Serikali iangamize mtandao wa watumishi hewa

13Apr 2016
Salome Kitomari
Nipashe
Mjadala
Serikali iangamize mtandao wa watumishi hewa

HIVI karibuni serikali ilitangaza kubaini wafanyakazi hewa zaidi ya 7,800 katika ngazi mbalimbali nchini na kuanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika.

Mchakato huo ulianza baada ya Rais Dk. John Magufuli, kuwataka wakuu wapya wa mikoa aliowapisha Machi 15, mwaka huu, kubaini watumishi hewa katika mikoa yao na kuwasilisha taarifa ndani ya siku 15 baada ya kuanza kazi.

Wakuu hao wa mikoa walikwenda kuanza kazi na Machi 30, mwaka huu, Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene, alipokea taarifa kwa kila Mkuu wa Mkoa kutaja idadi ya watumishi hewa aliowabaini.

Siku chache baadaye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki, alieleza watumishi hao wameisababishia serikali upotevu wa zaidi ya Sh. bilioni 7.5.

Fedha hizo kwa haraka zingeiwezesha serikali kujenga kilomita saba za barabara kwa kiwango cha lami, ikiwa ni makadirio yanayotajwa na wataalamu kuwa kila kilomita moja ya lami inajengwa kwa Sh. bilioni moja.

Katika sakata hilo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Malecela na Katibu Tawala wa mkoa huo, Abdul Dachi, walijikuta katika ‘wodi’ ya Dk. Magufuli na kutumbuliwa kwa kudanganya juu ya watumishi hewa.

Rais alieleza kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo alishtuka sana na kutuma watu kuchunguza na kubaini watumishi 45 na kwamba uchunguzi zaidi unaendelea.

Yapo mambo mengi katika watumishi hewa wanaotajwa na serikali, wakiwamo ambao walishafariki, walioachishwa kazi kwa makosa mbalimbali, lakini hawakuondolewa katika mfumo wa malipo na waliokwenda kusoma bila ruhusa na kesi zao kupelekwa katika mamlaka mbalimbali za maamuzi.

Licha ya watumishi hao kutokuwepo kazini na wanatakiwa kuondolewa katika mfumo wa malipo waliendelea kulipwa, fedha ambazo ziliingia katika mifuko ya wajanja wachache.

Katika hili kuna kuna mtandao kuanzia sehemu ya chini hadi juu, mathalani katika halmashauri Afisa Utumishi, Mkurugenzi Mtendaji, mhasibu na mkaguzi wa ndani anajua watumishi kadhaa wameshafariki, lakini bado wanaonekana katika orodha ya mshahara ni wazi kuwa hawezi kula fedha hizo pekee yake bila kushirikiana na Wizara na Hazina.

Wapo watumishi hususani walimu ambao walikwenda masomoni bila ruhusa ya mwajiri na wengine kwa sababu za utoro walisimamishwa kazi na kesi zao zinashughulikiwa na Mamlaka mbalimbali za maamuzi kama TSD kwa walimu.

Katika hili uwajibikaji unapaswa kufanyika kwa mtandao mzima ili kumaliza tatizo hilo kwa kuwa fedha hizo ziligawanywa kwa watu mbalimbali ili kulinda mwanya huo wa ulaji.

Mathalani, hakuna ubishi kuwa RC na RAS wa Shinyanga walipewa taarifa na wasaidizi wao, lakini hawakufuatilia ukweli wa taarifa husika, kwa mazingira hayo ni wazi kuwa wasaidizi hao wanajua mtandao wa ulaji ndiyo maana waliendelea na ile dhana ya kulindana.

Ni lazima serikali ishughulikie mtandao huo katika kumaliza mizizi ya upotevu wa mabilioni ya fedha ambazo zingeingia katika huduma muhimu za kijamii zingewezesha wananchi wanaotaabika kwa kukosa maji, huduma nzuri za afya na miundombinu duni kupata utatuzi.

Fedha za mshahara wa watumishi na uendeshaji wa serikali zinatokana na kodi mbalimbali kutoka kwa wavuja jasho wa nchi hii, lakini baadhi ya watu walijitengenezea himaya ya kuishi kama peponi huku walio wengi wanaopaswa kunufaika na nchi yao wakiendelea kutaabika.

Tayari serikali imewasilisha bajeti ya mwaka 2016/17 ambayo itakuwa ni Sh. trilioni 29.53, ambayo imepunguza utegemezi kwa wafadhili na kutoa mwelekeo wa kwenda kujitegemea kwa kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha.

Na Hivi karibuni wahisani mbalimbali zaidi ya 10 walitangaza kujitoa katika kuchangia bajeti jambo ambalo linaonyesha kuwa nchi inapaswa kujipanga vizuri kwa kuongeza makusanyo ya mapato na kuzuia mianya ya rushwa na upotevu wowote wa fedha.

Kwa mishahara hewa pekee serikali inapata fedha za kutengeneza kilomita saba za lami na ikifuatiliwa kwa undani zaidi fedha nyingi itaingia katika mfumo rasmi na kuiwezesha serikali kukusanya kila Shilingi yake na kuielekeza katika shughuli za maendeleo.

Bila kubaini mtandao wa wizi huo, bado wataendelea kucheza mchezo huo kwa kuwa kwa maisha ya kibinadamu wapo wanaofariki kila siku na wanaoacha kazi kutokana na sababu mbalimbali.

Serikali ije na mfumo thabiti wa kukabiliana na tatizo hilo katika kujiletea maendeleo endelevu kwa wananchi kuona mgawanyo wa keki ya taifa badala ya kuishia kusoma takwimu kila siku kwenye makaratasi au kusikia katika vyombo vya habari.