Saa ya mkononi inavyompamba mwanaume

27Feb 2016
Moshi Lusonzo
Nipashe
Mtindo
Saa ya mkononi inavyompamba mwanaume

SAA ya mkononi ni pambo linalopendwa kutumiwa na wanaume katika mazingira tofauti.

Kwa mujibu wa wataalam wa historia wanasema, matumizi ya saa yalianza miaka mingi iliyopita. Kipindi hichi ilionekana kama kifaa muhimu cha kutunza muda katika makazi ya watu na mahekalu ya ibada.

Lakini teknolojia ilivyozidi kukua, matumizi yake yaliboreshwa baada ya watu kuanza kuvaa mikononi kama pambo muhimu katika mwili.

Kutokana na mahitaji yake kuongezeka, viwanda na wabunifu wameongeza nguvu katika uvumbuzi wa aina mbalimbali za saa pamoja na kutumia madini ya gharama kwa ajili ya kuwavutia wateja.

MATUMIZI
Saa ya mkononi ni moja ya vitu vinavyong’arisha na kuleta utofauti endapo mtu akiivaa.
Wataalam wa urembo wanashauri kabla ya kununua saa, chunguza ngozi yako kama inaathirika na madini ya aina gani ili kuondoa usumbufu.

Nunu yenye ukubwa unaolingana na mkono wako ili iwe rahisi kuivaa na kuivua.
Kama unapata matatizo unapotumia saa zenye madini ya shaba na chuma, unashauriwa kununua zilizotengenezwa kwa plastiki au madini kama dhahabu.

UTUNZAJI
Unashauriwa kuwa makini katika utunzaji wa saa kwa kuweka mbali na unyevunyevu au sehemu inayoweza kuvunjika.

Hakikisha unakuwa na chombo maalum cha kuweka wakati unapolala. Baadhi ya watu wanalala wakiwa na saa mkononi, jambo hili ni hatari kwa usalama wa saa yako.
Mwisho.