Sasa zamu iwe ya wakulima kuwa na mkutano na Rais

11Jun 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Sasa zamu iwe ya wakulima kuwa na mkutano na Rais

BAADA ya tija ya mikutano miwili aliyoifanya Rais John Magufuli na sehemu ya makundi ya Watanzania yaliyo na mchango kwenye uchumi wa nchi, nimeshawishika kumsihi aendeleze utaratibu huo.

Ninasema hivyo kwa sababu kwa maoni yangu mikutano hiyo imempa alichokitaka na imemuwezesha kuchukua maamuzi ambayo yanasaidia sekta zinazohusika kufanya vizuri zaidi.

Januari mwaka huu, Rais Magufuli alikutana na wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam ili kusikiliza kero zao.

Si kero tu pia ushauri wa nini kifanyike ili wao na taifa lifaidike na madini yaliyoko nchini.

Inashangaza kwa hali ilivyo kwamba Ripoti ya Benki ya Dunia (WB) inaonyesha kutoitambua Tanzania kwa kuuza madini hata katika eneo la Afrika Mashariki pamoja na kumiliki utajiri mkubwa wa rasilimali hiyo kuliko nchi zingine za eneo hili.

Na ndiyo maana aliwataka wadau hao kueleza kero zote zinazosababisha hali hiyo na ushauri wao ambao ungehakikisha vikwazo vilivyomo katika mnyororo wa biashara ya madini vinaondolewa.

Wadau wakataja sababu za madini kuibiwa kwamba ni utitiri wa kodi kuanzia kwa mchimbaji hadi mfanyabiashara wa madini.

Na mmoja wa washiriki wa mkutano huo akatoa mfano kwamba mchimbaji akitaka kuuza dhahabu kwa mfano, alikumbana na tozo ya service levy ya asilimia 0.3, mrahaba asilimia 6, ukaguzi asilimia moja na ada ya clearance.

Kwamba hiyo ilikuwa mbali na kodi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambapo zikijumlishwa zilikuwa zinamfanya mchimbaji kulipa kodi ya jumla ya asilimia 12.3.

Kwa wafuatiliaji wanajua matunda ya mkutano huo kwamba ni pamoja na baadhi ya kodi zilizokuwa kero kwa wafanyabiashara na wachimbaji hususani wadogo zimefutwa.

Hizo ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Kodi ya Zuio ya asilimia tano inayotozwa kwenye bei ya kuuzia madini ya aina zote.

Aidha, masoko ya madini katika mikoa mbalimbali nchini yameanzishwa na taarifa za awali zinaonyesha kuwa mambo yanakwenda vizuri.

Ikumbukwe kwamba ufanisi katika sekta ya madini una tija kwa Watanzania wengi, kwani taarifa za Shirikisho la Vyama vya Uchimbaji Madini Tanzania (Femata), zinaonyesha kwamba watu milioni sita wanashughulika na sekta hiyo nchini.

Mkutano mwingine ulioacha mshindo ni ule uliofanyika wiki iliyopita Juni 7, jijini Dar es Salaam kati ya Rais Magufuli na wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka wilaya 139 nchini na wajumbe wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC).

Mengi yalielezwa na wafanyabiashara, hasa wakilalamikia tozo na kodi zisizo rafiki, lakini baadhi ya maofisa wa TRA wanaodai rushwa kutoka kwa wafanyabiashara.

Rais Magufuli naye alieleza dosari ya wafanyabiashara ikiwamo mbinu wanazotumia kukwepa kulipa kodi ya serikali kwa kutengeneza vitabu viwili vya mahesabu, kimoja kikibeba takwimu za uongo na kingine za ukweli.

Japokuwa matunda ya mkutano huyo ndiyo yanaanza kuonekana likiwamo la mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri na TRA, Muungwana anatarajia tija kubwa zaidi ya mkutano huo.

Ni kwa msingi huo, Muungwana ana maoni kwa Rais kuwa na mkutano wa aina hiyo na wakulima nchini, kundi ambalo linachukua asilimia 70 ya Watanzania wote.

Kwamba iwapo mkutano kama huo utafanyika, Rais atapata changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakulima wa pamba, korosho, kahawa, tumbaku, chai, mahindi, mpunga, iliki, karanga na mengineo kutoka katika midomo ya wahusika.

Kimsingi bado kuna yanayopaswa kufanywa kwa kundi hili ambalo ni muhimu katika suala zima la kupambana na umaskini, ili kuifikia Tanzania ya viwanda na kipato cha kati 2025.

Muungwana anaona mkutano kama huo utakuwa na tija zaidi katika sekta ya kilimo, ikichukuliwa kuwa maamuzi aliyofanya Rais Magufuli baada ya mikutano hiyo miwili ya inazidi kuleta manufaa kwa nchi.