Serikali isikilize kilio cha wakulima hawa wanaodai

12Nov 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Serikali isikilize kilio cha wakulima hawa wanaodai

NIMEVUTIKA kuendelea kuzungumzia kadhia ya baadhi ya wakulima wa pamba ambao hawajalipwa fedha zao hadi sasa, wengi wakiwa kwenye maeneo ya Kanda ya Ziwa, wakati msimu mpya wa kilimo ukiwa tayari umeshaanza.

Zipo sababu zilizonivutia, mojawapo ikiwa ni hatua ya Mbunge wa Busega, Raphael Chegeni, kuuliza swali la nyongeza bungeni wiki iliyopita, akitaka kujua mkakati wa serikali kuwalipa wakulima hao madeni wanayodai hadi sasa.

Hatua ya Chegeni imenifanya nijue kwamba kumbe suala la kilio cha wakulima hawa linafahamika hata kwa wabunge ambao kimsingi ni wawakilishi wa wananchi, likiwamo kundi hili maskini.

Kwamba hatua hiyo ya kuhoji mkakati uliopo, kumemwonyesha Muungwana ukweli kuwa bado wapo wawakilishi wa wananchi ambao wanaumia.

Wanaumia kwa jinsi wakulima wanavyohangaikia malipo yao hadi sasa, huku wakipigwa danadana na kampuni zilizochukua pamba yao kutoka kwenye maghala ya Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS).

Wakulima hawa wamepaza kilio chao kwa muda mrefu kwa viongozi wao wakiwamo wakuu wa mikoa na wilaya wenye jukumu la moja kwa moja kushughulikia changamoto za wananchi katika maeneo yao ili walipwe, bila mafanikio.

Na ndiyo maana Muungwana anaungana na Chegeni kuwasemea wakulima hawa kwani ndiyo hasa kazi ya mwakilishi wa wananchi, na kwa hiyo hapaswi kukaa kimya, ila kuendelea kusema hadi pale wakapolipwa fedha zao.

Kingine kilichonivutia ni takwimu zilizotolewa na serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, zilizobainisha kwamba hadi sasa tayari serikali imeshalipa Sh. bilioni 417 kwa wakulima wa zao hilo nchi nzima.

Aidha, Bashe akakiri hilo la baadhi ya wakulima wa pamba ambao hawajalipwa fedha zao kiasi cha Sh. bilioni 50!
Kimsingi, kiasi hicho cha fedha wanachodai wakulima hawa ni kikubwa kwao na kwamba iwapo zingelipwa mapema yumkini zingechangia tija na maendeleo yao kwa ujumla.

Wengi wa wakulima hawa ni wale wadogo wadogo ambao kwao pamba ni chanzo kikubwa cha mapato ya kujenga ustawi wao wa kiuchumi, kijamii, kitamaduni na hata kisiasa wakati mwingine.

Muungwana ana taarifa kwa mfano wa baadhi ya AMCOS katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, kudai hadi sasa mamilioni ya fedha kama ilivyo katika maeneo mengine.

Kwamba kuna AMCOS, zinadai Sh. milioni 60, Sh. milioni 100 na zingine zaidi ya Sh. milioni 100 kutoka kwa kampuni za ununuzi.

Na kwa bahati mbaya ziko kampuni za ununuzi ambazo hazijapeleka fedha kwenye AMCOS kutoka mwezi Agosti hadi leo hii Novemba, na kila zinapoulizwa lini zitapeleka fedha za wakulima, zimekuwa na majibu ya kupiga chenga.

Hayo ni pamoja na kuwa zimepeleka mahesabu ya kilo zilizokusanya kutoka AMCOS benki, hivyo zinasubiri sasa zipewe fedha na benki za kuja kuwalipa wakulima na lugha zingine ambazo zinachosha.

Kuna taarifa vilevile kutoka kwa viongozi wa AMCOS kwamba baadhi ya kampuni za ununuzi wa zao hilo sasa hazipokei tena hata simu za wenyeviti wa vyama vya ushirika wanaoulizia fedha za wakulima na hivyo kuwaacha wakulima wasijue la kufanya.

Kwa wanaojua maisha ya vijijini, mzunguko wa Sh. milioni 60 ama 100 zinazodaiwa na AMCOS kutoka kwa wanunuzi, una maana gani kwa maendeleo ya wanakijiji na kijiji kwa ujumla wake.

Wakati msimu wa kilimo umeshaanza, tayari mbegu za pamba zimeshapelekwa vijijini katika baadhi ya maeneo na mkulima anatakiwa anunue mbegu hizi kwa fedha taslimu na si vinginevyo.

Sasa mkulima huyu anayedai fedha zake, lakini anatakiwa anunue mbegu na mahitaji mengine ya kilimo kama mbolea kwa fedha taslimu, afanyaje?

Ni rai ya Muungwana kwa serikali ichukue hatua stahiki ili wakulima wa pamba wanaodai walipwe na hivyo kuwezesha ustawi wao na tija katika kilimo chao.