Sasa ushindi jimboni uviondoe viti maalum

13Jan 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Sasa ushindi jimboni uviondoe viti maalum

BUNGE ndilo linalohusika na maamuzi muhimu yahusuyo nchi kuanzia kutunga sheria, bajeti za serikali, sera, mipango na mambo mengine muhimu kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Wanaoingia bungeni hupatikana kwa njia tatu, mosi kuchaguliwa majimboni kwenye kura, wanawake wanaoingia kupitia viti maalumu na 10 wanaoteuliwa na rais.

Hata hivyo, kwa muda mrefu, wanawake wamekuwa wakipiga kelele wakitamani kuwapo kwa uwiano kati yao na wanaume, katika nafasi za uongozi ukiwamo ubunge wa majimboni badala ya viti maalumu.

Kilio chao kinatokana na ukweli kwamba, tangu nchi ipate uhuru, ushiriki wa wanawake katika bunge haujafikia asilimia 50 kwa 50 kwa kuchaguliwa majimboni, ambayo wamekuwa wakiitamani.

Ili kufanikisha lengo lao hilo, wamekuwa wakihamasishwa kuwania nafasi za uongozi, kwa kuwa wanayo fursa katika kukuza hata uchumi wa nchi.

Kwa mfano, kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, kulikuwapo na majukwaa mbalimbali ya kuhamasisha wajitose kuwania ubunge kwenye majimbo mbalimbali na udiwani katika uchaguzi.

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), ulifikia kuandaa ilani ya uchaguzi ya wanawake na kuisambaza katika vyama mbalimbali vya siasa, ili viwateue kuwania urais, ubunge na udiwani.

Ilani hiyo ya kuendeleza madai ya wanawake watetezi wa haki za ushiriki katika uongozi wa kisiasa, ilibeba madai yao, kwa kuwa ni wadau na washiriki wakuu katika michakato mbalimbali ya uchaguzi.

Pamoja na juhudi zao hizo, hakujawa na la kujivunia bado asilimia 50 kwa 50 hasa kwenye ubunge haijafikiwa ni kutokana na ukweli kwamba, katika uchaguzi mkuu uliopita ni wanawake wachache wamepata ubunge wa majimbo.

Katika majimbo zaidi ya 250 ya uchaguzi, wanawake waliopata ubunge wa majimbo hawazidi 20, hali inayoonyesha kuwa bado wana safari ndefu ya kufikia malengo yao wanayotamani.

Ipo mikoa mingi ambayo haina wabunge wanawake wa majimbo kama Mara wenye majimbo 10, ambayo yote yana wabunge wanaume, kana kwamba hakukuwa na wanawake waliojitokeza.

Umefika wakati sasa wa wanawake kujiuliza wanakwama wapi na hadi lini wasifikie kile wanachokitamani? Je, ni mfumo dume au ni vyama vyao kutokuwaamini au kuna sababu nyingine wanazozijua, zinazokwamisha?

Kwa kauli zao kuna wakati wanasema wamechoka kuwa wabunge ama madiwani wa viti maalum na wanatamani kuchaguliwa majimboni na kata, lakini wameendelea kushinda wachache.

Wakati mwingine mila na utamaduni hasa mfumo dume, fedha za kugharamia uchaguzi, utekelezaji mdogo wa sera za kimataifa na kitaifa kuhusu usawa wa kijinsia na vyama kutowapa nafasi huenda vikawa vikwazo kwao.

Ubunge kupitia majimbo ni wa muhimu, katika baadhi ya vyombo vya serikali ambavyo vinashughulika na kuandaa sera na mipango ya maendeleo, kwa kuwa wana uwezo kama walivyo wanaume.

Wanawake ndiyo wapigakura wakuu, wanatambua kuwa ni wadau muhimu katika shughuli zote za kisiasa na maendeleo ya jamii, wasikate tamaa, badala yake waendelee kupaza sauti ya kudai asilimia wanazotaka.

Lakini pamoja na hayo, suala ya kukaa na kutafakari ni wapi wamekosea, ni la muhimu, kwa kuwa litawasaidia kuibuka na mikakati zaidi ya kufanikisha ajenda yao ya kutaka asilimia 50 kwa 50 ifikapo 2025.

Yawezekana mfumo dume, unachangia kutokuwapo kwa usawa katika uwiano wa wanawake na wanaume kwenye uwanja wa siasa, hasa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi vya siasa hivyo wajitahidi kupitia majukwaa yao kupambana na utamaduni huo unaowakwamisha.