Serikali itoe kipaumbele ajira maofisa ughani kwa Tanzania ya viwanda

14Sep 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Serikali itoe kipaumbele ajira maofisa ughani kwa Tanzania ya viwanda

UZALISHAJI wenye tija katika kilimo nchini unahitajika sana kwa sasa hivi baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kutoa kipaumbele katika Tanzania ya viwanda.

Vyanzo mbalimbali vinabainisha kwamba kushamiri kwa sekta ya viwanda kunaenda sambamba na tija ya uzalishaji kwenye sekta ya kilimo.

Kilimo ni chanzo cha malighafi kwa sekta ya viwanda. Mfano hai ni viwanda vya nguo, sigara, sukari na mafuta.

Lakini kilimo pia kinachangia katika suala zima la usalama wa chakula kwa kuwa ndicho kinatoa chakula kwa rasilimali watu inayofanya kazi viwandani.

Aidha, umuhimu wa kilimo si katika sekta ya viwanda tu, lakini pia ni chanzo cha ajira kwa sehemu kubwa ya Watanzania.

Asilimia takribani 70 ya Watanzania milioni 50 kwa sasa wanategemea kilimo kama chanzo chao kikuu cha kiuchumi.

Kwa hali hiyo uwekezaji mkubwa kwenye sekta hii unamaanisha kulilenga kundi kubwa la Watanzania.

Na uwekezaji ukiwa wa tija kwa maana ya kuwanufaisha walio wengi katika sekta ya kilimo na hivyo kuondokana na umaskini maana yake ni kuwa kundi kubwa basi la wananchi litakuwa limenufaika.

Tafiti zimebainisha pia kuwa wakulima walio wengi ni wale wadogo wadogo ambao kimsingi hulima shamba kuanzia nusu ekari hadi ekari tatu.

Kimsingi kiwango hiki cha eneo si kikubwa vya kutosha na kwa hali hiyo tija inawezekana tu iwapo wakulima hawa watawezeshwa kuendesha kilimo cha kisasa.

Kilimo cha kisasa kwa maana ya matumizi ya pembejeo yanayoambatana na upatikananji wa huduma za ughani kutoka kwa maofisa ughani.

Kimsingi, ni kilimo cha kisasa tu ndicho kinachoweza kuwakwamua wakulima walio wengi ambao ni wadogowadogo.

Hata hivyo, kwa muda mrefu wakulima nchini wamekabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimefanya kilimo chao kisiwe na tija.

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na ugumu wa upatikanaji wa mbegu bora, dawa za kuua wadudu waharibifu wa mazao, mbolea, mashine za kisasa zinazotumia teknolojia rahisi ya kilimo na zinazouzwa bei ndogo.

Lakini pia kuna suala la ugumu wa upatikanaji wa mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha kutokana na masharti magumu ya utoaji wa mikopo, likiwamo sharti la dhamana.

Aidha, uchache wa maofisa ughani ambao ndio walengwa wa Muungwana kwa leo.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha amenukuliwa Bungeni akisema kuwa bado kuna tatizo la upungufu wa maofisa ughani nchini ikilinganishwa na idadi ya maofisa hao wanaotakiwa kuhudumia kila kijiji, kata na wilaya nchini.

Ole Nasha anasema, Tanzania inahitaji jumla ya maofisa ughani 20, 374 kwa ajili ya kutosheleza hitaji la wataalamu hao kwa kila kijiji, kata na wilaya nchini.

Anafafanua kuwa tayari serikali imeshaajiri maofisa ughani 8,756 kufikia mwaka wa fedha 2016/17 sawa na asilimia 43 ya hitaji kamili na kuwa itaendelea kuajiri ili kuziba upungufu huo pale fungu la fedha litakapopatikana.

Kama Muungwana alivyoainisha awali juu ya changamoto lukuki ambazo bado zinaikabili sekta ya kilimo pamoja na juhudi zinazochukuliwa na serikali, bado anaona serikali ingetoa kipaumbele zaidi katika ajira ya maofisa ughani nchini.

Msingi wa hoja yake ni kuwa maofisa ughani ni watu muhimu sana katika suala zima la kuongeza tija ya uzalishaji katika kilimo.

Hii ni kwa sababu ndio wanaopaswa kuelekeza wakulima mbegu zilizo bora, jinsi ya kupanda kisasa, dawa zinazofaa kwa wakulima, matumizi sahihi ya mbolea, uvunaji wa mazao, jinsi ya kuyahifadhi na ushauri mwingine wenye tija kwao.

Na ndiyo maana Muungwana anaiasa basi serikali itoe kipaumbele kikubwa kwenye ajira ya maofisa ughani, ili kuwezesha kilimo chenye tija ambacho ni chachu ya Tanzania ya viwanda.