Sera kutoa elimu bure inavyomuenzi Nyerere

12Oct 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Sera kutoa elimu bure inavyomuenzi Nyerere

ALHAMISI Oktoba 14, Watanzania wataadhimishi kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Nyerere  Rais wa kwanza wa Tanzania, aliyefariki dunia Oktoba 14 mwaka 1999 ikiwa ni miaka 14 tangu ang'atuke kwenye nafasi hiyo ya juu, aliyokuwa anaishikilia tangu kupata ...

uhuru mwaka 1961.

Yapo mengi aliyoyatenda kwa taifa wakati wa uongozi wake ambayo yamemfanya aitwe Baba wa Taifa, ikiwamo kutaka kila Mtanzania apate elimu, kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo.

Enzi ya uongozi wake, alitoa elimu bure, lakini pia kulikuwapo na madarasa ya elimu ya watu wazima iliyokuwa ikiitwa ngumbaru, kwa wale ambao hawakupitia mfumo rasmi, kuwasaidie wajue kusoma na kuandika.

Ikumbukwe kuwa baada ya uhuru, aliwatangazia vita maadui watatu, ujinga, maradhi na umaskini, hivyo akawekeza zaidi kwenye elimu kwa lengo la kutokomeza ujinga, ili iwe rahisi kumaliza hao wengine wawili.

Kile alichokisimamia kwenye elimu wakati wa uongozi wake, kiliendelezwa na waliochukua nafasi na hata alipofariki dunia waliomfuatia wameendelea kuhakikisha watoto wanapata elimu.

Sasa ni miaka 22 tangu alipofariki dunia, lakini alichosimamia kwenye elimu wakati wa uongozi wake kinaendelea kudumishwa ili kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule asome kadri anavyoweza.

Kwa mfano, sera ya elimu bila malipo ilianza rasmi nchini baada ya serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani mwaka 2015 na bado inaendelea katika awamu ya sita.

Sera hiyo inamaanisha kufutwa kwa ada zote katika shule za sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na lakini michango kwa wazazi na walezi katika ngazi ya elimu ya msingi.

Sera hiyo imeleta ahueni kwa wazazi na walezi, hasa kulingana na hali duni za kiuchumi za Watanzania wengi na imekuwa na tija katika sekta ya elimu, kwani imetoa fursa kwa kila mtoto kusoma.

Kumekuwapo na taarifa mbalimbali kuwa, hatua za serikali kutoa elimu bure zimehamasisha watoto wengi kuandikishwa shule kila mwaka, na hicho ndicho Baba wa Taifa alichokikusudia kwamba kila mtoto apate elimu.

Maendeleo hayo ya elimu kwa sasa, mzizi wake ni Mwalimu Nyerere ingawa zipo  changamoto kadhaa kwa sasa, kutokana na kutomwandaa mwanafunzi kujitegemea badala yake wahitimu huzunguka kutafuta ajira.

Pamoja na hayo, kusoma ni hatua na kupata ajira ni hatua nyingine, hivyo umuhimu wa elimu uko palepale, iwe ya kujitegemea au kutojitegemea, kwani mtu anaweza kuitumia kufanya mambo makubwa ya maendeleo.

Zipo juhudi mbalimbsli zikifanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu za kutoa mafunzo ya kuwezesha wahitimu watarajiwa kujipanga kwa ajili ya kujiajiri badala ya kutamani kuajiriwa tu.

Ni kweli kwamba, shule nyingi zinakabiliwa na uhaba wa madarasa, madawati, walimu na vifaa vya kufundishia, lakini angalau kile alichokiasi Baba wa Taifa cha kutaka kila mtoto apate elimu kinaendelezwa.

Kwa wale ambao hawakupata elimu katika mfumo rasmi, walipata elimu ya ngumbaru, kwa sasa wamewekewa mfumo mwingine kama Mpango wa Elimu kwa Waliokosa (MEMKWA), ulioanza kutekelezwa na awamu ya tatu.

Vilevile, ili kuhakikisha Watnzania wanapata elimu, kumekuwapo na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) ambayo ni programu ya serikali ya kuboresha elimu ya msingi kwa watoto wote nchini.

Hiyo ni programu inayojumuisha wasichana na wavulana, matajiri na maskini, pamoja na watoto wenye ulemavu, ikilenga kuhakikisha hakuna hata mmoja anayeachwa nyuma katika kupata elimu.

Kinachofanyika kwenye elimu leo, kinaakisi kile ambacho kiliasisiwa na Baba wa Taifa, hiyo yanapotajwa mafanikio ya elimu nchini, jina la Hayati Baba wa Taifa, linahusika kwa kiasi kikubwa.