Serikali itumie kwa tija ushirikiano na Israel

08Nov 2016
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Serikali itumie kwa tija ushirikiano na Israel

TAARIFA kwamba nchi ya Israel imefungua ofisi ya kutolea viza hapa nchini, kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa Watanzania waliokuwa wakilazimika kwenda jijini Nairobi, nchini Kenya, kupata huduma hiyo ni za kufurahisha.

Lakini si za kufurahisha tu, lakini pia zinatia moyo.

Ijumaa wiki iliyopita, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kwa kushirikiana na balozi wa Israel nchini, aliye na makazi yake Kenya, Yahel Vilan, walizindua ofisi hiyo, ambayo iko katika hoteli ya Kilimanjaro ama Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi, wa ofisi hiyo, Balozi Vilan alisema kuwa serikali yake imeamua kufungua ofisi hiyo kama hatua ya kuitikia ombi la Rais John Magufuli la kutaka uhusiano wa nchi hizi mbili uimarishwe zaidi.

Alisema, kwa kufungua ofisi ya viza, alitarajia pande zote zitafaidika na hasa katika nyanja ya utalii.

Kwamba Watanzania watasafiri kwa urahisi kwenda nchini Israel kwa shughuli za kuhiji ama kutembelea vivutio mbalimbai zilivyoko katika nchi hiyo.

Lakini vilevile akasema kuwa, na hata kwa Waisrael, wengi wao sasa watakuwa na fursa ya kuja kwa wingi kuitembelea Tanzania.

Aidha Balozi Vilan alisema, Israel sasa inaichukulia Tanzania kama rafiki yake mkubwa na hasa baada ya Tanzania kuiunga mkono Israel kwenye mgogoro wake na Kamati ya Hifadhi za Dunia (WHC) ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).

Mgogoro huo ulilenga kuitenga Israel na hekalu la kihistoria liliko jijini Jeruslamu nchini Israel.

Aidha Vilan alisema, Israel kama nchi iliyoendelea sana kisayansi na katika teknolojia ya maji, umwagiliaji, afya, ujenzi na masuala ya usalama, iko tayari kushirikiana na Tanzania katika maeneo hayo kwa ustawi wa watu wa nchi zote mbili.

Ni katika kipande hiki ndicho kilichomvutia Muungwana kulonga leo katika safu hii.

Muungwana analonga leo kwanza akikiri kuwa, ni kitu chema kuzidi kuimarisha uhusiano na Israel kwa mantiki ya kidiplomasia.

Kwamba maadamu serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwaletea wananchi wake maendeleo kwa kutumia vyanzo vyote vinavyopatikana, diplomasia ya uchumi ni mojawapo ya vyanzo vinavyoweza kulitimiza hilo, kwa mapana.

Kwamba nchi yeyote ile iliyo tayari kwa ajili ya ushirikiano na Tanzania, kama tulivyoshuhudia hivi karibuni katika ziara ya mfalme Mohammed VI wa Morocco, ikikaribishwa ili mradi uhusiano uwe na manufaa kwa pande zote mbili.

Lakini kwa Israel, kuna faida kubwa zaidi kwa Tanzania, kutumia maendeleo ya kiteknolojia na uzoefu wa taifa hilo katika nyanja alizozitaja balozi Vilan kuwa wako tayari kwa ushirikiano, yaani kwenye teknolojia ya maji, umwagiliaji, afya, ujenzi na masuala ya usalama.

Kubwa ambalo Muungwana anadhani Tanzania inaweza kuanza nalo moja kwa moja ni lile la masuala ya usalama.

Tanzania sasa inakabiliwa na changamoto kubwa katika eneo hili, na hasa upande wa uwindaji haramu ambao umesababisha rasilimali nyingi za taifa kuteketea karibu kila siku na hasa wanyama kama tembo.

Serikali ya Dk. Magufuli inaendesha operesheni kabambe ya kuwakamata majangili na wafadhili wakubwa wa biashara ya pembe za ndovu, na tayari kuna majangili yaliyokamatwa akiwa na nyara hizo za serikali.

Sasa iwapo serikali itatumia vizuri ubobezi na uzoefu wa Israel katika masuala ya ulinzi na usalama, yumkini itasaidia kuwakamata wahusika kabla hawajafanya ujangili, badala ya kuwafuatilia pale wanapokuwa tayari wameshafanya ujangili wao.

Kwamba, itakuwa ni vizuri kuwakamata majangili kabla hawajaua tayari wanyama wetu, na hili linawezekana kama tutashirikiana na Israel.

Ni kwa msingi huo ndipo Muungwana anapoishauri serikali kutumia kwa ukamilifu utayari huu wa Israel wa kushirikiana na Tanzania, ili iweze kutokomeza janga la ujangili haraka.