma ile pesa kwake. Nilipoituma akanitumia meseji yenye orodha ya magari. Akaniambia chagua moja ya haya magari uniambie. Nikamwambia nataka Freelander kwa kuwa ni gari niipendayo sana.

Akaniambia kama umeipenda hiyo tuma hela laki tano nitakupa na dereva akuletee Dar. Ikabidi niende kuazima hiyo hela. Kaka mmoja namfahamu nikamwendea ili aniazime, lakini yeye akanitahadharisha akaniambia usiitume utatapeliwa.

Nikamwambia hapana, wewe nipe hiyo hela, nitakulipa mimi. Akasema hapa sikupi, nenda katafute hela yako mwenyewe umpe.

Akakataa kabisa. Wakati nafikiria nini cha kufanya, roho ikashtuka, nikampigia simu mume wangu nikamwambia kuhusu hilo jambo, akaniambia acha na nisisikie hadithi hiyo tena. Basi nikawa kama wananitishia nikaacha.

Ikabidi nimwambie yule mtu, nikampigia simu. Nikamuuliza mbona naona kama huu mchezo ni wa kitapeli? Nilipomwambie vile tu, akani-block (akafunga mawasiliano). Maisha Ndivyo Yalivyo.

Je, unalo suala la kifamilia/ndoa/mahusiano linalokutatiza? Wasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; [email protected] au [email protected]