Sababu, umuhimu kushiriki uchaguzi serikali za mitaa- 2

02Nov 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Sababu, umuhimu kushiriki uchaguzi serikali za mitaa- 2

WIKI iliyopita tuliona kuwa ilipofika Mei 1969, ushuru wa mazao uliokuwa unatozwa na serikali za mitaa na vijiji, ulifutwa na uamuzi huo katika masuala mengi uliathiri kwa kiasi kikubwa mapato ya serikali za mitaa na vijiji nchini.

Licha ya kwamba serikali zilitegemea zaidi misaada na ruzuku kutoka serikali kuu baada ya vyanzo kadhaa vya mapato yake kufutwa, pia katika kipindi hicho hicho Hazina ilipunguza ruzuku kwa serikali hizo.

Uamuzi huo ulitokana na sababu kwamba Hazina au Serikali Kuu ilichukua baadhi ya majukumu ambayo hapo awali yalikuwa ya serikali za mitaa na vijiji. Mfano wa majukumu hayo ni kama vile ulipaji wa mishahara ya walimu wa shule za msingi wa daraja “A” na “B” na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kusomea'.

Wizara nyingine, kama ya Afya, Ujenzi na Madini nazo pia kwa wakati huo zilichukua baadhi ya majukumu ya serikali hizo hivyo tena, kupelekea upungufu wa mapato, na hatimaye halmashauri nyingi zilishindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, hali ambayo ilisababisha kujikuta katika migogoro na serikali kuu.

Kwa kifupi, madaraka mikoani au serikali za mitaa na vijiji yalirudishwa rasmi mwaka 1982 kisheria. Lengo likiwa ni kusogeza huduma zaidi za kimaamuzi kwa wananchi ili kurahisisha mbinu za kuwafikishia maendeleo.

Serikali za mitaa zinajumuisha mikoa, wilaya, vijiji na vitongoji huko wananchi wamepatiwa mamlaka ya kuchagua viongozi wao katika maeneo husika. Sanjari na kusimamia rasilimali zao kama vile ardhi, kukusanya mapato, kupanga bajeti na kusimamia matumizi.

Umuhimu wake ni kuwapatia wananchi mamlaka za kimaamuzi kupitia vikao vyao wenyewe kama vile katika halmashauri za wilaya au vijiji kupanga bajeti na kusimamia fedha zinazotolewa na serikali kuu kwa ajili ya maendeleo katika maeneo yao.

Majukumu

Mwenyekiti wa Mtaa au Kijiji kikatiba ndiye mkuu wa serikali katika ngazi hiyo.

Ana wajibu wa kuitisha na kuongoza mikutano yote ya halmashauri ya ngazi hiyo, pamoja na mikutano mikuu ya pia.

Lakini endapo mwenyekiti hayupo katika mkutano wowote, wajumbe wa mkutano unaohusika wanaweza kuchagua mwenyekiti wa muda wa mkutano huo.

Mwakilishi wa mtaa au kijiji kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata Ward Development Commetee.
Ana jukumu la kuhudumia kwa usawa wana-mtaa au kijiji wote, bila kujali tofauti za kisiasa, kijinsia au za kidini na

Anatakiwa kuwa mfano wa uongozi na utendaji bora wa kazi, kwa kuwa na shughuli zake mwenyewe za kujitegemea kimapato ambazo zinaweza kuigwa na wana-mtaa wa kijiji wenzake.

MADARAKA/ MAJUKUMU

Mkutano Mkuu wa Kijiji ndiyo unaosimamia na kuwajibisha watendaji, kuweka taratibu za namna ya kuitisha vikao vya dharura.
Kupitia Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi huwachagua wenyeviti wa kijiji na wajumbe wa halmashauri ya kijiji.

Unahusika kujaza nafasi za viongozi wa halmashauri ya kijiji zilizo wazi. Aidha, hujadili na kupokea au kukataa taarifa za utekelezaji wa shughuli za kijiji kutoka halmashauri ya kijiji.

Jukumu jingine ni kupokea, kujadili na kupitisha au kukataa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za kijiji, aidha hupokea, kujadili na kupitisha au kukataa mapendekezo ya kodi, ushuru na vyanzo vingine vya mapato ya kijiji.

Pia, hupokea na kujadili taarifa ya makusanyo ya fedha za kodi, ushuru na mapato mengine ya kijiji, kujadili na kufanyia maamuzi mapendekezo ya serikali ya kijiji ya kutunga sheria ndogo ndogo.

Kupokea na kujadili na kuyafanyia maamuzi masuala kuhusu ugawaji wa ardhi na matumizi ya rasilimali zingine za kijiji.

Kazi nyingine ni kuhoji, kudadisi, kukosoa, kukubali au kukataa taarifa na mapendekezo ya serikali ya kijiji.

Aidha, huhusika kuondoa madaraka serikali ya kijiji au mjumbe yeyote kabla ya muda wao na hupitisha azimio la kumkaripia rasmi mjumbe yoyote wa halmashauri au halmashauri kwa ujumla kwa utendaji mbovu.