Sare makonda, madereva zilivyo adhabu kwa abiria

27Jul 2021
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Sare makonda, madereva zilivyo adhabu kwa abiria

MAKONDAKTA na madereva wa mabasi ya mijini na kwenye majiji zikiwamo daladala jijini Dar es Salaam, wanakera linapokuja suala la kuvaa sare ambalo hawalizingatii licha ya kwamba ni utaratibu.

Makondakta pamoja madereva ni kama vile hawataki kuvaa sare hizo, wakati wengine wanashangaza kwa uchafu, uchakavu na kupauka kwa nguo hizo.

Mathalani, yuko anayevaa shati lenye mkono mmoja uliokatwa, wakati mwingine umeraruka, hakuna vifungo, vazi ni kubwa kuliko kipimo chake, suruali hazina zipu na muda mwingine zinawavuka, lakini cha kushangaza ndani wamevaa bukta au boksa ambazo zinaonekana.

Wakati mwingine ni kawaida sare hizo zinalalamikiwa kuwa zinanuka na miguuni madereva na makonda wanavaa makubazi au raba chafu zinazotoa harufu pia. Vijana hao hawachani nywele, lakini wana lugha mbaya na kejeli kwa abiria.

Kwa ujumla kuchezea sare kunaelekea kuwa sugu hata mamlaka za usimamizi katika hili zimepungua kasi ya kuwakemea, ikiwamo trafiki ambao kazi kubwa imekuwa ni kuwapiga faini huku Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA), zikikaa kimya kwenye usafi wa mwili.

Usafiri kafiri! Walijisemea wahenga. Usafiri huu unaonekana ni kama bora liende, daladala ni chafu, hakuna vyombo vya kuwekea taka, hata kama kipo wakati mwingine ni balaa kwa abiria vinaning’inia juu ya vichwa vyao na vimejaa taka ambazo zinanuka.

Sare hizi inavyooneka makondakta na madereva wanazo moja au wanachangia pengine ni kwa sababu zinauzwa ghali huko zinakopatikana.

Sare zinavaliwa zikiwa chafu kutoka Jumatatu hadi Jumatatu, sasa 24, siku 365 za mwaka hakuna mabadiliko yoyote.
Sare hizi ni kero kwa abiria, hasa pale kondakta anapobanana nao kwenda mbele na nyuma kukusanya nauli hasa wakiwa wamebanana kupindukia bila kujali kuwa kuna corona.

Jamii haipaswi kulikalia kimya kwani hii ni huduma kama zilivyo nyingine uvaaji wa sare hizi upo kulingana na sheria, kanuni na taratibu za usafirishaji katika usafiri wa umma.

Ushuhuda ni kwamba usafiri wa mabasi yaendayo mikoa tofauti na nchi jirani wanajitahidi kuvaa sare safi na unadhifu humvutia mteja na uvaaji wa sare haujaanzia au haupo tu kwa makondakta na madereva.

Maeneo mengi ikiwamo sare katika sekta, idara, taasisi na ngazi tofauti kwa lengo la kuongeza weledi kwenye kutoa huduma, kuweka utambulisho wa wahusika na kuongeza unadhifu.

Sare licha ya kuvaliwa na watu wengi kama polisi, wanajeshi, wauguzi, manahodha ya meli, rubani wa ndege usafi wa mavazi hayo ni muhimu ili kuhudumia wateja na kuepusha usumbufu.

Pamoja na kuzungumzia masuala ya kuweka nauli na kuainisha viwango vinavyotakiwa kutozwa kwa abiria, mamlaka wadhibiti wanawajibika pia kushughulikia usafi wa makondakta na uvaaji wa sare kikamilifu.

Hakika wananchi wanakerwa na uvaaji wa makondakta na madereva ambao huchangia pia uendeshaji wa kivurumai, matusi na lugha mbaya kwa wateja hasa linapokuja suala la kuwasindilia abiria kwenye magari bila kujali afya na usalama wao na mizigo waliyo nayo.

Heshima ya kazi ya mtu huanzia na mhusika mwenyewe ndipo wengine wataiheshimu kazi yake, mtindo wa kuzivaa nguo ambazo hazina unadhifu, shati kubwa, suruali inayoning’inia miguuni na zinazofungwa kwa kamba za mkonge achilia mbali uchafu wa mwili kunawafanya watu wasiwathamini wahusika.

Tatizo hilo la kukosa sara nalo liko kwa madereva wa pikipiki. Waendesha boda boda nao ni wachafu na pengine ni wakati wa mamlaka zinazohusika kuona umuhimu wa kuwahimiza kubadilika.