Serikali isiridhie programu mzigo kwenye shule binafsi

24Jul 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Serikali isiridhie programu mzigo kwenye shule binafsi

WIKI kadhaa zilizopita wamiliki wa shule binafsi walilalamika kuanzishwa kwa programu zinazowalazimu kuzilipia, na kuitaka Serikali kuzichunguza na hatimaye kuchukua hatua ili kupunguza usumbufu na gharama.

Malalamiko hayo yalitokana na barua waliyoandikiwa na Wizara ya Elimu kuwa imekubali taasisi ya Anti-Poverty and Environment Care (Apec), kutoa mafunzo kwa madereva wa mabasi ya wanafunzi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Dar es Salaam.

Katika barua ya Taasisi hiyo, imependekezwa kwamba madereva wapewe vyeti vya Apec, baada ya mafunzo.

Aidha, wanataka maofisa elimu kata kuendesha ukaguzi na kuchukua hatua kwa madereva ambao hawatakuwa na vyeti vya taasisi hiyo.

Katika malalamiko yao wamiliki wa shule hizo walibainishwa kwamba si mara ya kwanza kwa wizara kuridhia watu na taasisi mbalimbali kuwapelekea programu ambazo huwaingiza kwenye gharama kubwa.

Gharama ambazo wakati mwingine hufikia hadi kiasi cha Sh. 300,000 kwa mtumishi mmoja.

Walikwenda mbali zaidi na kutoa mfano wa programu za madereva zilizoletwa mwaka jana, ambapo shule zilitakiwa kugharimia Sh. 300,000 kwa kila dereva wake kwa mafunzo yalifanyika kwa wiki moja.

Mbaya zaidi wakabainisha kwamba pamoja na gharama hizo hawajawahi kuona mitaala ya vyuo au taasisi hizo.

Kwa kawaida vyeti vya udereva hutolewa na vyuo vilivyosajiliwa na Serikali, vikiwamo vya Veta na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Lakini ni ajabu taasisi binafsi inapofikia hatua ya kuwa na nguvu ya kutoa maelekezo ya kukamatwa madereva iwapo hawataonyesha vyeti vilivyotolewa na taasisi hiyo, na walengwa wakiwa shule binafsi pekee.

Wachambuzi wa elimu wanahoji iweje suala hili lielekezwe kwa madereva wa shule binafsi, huku wa umma ambao ndio husafirisha wanafunzi wengi wakiachwa?

Kwa nini kuwe na makundi mawili ya wanafunzi kwamba wale wa shule binafsi waendeshwe na madereva waliofunzwa vyema na wengine wabaki na vyeti vilivyowawezesha kupata leseni tu?

Usafiri wa umma unategemewa na wanafunzi wengi zaidi na huko ndiko kuna utitiri wa mabaya kama vile matumizi ya lugha chafu kwa wanafunzi bila kujali umri wao.

Hivyo, Muungwana anaona kwamba kama lengo ni kufanya maboresho ili kuwa na maadili, ni vyema mafunzo haya yakawa kwa madereva wote bila ya kubagua.

Vilevile, hili la wamiliki wa shule binafsi kulundikiwa programu nyingi za kulipia kwa ajili ya watumishi wao ni vyema likaangaliwa pia, kwani linaathiri utendaji wa shule hizo.

Kwamba kutakuwa na ongezeko la michango na hivyo wazazi ndio watakaotwishwa mzigo wa kutozwa ada zaidi na wamiliki wa shule.

Na hiyo ni katikati ya kilio cha muda mrefu cha wazazi juu ya ada kubwa inayotozwa na shule binafsi nchini na mara kadhaa Serikali imeahidi kulitazama suala hilo lakini utekelezaji wake umekuwa ni mgumu.

Muungwana haoni umuhimu wa kuongeza mzigo huu kwa wazazi kupitia mafunzo ambayo wamiliki wa shule hawajaridhika nayo.

Kama kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa madereva, uwekwe utaratibu iwe ni sehemu ya elimu wanapokwenda vyuoni.

Mzazi ambaye ni mwajiriwa anatozwa kodi kwenye mshahara wake, anaponunua bidhaa, kama anamiliki gari anatozwa kodi kwenye mafuta, anapolinunua gari anatozwa kodi.

Aidha, anatakiwa kuwa na stika ya nenda kwa usalama, anakata bima kwenye gari yake, anapotumia simu kupiga, kupokea, kutuma fedha nako anakatwa kodi.

Mzazi huyo huyo ambaye anasomesha mwanaye katika shule binafsi kuliko na mazingira mazuri zaidi ya utoaji elimu, nako anakutana na ongezeko la ada linalochangiwa na michango mingi ikiwamo inayoridhiwa na Serikali kupitia taasisi mbalimbali.

Muungwana akiwa ni mzazi, mdau wa elimu na mwanahabari anaona kabisa kwamba jambo hili si sahihi, zaidi ya kuwaumiza wazazi.

Hivyo ni vyema Serikali ikaliangalia kwa umakini mkubwa.