Ruvu kuweni wapole, kanuni mlipitisha wenyewe

17Feb 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ruvu kuweni wapole, kanuni mlipitisha wenyewe

MATUKIO haya mara nyingi hutokea kwenye Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, lakini safari hii limetokea kwenye Ligi Kuu na ndiyo maana mashabiki wengi wameonekana kushangaa.

Msimu huu kwenye Ligi Daraja la Kwanza kuna timu imepokwa pointi baada ya kutokuwa na gari la wagonjwa kwenye uwanja wake wa nyumbani na wageni kupewa pointi.

Halikuzungumzwa kwa sababu mashabiki wengi hawafuatilii. Sasa limetokea kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara. Jumatano iliyopita Prisons ya Mbeya ilipewa pointi tatu na magoli matatu baada ya gari la wagonjwa kukosekana kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Nilisema kukosekana siyo kwamba halikuja kabisa, ila liliwasili dakika mbili baada ya muda wa nusu saa wa kusubiri uliowekwa kumalizika.

Ina maana liliwasili nje ya muda, hivyo Prisons wakaondoka uwanjani.

Hali hii ilizua sintofahamu, kila mmoja akiongea lake, lakini Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, katika kikao chao wiki hii, kiliizawadia Prisons pointi tatu na magoli mawili kutokana na Ruvu Shooting kuvunja kanuni hiyo.

Ni kanuni iliyopitishwa msimu huu wa ligi. Ni kwamba timu yoyote mwenyeji ndiyo ina wajibu wa kuleta gari la wagonjwa na vijana waokota mpira viwanjani.

Klabu yoyote ile ikikiuka maagizo haya, basi mwamuzi hatakiwi kuchezesha mechi hiyo, na timu ngeni itapewa ushindi wa pointi tatu na magoli matatu.

Na ndicho kilichotokea. Nimeona viongozi wa Ruvu Shooting wakilalamika sana juu ya hili.

Lakini ukisikiliza malalamiko yao yanalenga sana kwenye ubinadamu na si kanuni.

Wanadai gari la wagonjwa halikuwapo kwa wakati kwa sababu lilipeleka mgonjwa kwenye Hospitali ya Tumbi. Ni kweli, lakini hili haliwezi kufanya kanuni ya soka ibadilishwe.

Kanuni inamtaka mwamuzi asubiri gari hilo kwa muda wa nusu saa baada ya muda ambao mpira ulitakiwa kuanza.

Dakika moja baada ya nusu saa mwamuzi anatakiwa kuvunja pambano. Vyovyote itakavyokuwa ni kwamba kanuni imevunjwa na Ruvu Shooting hawana cha kujitetea na inabidi tu wakubali, waangalie mbele na kujifunza kutokana na hili lililotokea.

Ni kwamba kanuni hizi zilipitishwa kabla ya Ligi Kuu kuanza na viongozi wa klabu zote, hivyo kwao hapo hakukuwa na kipya wasichokijua. Na kama walikuwa hawajui, basi hilo ni tatizo lao.

Mara nyingi kanuni hizi hutungwa na kupitishwa kabla ya msimu mpya wa ligi kuanza.

Shirikisho la Soka Nchini (TFF) huwataka viongozi wa klabu kupeleka mapendekezo yao, lakini baadaye hupewa kuyapitia na kuyafanyia marekebisho yale ambayo wanaona yanaweza kuleta matatizo, au hayatekelezeki.

Lakini mara nyingi viongozi wa baadhi ya klabu hupuuza kupeleka maendekezo au kuyapitia na matokeo yake, kanuni hizi zinapokuja kutumika ndipo wanaposhtuka na kushangaa.

Vile vile wapo baadhi ya viongozi wanapopitisha mapendekezo haya hawadhani kama yatawakuta wao, badala yake wanaona kuwa wenzao ndiyo wanaweza kuathirika, sasa linapowakuta wanaanza kulalamika kana kwamba ndiyo wanaziona kwa mara ya kwanza kanuni hizo.

Kwa kuwasaidia tu viongozi wa Ruvu Shooting kama wanaona kanuni hiyo haina tija basi msimu ujao wapambane kuiondoa na kuleta kanuni mbadala, lakini kwa sasa hawakwepi mkono wa adhabu, ili iwakumbushe na klabu zingine kuwa kuna aina hiyo ya kanuni ambayo waliipitisha wenyewe na inafanya kazi.