Sasa taifa lipasue vichwa kijulikane kiini mimba za utotoni

09Sep 2017
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Sasa taifa lipasue vichwa kijulikane kiini mimba za utotoni

HIVI kama taifa imetokea kupasua vichwa na kujiuliza ni nini hasa chanzo cha tatizo la ujauzito kwa wanafunzi?

Suala la mimba za utotoni limeongezeka kutoka asilimia 23 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 27 kati ya mwaka 2016 na 2017.

Ongezeko hilo la asilimia nne, limetokana na mambo mengi ikiwamo kukosekana kwa fursa ya elimu ya afya ya uzazi kwa vijana, wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 20.

Kwa upande wa mabinti hawa ndiyo wanaoathirika na mimba hizi.

Kila mwaka vyombo mbalimbali vya habari vinahabarisha umma kuhusu baadhi ya wanafunzi mabinti wa shule za msingi na sekondari kushindwa kusoma baada ya kupata mimba.

Mfano kuna ripoti kuwa wasichana 2,971 waliokuwa wanafunzi wa shule nane za msingi na 22 za sekondari za Wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa, walikatisha masomo kutokana na mimba na ndoa za utotoni. Hii ni kati ya kipindi cha mwezi Januari hadi kufikia Juni mwaka huu.

CHANZO CHA TATIZO
Kwa mujibu wa utafiti wa mimba za utotoni uliofanywa mwaka 2010 na Chama cha Wanahabari Wanawake, (Tamwa) ni pamoja na hali duni ya uchumi wa familia.

Ufukara na hali ngumu ya kiuchumi ya familia ni kisababishi kikubwa cha wasichana kukatisha masomo.

Wazazi wanashindwa kuwatimizia mahitaji ya msingi ya mtoto wa kike kwa wakati, hivyo kuathirika kisaikolojia na kufanya maamuzi yasiyo na mustakabali chanya.

Baadhi wanaamua kuacha shule na kubaki nyumbani ama kuolewa ili angalau wapambane na maisha tayari wakiwa nje ya mfumo wa shule.

Uduni wa elimu inayotolewa na mazingira magumu ya kujifunzia, kwa shule za serikali za vijijini, ni sababu kubwa ya wasichana kukatisha masomo.

Shule binafsi nyingi hata zikiwa maeneo ya vijijini, zina mazingira rafiki ya kujifunzia.

Tatu ni suala la malezi duni ya baadhi ya wazazi na kwani wengi hawatumii muda wao mwingi kuwajenga watoto wao kimaadili. Hivyo basi wasichana waliokosa maadili wanashindwa kujiongoza vema na huishia kufuata ushawishi mbaya.

Kukosekana kwa elimu ya afya ya uzazi kwa wasichana waliopevuka kimaumbile, wanaoihitaji ili waweze kuyapokea mabadiliko ya makuzi kwa umakini ni sababu nyingine.

Jambo la kusikitisha, sio tu vijijini hata pia mijini. Wazazi wengi hawaongei na watoto wao wa kike ambao tayari wako katika umri wa kukua.

Bila wasichana hawa kupatiwa maelekezo ya msingi kuhusu ukuaji na hasa namna ya kuepukana na mimba, wengi wanatumbukia kwenye mtego wa mimba za utotoni bila ya kujijua.

Mitazamo hasi kuwa thamani ya mtoto wa kike ni kuolewa au kuwa mama na kuzaa ni kiini kingine cha mimba za utotoni.

Wanajamii wenye mitazamo kama hii ndiyo wanaowakatisha tamaa wasichana badala ya kuwahimiza kuwa na bidii shuleni , wanawashawishi kutenda mambo yanayowavurugia maisha.

Utafiti wa Masuala ya Afya uliofanywa na serikali na wadau unabainisha ukweli huo ambao kwa kiasi kikubwa unaathiri jamii nyingi za Kitanzania.

Utafiti wa kidemografia na afya (TDHS) wa mwaka 2004 na 2005 unaonyesha kuwa mmomonyoko wa maadili ndani ya jamii na tabia ya kutoipatia sheria nafasi yake unachochea.

Aidha, jamii ilipofikia ni kuona kawaida mabinti au wanafunzi kuwa na mahusiano ya kimapenzi na waalimu wake shuleni na kusingiziwa mwanafunzi mwenzake wa kiume janga la mimba linapotokea. Kama ilivyotokea siku za hivi karibuni Wilayani Bunda huko mkoani Mara.

Halikadhalika, tabia ya baadhi ya baba kuwanyanyasa kingono mabinti zao kutokana na imani, mila na desturi au imani za kishirikina ni mambo yanayochangia.

VIPAUMBELE
Kulingana na uzito tatizo hili, kila suala la mwanafunzi kupata mimba, kabla ya kufikiwa uamuzi wa mhusika kufukuzwa shule ni lazima kwanza wadau wakuu wajiridhishe kuwa amepata mimba katika mazingira gani.

Hapo ndipo, kama taifa, kutakuwa na taratibu kuaanza kuuelekea mstari mnyoofu wa kumkomboa mtoto wa kike!

Kwanini nasema hivyo, dhahiri Serikali inatambua kuwa mimba na ndoa za utotoni kwa kiasi kikubwa zinawakuta wasichana wa familia masikini, ambao wakati mwingine licha ya kutokuwa na hakika ya kupata chakula, bado wanalazimika kuifuata shule kwa umbali wa hata zaidi ya kilomita 10 kwenda na kurudi.

Njiani wanapita mapori na vichaka kadhaa. Je, tutakuwa sahihi kumhukumu sawa na yule wa mjini, anayetoka katika familia yenye afuheni kwa kiasi tena ikibidi anafuatwa na kurejeshwa kwa usafiri wa shule au gari la nyumbani?

Kama bado haitoshi, hivi ni kweli shule nyingi za vijijini za serikali, (msingi na sekondari), zinafanana miundombinu hata kwa asilimia 20 na zile ambazo zinapatikana mijini? Na zile alizoacha mkoloni licha ya kuchakaa lakini bado zinaonyesha zilipangiliwa vizuri kuliko zinazojengwa sasa kwa kuchakachuliwa.

Tatizo huwa kubwa mpaka wananchi wajikusanye Shilingi 200 hadi zitimie wajenge shule kwa jasho lao!