Sasa manung'uniko ya abiria yatakwisha

13Jan 2019
Sabato Kasika
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Sasa manung'uniko ya abiria yatakwisha

MABASI ya abiria ya kwenda mikoani na nchi jirani, yameanza kusafiri saa 11 alfajiri kuanzia mwaka jana, huku yale yatakayotembea usiku yakiwa wameunganishwa kwenye mfumo maalumu wa ulinzi au king’amauzi ambao kitaalamu huitwa (GPS).

Lengo la kuunganishwa ni ili mabasi hayo yaweze kuonekana katika mfumo wa Mamlaka Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, kwa lengo la kudhibiti ajali za barabarani.

GPS inadhibiti kasi ya kilometa 80 kwa saa na inapoongezeka mfumo huishusha kasi hiyo hadi kufikia 80.

Hatua ya kuruhusu mabasi kuanza safari mapema inaonekana kuwa itamaliza kama si kupunguza kilio cha muda mrefu cha abiria, ambao wamekuwa wakilalamikia kuchelewa kufika kule wanakokwenda kutokana na mabasi kumulikwa na tochi njia nzima. Leo GPS inachukua nafasi ya tochi kwani kama suala ni mwenda mkali king’amuzi kimeudhibiti.

Yaani yanachelewa kuondoka Ubungo Dar es Salaam halafu njiani yanatakiwa kwenda mwendo mdogo ambao wakati mwingine husababisha walale njiani au wafike muda mbaya kule wanakokwenda.

Kwa abiria wanaosafiri kutoka Dar es Salaama hadi Mwanza, watakuwa wamekumbana na kadhia hiyo ya kulala, Nzega, Shinyanga, au kufika Mwanza kati ya saa 6:30 hadi saa 7:00 usiku.

Hivyo kuanza safari mapema kutawafikisha kule wanakokwenda bila kulala njiani hata kama mabasi yatamulikwa na tochi za trafiki, ambazo zimeenea barabara zote nchini.

Lakini tatizo jingine ambalo limekuwa likichangia mabasi kuchelewa kuondoka katika kituo kikubwa cha mabasi Ubungo ni ukaguzi na kuweka stika asubuhi yanapotaka kuondoka.

Septemba mwaka huu, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditye, alitoa wito kwa wamiliki kupeleka mabasi yao siku moja kabla kwa ajili ya ukaguzi na kuweka stika ya kupakia abiria ili yaondoke kwa muda waliokubaliana, ambao ni saa 11 alfajiri.

Naibu Waziri alisema hakuna sababu ya kuwazuia wamiliki wa mabasi wanaotaka magari yao yaanze safari saa 11 alfajiri, kwasababu maeneo mengi ya nchi yapo salama kwa sasa.

Kinachotakiwa ni kila upande kutimiza wajibu wake kufanikisha ratiba hiyo mpya ambayo kwa itasaidia abiria kufika kwa wakati kule wanakokwenda.

Chama cha Wamiliki Mabasi Tanzania (Taboa), kinasema utaratibu wa mabasi kusafiri hadi kufika kule yanakokwenda bila kulala njiani unahusu yale yanayokwenda katika mikoa mingi.

Mikoa michache hiyo ni Tabora, Kigoma na Rukwa, kutokana na sababu za kiusalama, hivyo ipo haja kwa mamlaka kuhakikisha kunakuwepo na usalama wa kutosha ili abiria wanaokwenda huko waweze kuondokana na adha ya kulala njiani.

Hata Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewahi kumpa maagizo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, akihoji kwanini mabasi hayatembei usiku huku biashara mbalimbali zinafungwa saa 12 jioni.

Waziri huyo alifanya ziara Makao Makuu ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Ukonga na kumpa siku 14 IGP Sirro akimtaka amweleze mikakati ya kuwazesha Watanzania kufanya kazi saa 24 na mabasi kusafiri usiku.

"Tunataka Watanzania wafanye kazi za kiuchumi kwa saa 24. Hatuwezi tukafikia malengo ya uchumi wa kati kama Watanzania hawafanyi shughuli za kiuchumi. Hatuwezi tukakubali kupewa amri na majambazi ni saa ngapi tufanye shughuli za kiuchumi," anasema Lugola.

Kauli za viongozi hao wa serikali zinaonyesha ni jinsi gani kuna umuhimu wa abiria kusafiri na kufika kwa wakati kule wanakokwenda wakiwa safari badala ya kuishia njiani na kuanza safari kesho yake.

Cha msingi ni kila upande kutimiza wajibu inavyotakiwa, kuanzia madereva, wamiliki wa mabasi, abiria na serikali kwa ujumla ili kufanikisha utaratibu mpya wa kuanza safari mapema.

Katika mabasi ya abiria wapo wafanyabiashara wanaokwenda kufuata biashara zao maeneo mbalimbali, kufuatilia kazi au kufanya shughuli nyingine nyingi , hivyo kufika kwa wakati kule wanakokwenda, kutasaidia kuboresha shughuli za kiuchumi.