Safi sana faini 50,000/-, viboko 15 kwa wazazi walevi

29May 2016
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Safi sana faini 50,000/-, viboko 15 kwa wazazi walevi

SERIKALI ya Kijiji cha Sanya, wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro, hivi karibuni imefikia umauzi wa kutangaza adhabu ya kuchapwa viboko na kutozwa faini kwa mtu yeyote atakayekutwa baa na mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya baadhi ya watu kuwachukua wanafunzi na kwenda nao baa nyakati za jioni.

Tabia hii imeshamiri kwa baadhi ya watu wilayani humo hali inayochangia wanafunzi wengi hasa wa kike kukatisha masomo yao kwa sababu ya kupata ujauzito au utoro shuleni.

Kutokana na hali hiyo kumekuwapo na ongezeko kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa sababu ya watoto wanaozaliwa kukosa matunzo kutoka pande mbili za wazazi.

Kijiji hicho kimetangaza mtu yeyote atakayekutwa na mtoto chini ya umri wa miaka 18, atatozwa faini ya Sh. 50,000 na kuchapwa viboko 15 ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Mara nyingi watu wanaofanya vitendo hivyo vya kuwaharibia watoto wa wenzao maisha, pia wana watoto nyumbani na pengine ni wakali kama pilipili wanapoona watu wengine wakiwanyatia watoto wao.

Serikali kwa kushirikiana na wanaharakati wanaotetea haki za watoto, wamekuwa wakipinga vitendo hivyo vinavyofanywa na watu wazima tena wenye akili timamu, na kutoa elimu kwa watoto ili kuwakwepa watu wa aina hiyo.

Hata hivyo, baadhi ya watoto wanaotoka katika familia duni, hujikuta wakiingia katika mtego huo, baada ya kupata vishawishi kutoka kwa watu kwa kudanganywa kuwa watawasaidia na kuondokana na shida walizonazo.

Tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira magumu, huchangiwa na tabia kama hizi zinazofanywa na watu wazima wanaoshiriki ngono na watoto na kuwasababishia kupata watoto wakiwa na umri mdogo na kuwapo kwa wimbi la utoaji mimba na utupaji watoto.

Hata wale wanaojaribu kuwatunza watoto wanaowazaa hushindwa kuwapatia matunzo bora na mwishowe huishia kuwa ombaomba mitaani.

Wanaharakati wanaotetea haki za binadamu wanapozungumzia ukatili wa watoto, hawazungumzii tu kuwapiga au kuwanyima chakula, bali hata kuwanyima haki zao za msingi kama kuwakosesha elimu, chakula, mavazi na mahali bora pa kuishi..

Uamuzi wa wakazi wa kijiji cha Sanya unapaswa kuigwa na vijiji vingine nchini kwa kuwa vitendo hivyo mara nyingi hufanyika maeneo hayo kutokana na kutotekelezwa kwa sheria mbalimbali zilizowekwa.

Watu wengine utawakuta asubuhi wakiwa kwenye vilabu vya pombe badala ya kujishughulisha na kazi za uzalishaji mali. Pombe hizo zikisha wakolea huwatuma kufanya vitendo viovu vikiwamo vya kuwatamani watoto walio na umri sawa na watoto wao waliowazaa.

Katika kutekeleza adhabu hiyo, kijiji hicho kimeamua kupiga marufuku uuzwaji wa pombe nyakati za kazi na kutoa amri kwa baa zote kuanza biashara hiyo saa 9 alasiri.

Adhabu hii pia inapaswa kuwagusa baadhi ya wazazi ambao pia hupenda kwenda na watoto wao kwenye vilabu vya pombe au kwenye baa na kushinda nao.

Watoto hao hujifunza tabia mbaya zinazofanywa na watu wazima wanapokuwa wameshalewa na hata mtoto wa aina hiyo anapokanywa ni vigumu kujirekebisha kwa sababu ya kuiga tabia zinazofanywa na wazazi wake.

Athari za pombe huleta madhara makubwa katika familia hasa kwa watoto kushindwa kupata malezi bora toka kwa wazazi wao.

Ndio maana mara kwa mara tunasoma, tunasikiliza au kuangalia kwenye vyombo vya habari matukio kadhaa ya ukatili wa watoto, wengine wakifungiwa ndani na wazazi wao wanapokwenda vilabuni.

Adhabu hii inaweza kuwa suluhisho kubwa kwa wale wazazi wenye tabia hizo na pia kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia hizo.

Tena ingekuwa vyema kama adhabu hiyo ya viboko ingefanyika hadharani ili kuwashikisha adabu watu wenye tabia ya kuharibu watoto wa wenzao.
[email protected]; Simu: 0774 466 571