Salamu za kukumbatiana ‘wauu!...’ ziachwe kwa muda

19Mar 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Salamu za kukumbatiana ‘wauu!...’ ziachwe kwa muda

KUGUSANA mwili kwa namna mbalimbali, iwe kupeana mkono au vinginevyo, mara zote inabeba ishara ya ‘yuko pamoja’ kwa upendo.

Hivyo, zile salamu kwa mtindo wa kukumbatiana, inatajwa kuwa moja ya ishara ya furaha na upendo miongoni mwa watu wa jamii. Waafrika nao tumo. Hiyo ni kawaida kwetu Waafrika, tunapokutana nyumbani, barabarani au sehemu yoyote.

Kukumbatiana na kupeana mikono, ni salamu za jadi zinazoendelea kudumishwa kwenye baadhi ya makabila ya Kiafrika, kizazi kimoja hadi kingine, tukitakiana mema maishani. Watanzania nasi ni sehemu ya hilo.

Sasa imeibuka corona, ugonjwa wa kuambukiza, unaoilazimu jamii kuachana kwa muda mambo ya kugusana pasipo lazima.

Virusi vya corona, wataalamu wanatuambia ni tatizo kubwa linaloikabili dunia na tayari serikali imeshatangaza, Mtanzania mwenzetu mmoja tayari ana virusi vyake, hali inayotupa shaka, baadhi wanaangukika taharuki.

Kabla ya kugundulika mgonjwa mwenye virusi vya corona nchini, serikali ilishatahadharisha na kuwapa Watanzania maelekezo ya nini cha kufanya, ili kujikinga na ugonjwa huo.

Hapo kuna suala la kusalimiana pasipo kugusana. Pamoja na maelekezo hayo, bado wapo baadhi ya watu hawajaanza kuzingatia hilo.

Hii inatokana na ukweli kwamba kwenye mikusanyiko ya watu ikiwamo vitu vya mabasi, baadhi ya watu wamekuwa wakisalimiana kwa kukumbatiana na kushikana mikono kama kawaida.

Wanafanya hivyo huku kukiwa na maelekezo yaliyotolewa na serikali kana kwamba ni jambo la kawaida, wakati wakijiingiza kwenye hatari aidha kwa kujua ama kwa kutojua.

Lakini, pamoja na yote, jambo la msingi ni kuzingatia maelekezo, ingawa kuna baadhi waliozoea kusubiri hadi washuhudie ndipo wachukue hatua na kumbe tayari wamechelewa.

Kwa hali ilivyo sasa, salamu za kukumbatiana zikome kwa muda, kupisha udhibiti wa kuenea corona na ndipo mambo mengine yaendelee, kuliko kung'ang'ania hatari, kuliko kung’ang’ania mbwembwe za uhusiano, sakata likiwa sehemu yake.

Viongozi wakuu wa nchi wameitikia maelekezo hayo na wameanza kuyafanyia kazi mara moja. Hivyo, sioni hivyo kwa nini wengine tubaki katika mzaha.

Mara tu baada ya maelekezo, Rais na Waziri Mkuu wametuonyesha mfano vitendo, kufuata maelekezo ya Wizara ya Afya, Meandeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kuhusu tunachopaswa kufuata kutetea uhai wetu.

Virusi vya corona vilikuwa vinatajwa katika nchi nyingine na sasa ni hapa hapa nyumbani. Ndipo swali langu la msingi linachukua nafasi yake, wale wasiotaka kuachana na salamu za kukumbatiana na kushikana mikono, wanatafuta nini?

Hadi juzi tumeona hatua zaidi za kiserikali, shule zimefungwa kwa muda. Ni jitihada za kuwanusuru wanafunzi na jamii zao dhidi ya ugonjwa huo.

Ndugu zangu, hatua hizi ziwazindue wale ambao ni wagumu kuzingatia maelekezo, walioyapa uzito maneno ya mitaani ama kwa kupuuzia au kutiana hofu bila sababu za msingi.

Mtindo wa kuchukua maeneo ya vijiweni na kuyafanyia kazi bila kuchukua hatua zinazotakiwa, ni sawa na kujiangamiza. Hivyo, kwa kuwa ugonjwa umetajwa kuwapo nchini, tahadhari kubwa zinatakiwa kuchukuliwa.

Siyo wakati wa kuambiana kuwa ‘kama Mungu amekupangia kufa kwa virusi vya corona utakufa tu’, bali kufuata maelekezo, ikiwamo kuacha salamu za kukumbatiana na kupeana mikono.

Uzembe uachwe kwenye mambo ya hatari kama hayo. Kila mmoja wetu achukue hatua kwa nafasi yake, inagawa inawezekana kuwapo changamoto, katika sura mbalimbali, kulingana na maazingira ya kila mmoja wetu.

Maelekezo kwamba watu wasikumbatiane na wasipeane mikono yasipite bure, bali yazae matunda katika vita hii dhidi ya corona.

Pia, ni vyema kukumbuka kwamba dhana ‘mazoea yana taabu’ na yanaweza kukuingiza kwenye matatizo. Ni wakati wa kuishi kulingana na mazingira na jinsi dunia inavyokwenda, kama ambavyo sasa inapambana na virusi vya corona.

Kila mmoja kwa njia moja ama nyingine ana nafasi ya kushiriki katika vita dhidi ya virusi hivyo, madaktari wanafanya sehemu yao, na wananchi kwa upande wao, wanatakiwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu hao wa afya.