Serikali iwamulike kwa kina wanaokuja kuwekeza bangi

12Feb 2020
Beatrice Moses
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Serikali iwamulike kwa kina wanaokuja kuwekeza bangi

MAMLAKA za kiusalama nchini hivi karibuni, zimemkamata mwekezaji raia ya Poland, akiwa amelima bangi kwenye eneo lake alilokabidhiwa kwa uwekezaji wa hoteli na kituo cha yatima.

Taarifa kutoka kwa wananchi ndizo zinatajwa kuwa chanzo kilichowezessha kukamatwa kwa mwekezaji huyo, ambaye kwa hakika kama serikali isingechukua hatua za haraka, ni wazi angesababisha uharibifu mkubwa, ikiwamo kuchochea uhalifu katika eneo la utalii mkoa wa Kilimanjaro.

Serikali imekuwa ikihamasisha na kufanya jitihada za kuboresha mazingira ya uwekezaji na katika juhudi zake za mwka jana, ilitangaza kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996.

Ni sera iliyotungwa, ikiwa sehemu mojawapo ya jitihada za serikali kutatua changamoto zinazoikabili nchi katika kufikia matumizi bora ya rasilimali zake, ili kuwezesha kunufaika na kufikia malengo ya kiuchumi pia kijamii.

Ilibainisha wazi kwamba, mapitio hayo yanafanyika kutokana na mabadiliko mbalimbali ya mazingira ya biashara na uwekezaji katika ngazi za kitaifa, kikanda na dunia tangu kutungwa sera hiyo mwaka 1996.

Aidha, mapitio hayo yanadaiwa yatawezesha kutungwa sera mpya ya uwekezaji na kuandaa mkakati wa utekelezaji utakaowezesha nchi kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kwa haraka.

Pia, itakuwa ni kutumia ipasavyo fursa zitakazotokana na uchumi wa kati na ilibainishwa kwamba, kazi hiyo inazingatia dhana ya uwazi na ushirikishwaji wa wadau wote muhimu.

Kitendo cha mwekezaji huyo ni kuhujumu juhudi zinazofanywa na serikali, kwa taarifa za awali alijitambulisha kuwekeza kwenye kituo cha yatima na hoteli tajwa.

Vyombo vya habari nchini viliripoti tukio la kukamatwa kwa mwekezaji huyo, ikibainishwa kuwa alianza kazi hiyo ya kuzalisha bangi na kuuza katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Inadaiwa baada ya kukamatwa, mwekezaji huyo alijaribu kuwashawishi maofisa waliokuwa katika kikosi kazi hicho kupokea rushwa ya Sh. milioni 10, ili ‘mambo yaishe’ na aliahidi kuwalipa kila baada ya mwezi mmoja, fedha Sh. milioni 40.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, ni kwamba aliingia nchini kwa ajili ya kuwekeza katika ujenzi wa hoteli za kitalii, karibu na uso wa Mlima Kilimanjaro, eneo la Njiapanda Himo katika Wilaya ya Moshi.

Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya nchini, James Kaji, alithibitisha kukamatwa kwa mwekezaji huyo na wenzake watatu, akiwamo mkewe.

Mwekezaji huyo anadaiwa kuingiza nchini aina mpya ya mbegu ya bangi kutoka Hispania na aliileta mkoani Kilimanjaro, ambako amekuwa akiivuna katika eneo maalum lililozungushwa uzio mrefu wa tofali.

Hapo anadiwa aliichakata kwa kutengeneza malighafi mfano wa ‘asali na jam’ inayouzwa zaidi katika masoko ya nje, kupitia mipaka ya Pangani, Tanga na Zanzibar.

Ni mwekezaji anayetajwa kuendesha kilimo hicho haramu tofauti na maelezo yake ya uwekezaji na kwa mujibu taarifa ya awali ya Kamishna Jenerali Kaji, kuna baadhi ya wateja wa bangi inayozalishwa na mwekezaji huyo, wanaokuja kutoka Ulaya.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, alibainisha kuwa sema, Tanzania inaongoza kwa uwekezaji Afrika Mashariki na imemudu kuvutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.18.

Majaliwa katika uwasilisho wake, kupitia Taarifa ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na makadirio ya mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2019/2020, kwenye mkutano wa 15 wa Bunge.

Uganda inatajwa kufuata kwa Dola za Marekani milioni 700, na Kenya dola za Marekani milioni 670.

Ripoti mbalimbali za uwekezaji duniani zinaonyesha Tanzania imeongoza kwa kuvutia uwekezaji miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki.

Taarifa ya Uwekezaji ya Dunia (World Investment Report) ya mwaka 2018 kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) inabainisha kiasi hicho cha uwekezaji.

“Taarifa nyingine ya ‘The Africa Investment Index (AII) 2018’ inaonyesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 13 kati ya nchi 54 za Afrika katika kutoa fursa za masoko na vivutio vya uwekezaji.”

Vilevile, Waziri Mkuu anasema kuwa taarifa iitwayo ‘Where to Invest in Africa’ (wapi kla kuwekeza Afrika) ya mwaka 2018, nayo imeonyesha Tanzania imeshika nafasi ya saba kati ya nchi 52 zinazovutia zaidi kwa uwekezaji barani Afrika.

Waziri Mkuu aliahidi kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwamo kutekeleza mapendekezo ya Mpango Kazi Jumuishi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini.

Naamini kuwa serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kutoa taarifa kwa vyombo husika mara wanapobaini kuwa kuna matukio yasiyo ya kawaida yanatendeka katika maeneo yao ya kazi au makazi.