Segerea kufanya kampeni ya mazingira bora kwa elimu bora

02Feb 2016
Nipashe
Tesa
Segerea kufanya kampeni ya mazingira bora kwa elimu bora

SEKTA ya Elimu bado imegubikwa na changamoto nyingi licha ya kuwapo jitihada nyingi zinazofanywa na serikali na mashirika mbalimbali yasiyo ya serikali ili kuhakikisha kuwa inapiga hatua.

Shule nyingi za sekondari na msingi zina ukosefu mkubwa wa miundombinu ya kusomea kama vile madawati, vyoo vya kisasa na visima vya maji hali inayosababisha watoto kwenda umbali mrefu kutafuta maji kwa ajili ya shughuli mbalimbali za usafi wa shule na wao binafsi.
Pia bado kuna upungufu wa shule katika baadhi ya kata na kusababisha watoto wengine kuchelewa kuanza shule au kupangiwa shule za mbali na kujikuta katika mazingira magumu ya kwenda na kurudi.
Jitahada nyingi zimekuwa zikifanywa na serikali hata na baadhi ya mashirika yasiyo ya serikali na watu binafsi katika kuokoa jahazi la elimu, kwani ndio ufunguo wa maisha wa kila mtoto.
Katika harakati za kuondoa changamoto za elimu shuleni Mbunge wa jimbo la Segerea Bonnah Kaluwa ameanzisha kampeni ya “Mazingira bora kwa elimu bora”.
Lengo la kampeni hiyo, ni kufanya tathimini na tafiti kwa shule zilizopo ndani ya jimbo lake ili kubaini changamoto zinazozikabili na kuzitatua.
Mbunge huyo anasema, sekta ya elimu bado ina changamoto nyingi sana licha ya Rais wa awamu ya tano, John Magufuli kutangaza kuwa sasa elimu ni bure.
“Watu wanafikiri Rais kutangaza kuwa elimu ni bure basi na matatizo katika shule yamekwisha, nawaomba wafahamu kwamba, bado kuna changamoto nyingi katika shule nyingi.
“Mfano bado kuna shule zina upungufu wa madawati ya kutosha hivyo watoto wanakaa chini kipindi cha masomo lakini hata baadhi ya kata zina upungufu wa shule za sekondari,”anaendelea kusema.
Anasema malengo ya kampeni hiyo ni kusaidia jamii jimbo la Segerea katika sekta ya elimu na nchi kwa ujumla.
“Hii kampeni si kwa ajili ya kumnufaisha mtu binafsi, bali inalenga kusaidia jamii ndani ya jimbo la segerea katika upatikanaji wa elimu bora kupitia maboresho ya miundombinu ya shule kama madarasa,vyoo, mifumo ya maji, madawati na mahitaji mengine,”anafafanua Kaluwa.
Mbunge huyo anasema, jamii yote ni mashuhuda kuwa kuna changamoto nyingi katika sekta ya elimu nchini, hivyo kampeni yake inafanya kila jitihada katika kutatua changamoto hizo.
Anaweka wazi kuwa Sh. bilioni 9 zitatumika katika mradi huu kwa ajili ya marekebisho ya baadhi ya miundombinu katika shule zilizopo ndani ya jimbo lake.
Kaluwa anasema, utafiti waliofanya katika kata 13 zilizopo ndani ya jimbo hilo wamegundua kuwa, shule zina upungufu wa madawati,vyoo vya kisasa na mifumo ya maji.
“Utafiti huu niliofanya mimi na viongozi wenzangu tumebaini kuwa tunahitaji jumla ya madawati 15,000, matundu ya vyoo vya kisasa 1335, visima vya maji 12 na vyumba maalumu kwa ajili ya watoto wa kike ni 38.
Hata hivyo anasema kampeni hiyo ni muendelezo wa kampeni aliyowahi kufanya akiwa diwani wa kata ya Kipawa na kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.
“Kimsingi huu ni muendelezo wa kampeni niliyowahi kufanya katika kata ya Kipawa , kupitia mfuko wangu wa Bonnah Education Trust niliweza kumaliza tatizo la madawati hadi namaliza kipindi changu cha uongozi niliweza kutatua tatizo la madawati kwa asilimia 80.
“Hii kampeni ilifanya vizuri sana katika kata ya Kipawa hivyo nikaona ni jambo jema kulianzisha Segerea na nina imani kubwa katika kipindi cha miezi sita ya utekelezaji tutaweza kutatua matatizo mengi,” anasema.
Kaluwa anasema lengo lake ni kuona kila mwananchi wa ndani na nje ya jimbo lake ananufaika na mfuko huo hasa katika sekta ya elimu.
Mbali na hayo, anasema watashirikiana na serikali, sekta na mashirika binafsi na wadau wa elimu katika utekelezaji wa kampeni hiyo ili iweze kuzaa matunda.
Pia anasema kampeni hiyo wanatarajia kuifanya kwa awamu mbili ambazo ni matembezi ya hiari na chakula cha jioni kwa lengo la kukusanya fedha.
“Matembezi haya yatafanyika ndani ya jimbo kwa kushirikisha wananchi na wadau wote wa elimu tukiwa na lengo la kukusanya fedha za kuboresha miundombinu ya elimu,”anasema.
Aidha mmoja kati ya mdau wa elimu na mshiriki katika kampeni hiyo Flaviana Matata ambaye ni mwanzilishi wa Taasisi ya Elimu ijulikanayo Flaviana Matata Foundation anasema ushirikano ndio nguzo kubwa katika kukamilisha vema kampeni hiyo.
“Nimezunguka sana vijijini katika kusaidia masuala mbalimbali ya elimu, kuna wakati unafanya jambo jema lakini baadhi ya watu wanakuwapo kwa ajili ya kukuangusha usifanikiwe.
“Hatuna wakati wa kuwekeana vikwazo huu ni wakati wa kusaidiana pindi unapoona mwenzako anafanya jambo jema, hasa litakaloleta maendeleo katika jamii au nchi kwa ujumla.
Matata anasema, wadau mbalimbali wa elimu wajitokeze katika kusaidia sekta ya elimu, kwani bado kuna changamoto nyingi hasa katika maeneo ya vijijini.
Vilevile alisema viongozi wengine waige mfano wa mbunge huyo, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanaisaidia serikali kufikia malengo yake kwa haraka na viwango bora.