Serikali iangalie ustawi wa watoto wanaoshinda stendi

06Sep 2017
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Serikali iangalie ustawi wa watoto wanaoshinda stendi

UPITAPO katika vituo vikubwa vya daladala nyakati za asubuhi, mchana ama jioni utawaona watoto wakirandaranda na kutokuwa na kazi yoyote wanayoifanya.

Kama watakuwa wanafanya kazi basi utawaona wamejitwisha kichwani beseni la matunda wakifanya biashara. Haya ndiyo maisha ya watoto wengi wanaozagaa kwenye stendi kubwa za daladala jijini Dar es Salaam.

Jiji ambalo kimsingi ni makazi ya serikali ya awamu ya tano, Jiji ambalo viongozi wote na mamlaka husika zimepiga kambi. 

Katika kituo cha Makumbusho, Simu 2,000 (Mawasiliano), Mbezi Mwisho na vinginevyo mara nyingi nyakati za jioni utakuta idadi kubwa ya watoto wakiuza bidhaa ndogo ndogo kama vile Sigara, karanga, Ubuyu, Kashata na matunda. 

Ukiwaangalia kwa mtazamo wa harakaharaka, watoto hao wana umri usiozidi miaka 15, muda wote wanashinda katika vituo hivyo wakiwa na wapiga debe na madereva ambao baadhi yao huwa na kauli mbaya. 

Watoto hao mara nyingi hushinda na wavuta unga na wanywa pombe kali wanaoongea lugha za matusi ambazo ni lugha zenye athari kwa tabia na ukuaji wa watoto. 

Hapa siwazungumzii wale watoto ombaomba ambao tumeshawazoea kuwaona katika makutano ya barabara wakiomba pesa pindi magari yanaposimama La hasha! Ninawazungumzia wale watoto tunaowakuta asubuhi vituo vya daladala wakiwa wanazurura tu.
 
Ukienda katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani eneo la Ubungo utawakuta.Watoto hawa wanakusanyika eneo hilo jioni, wakati mwingine wako peke yao ama na wazazi wao.

Wakati nikiwa mdogo, nilikuwa naona wazazi wakiwafungia watoto wao majumbani ama wanawakabidhi kwa majirani kucheza nao, lakini hilo kwa sasa halipo tena.

Nakumbuka wakati Tume ya marekebisho ya Katiba mpya ilipokuwa inazunguka mitaani kukusanya maoni, baadhi ya wadau wanaotetea haki za watoto walipendekeza katika katiba mpya kuwe na msingi utakaolinda haki za watoto. 

Walipendekeza katiba mpya iwawezeshe watoto kupata huduma za elimu, kuwalinda dhidi ya ukatili wa kijinsia na kwa watoto wa kike kuepushwa na ndoa za utotoni.

Pengine katiba mpya itakapokamilika itakuwa dawa ya kuzuia utumikishwaji watoto wadogo.

Watoto hawa wakiachwa waendelee kuishi katika vituo hivyo kuna hatari kubwa ya kutengeneza kizazi chenye vijana ambao ni wezi. 

Pengine huenda vitendo cha uhalifu hapa nchini havimaliziki kutokana na kukua kwa watoto hawa wasiokuwa na shughuli yoyote ya kufanya, ambao wanatafuta riziki kila siku. 

Wengi wa watoto hao ukiwauliza kwa nini wapo vituoni utawasikia wakijibu kuwa wamekimbia nyumbani kutokana na mateso makali wanayoyapata kutoka kwa wazazi wao sana sana mama wa kufikia.

 Ukiwauliza zaidi wanakula wapi au wanalala wapi, watakujibu kuwa wanakula katika vibanda vya mama lishe baada ya kupewa kazi ya kuosha vyombo, na kuhusu kulala watakujibu wanalala Stendi ya mabasi Ubungo. 

Pengine baba wa watoto hawa wapo katika Jiji hili hili la Dar es Salaam na wameridhika kutoweka kwa watoto wao nyumbani, Pengine hata hawajaonyesha jitihada zozote za kuwatafuta. 

Baadhi ya watoto hawa ukiwauliza kwa nini wako mitaani watakujibu kuwa walitoroka nyumbani baada ya wazazi wao wote kufariki na baada ya kuchukuliwa na ndugu zao kama vile shangazi walijikuta wanatumikishwa kazi nyingi. 

Hakika jambo hili lisipovaliwa njuga na mamlaka husika hususani Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto linaweza kuwa hatari kwa taifa kwa sababu kila siku idadi ya watoto wanaozurura mitaani inaongezeka. 

Ninaamini serikali ipo, tena serikali makini inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, inawajibu wa kuwaangalia kwa jicho la tatu watoto hawa na hasa kwa upande wa bajeti ili iwafikie katika kuangalia mustakabali wao.