Sekta binafsi iwezeshwe kuokoa tasnia ya habari

29Nov 2020
Joseph Kulangwa
Nipashe Jumapili
FIKRA MBADALA
Sekta binafsi iwezeshwe kuokoa tasnia ya habari

HIVI karibuni akizungunmza kwenye mkutano mkuu wa Shirikisho la Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi, alitoa kauli nzuri na mwafaka kwa tasnia ya habari nchini.

Dk Abbasi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, alizungumzia umuhimu wa wafanyakazi katika vyombo vya habari nchini, kuwa na mikataba ya kazi, ili kuleta mazingira ya usalama na haki kazini.

Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo baada ya kuambiwa na washiriki wa mkutano huo wa siku mbili uliofanyika Morogoro Novemba 16 na 17, mwaka huu, jinsi hali halisi ilivyo katika baadhi ya vyombo vya habari.

Mgeni huyo rasmi, akasema ataiagiza Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuhakikisha kwamba wafanyakazi katika vyombo vya elektroniki kwa maana na redio na televisheni, nao wanatekeleza matakwa hayo ya kiutumishi na kuweka mazingira mazuri ya kazi.

Ni kweli, kuwa mazingira ya kazi na maslahi katika vyombo vingi vya habari nchini, hususan vya binafsi ni duni, kutokana na kipato cha vyombo hivyo kupungua kwa sababu mbalimbali, lakini kubwa ikiwa ni ya matangazo.

Si siri, kwamba matangazo ndiyo roho ya kiuchumi ya chombo chochote cha habari, mbali na mauzo ya nakala, na katika redio na televisheni ni zaidi, kwa sababu bila matangazo, hakuna kipato hakuna malipo.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wamiliki wamewageuza wafanyakazi wao katika vyumba vya habari kama vibarua au wa kujitolea. Imefika hata baadhi ya waandishi kuomba kujitolea na si kuajiriwa, kwa sababu hakuna ujira wa kuwalipa.

Matokeo yake, waandishi wamekuwa wakiishi kwa posho za nauli katika vikao wanavyoalikwa kuhudhuria kuchukua habari. Hali hiyo pia imechangia baadhi kukiuka maadili ya uanahabari na kupokea rushwa, ili kumsifia au kumchafua mtu au taasisi.

Wapo baadhi ya wamiliki kwa kudharau wafanyakazi wao, wamekuwa wakiwapanga mstari na kuwalipa chochote alichonacho mfukoni siku hiyo, kama nauli ya kuwaleta na kuwarudisha nyumbani. Mfanyakazi akihoji huambiwa hali ni mbaya.

Na kweli, kama hakuna tangazo linaloingia huku gharama za uendeshaji zikiongezeka, ni nini matarajio ya mwajiri? Ataishia tu kulipa kijungujiko na maisha kuendelea kuwa magumu kwa wafanyakazi wake.

Ingawa Dk Abbasi si Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi inayosimamia TCRA, ni dhahiri atawasiliana na mwenzake wa wizara husika, ili vyombo vyote vya habari viitekeleze hili.

Ni wazi sasa kwamba kutokana na hali hiyo, upo umuhimu wa vyombo hivi kuwa chini ya wizara moja, pengine ikaitwa Wizara ya Habari na Mawasiliano, ili vyombo kusimamiwa kwa pamoja na kuleta ufanisi.

Lakini pia, ipo haja kwa Serikali hasa kwa kuzingatia kauli ya Rais John Magufuli akizindua Bunge la 12 hivi karibuni, ya Serikali kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi, kuelekeza taasisi za umma hata binafsi kupeleka matangazo yao kwenye vyombo hivyo kama ilivyokuwa awali.

Utaratibu wa Idara ya Habari, Maelezo, kusimamia matangazo kwenye vyombo vya habari, umeviathiri, kiasi kwamba kama hali hii itaendelea, kwa muda mrefu, ni wazi vitakufa na kubakiwa na mitandao ya kijamii katika kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha umma.

Wapo wanaoaimini kwamba nafasi ya magazeti, redio na televisheni katika jamii imekuwa finyu, kwa sababu leo taarifa ziko kiganjani kupitia mitandao ya kijamii, bila kujali uhakika na ukweli wa habari hizo ambazo hazifanyiwi kazi.

Ukweli ni kwamba hata kwa aina ya Bunge la 12 lilivyo, lenye idadi kubwa ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), watu wengi watategemea zaidi magazeti na redio, kujua mengi ya upande wa pili (Upinzani) kuliko wa CCM ambao una wasemaji wengi bungeni tayari.

Naiomba Serikali izingatie dhamira yake ya kushirikiana na sekta binafsi, ikiamini kwamba ndiyo yenye mchango mkubwa katika kutoa ajira kwa Watanzania, kwa kuwa ndiyo hasa inayotakiwa kufanya biashara na si Serikali. Alamsiki!