Serikali iwezeshe kununuliwa pamba ya wakulima nchini

02Jul 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Serikali iwezeshe kununuliwa pamba ya wakulima nchini

ILI kuhalalisha tulonge yangu, ninaanza kwa kuitalii Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 hadi 2020.

Kimsingi Ilani hiyo inasisitiza vipaumbele vinne ambavyo ni pamoja na vita dhidi ya rushwa na ufisadi, kutengeneza ajira na kuendeleza kwa kiwango cha juu hali ya ulinzi na usalama wa taifa letu.

Lakini kipaumbele cha nne ni kuendeleza vita dhidi ya umaskini nchini, ambayo ndiyo mada ya leo.

Vita dhidi ya umaskini ni moja ya vipaumbele vilivyoko katika Ilani ya CCM, na kwa namna hiyo, tija yoyote inayogusa ustawi wa Watanzania walio wengi nchini, nikimaanisha wakulima, si ya kuiweka kapuni.

Kwa hivi sasa kuna kilio ambacho kinazidi kuripotiwa karibu kila siku na vyombo vya habari, cha wakulima wa pamba kutoka maeneo mbalimbali, wakiwa hawajui hatima ya pamba yao ambayo wameihifadhi majumbani mwao.

Wanaendelea kuihifadhi kwasababu hawana cha kufanya kwa kuwa hakuna kampuni ama wanunuzi wa zao hilo waliojitokeza kuinunua, pamoja na msimu wa ununuzi kuzinduliwa kutoka Mei 2, mwaka huu, takribani miezi miwili sasa.

Muungwana amekwishaandika tena juu ya kadhia hii inayoendelea kudidimiza wakulima wa pamba kiuchumi, kwa kuwa matarajio yao yanaonekana kutolipa hadi sasa.

Na hii ni baada ya jitihada kubwa walizozifanya za kuongeza tija katika uzalishaji kutokana na hamasa ya wadau, serikali ikiwamo.

Cha kusikitisha hata baadhi ya wakulima waliopeleka pamba yao kwenye Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS), wakitarajia itanunuliwa, wameambulia kuorodheshwa majina katika baadhi ya maeneo kwa ahadi kwamba watalipwa fedha zikija.

Kuna tukio la pamba kupakiwa kwenye magari ili iondoshwe katika moja ya maeneo mkoani Simiyu, bila ya wakulima kulipwa fedha zao.

Ni bahati kwamba wakulima walishtuka mapema na hivyo kuzuia magari, wakitaka kwanza walipwe fedha zao.

Taarifa zinasema hatua yao hiyo ilipata nguvu baada ya Mkuu wa Wilaya kuingilia kati na kuagiza pamba hiyo isichukuliwe hadi pale wakulima watakapolipwa fedha zao.

Aidha, mkuu huyo akaagiza pamba ya wakulima isikopwe kwa namna yoyote bila ya kununuliwa kwa fedha taslimu na kwa bei elekezi ya Sh. 1,200.

Liko pia tukio la baadhi ya wakulima waliopeleka pamba yao kwenye vyama vya ushirika vya msingi kwa ajili ya kuiuza na wakaamua kurudi nayo nyumbani, baada ya kukuta hakuna fedha.

Hatua kama hii ina athari ya moja kwa moja kwa mkulima, kwa maana ya ubora wa pamba yake.

Kwamba inaposafirishwa kwa tela ya kukokotwa na maksai kwa mfano kutoka nyumbani kwenda AMCOS na kisha kurudishwa nyumbani tena, ubora unaathirika.

Kwamba kuna masuala ya vumbi la njiani kwenda na kurudi, suala la kushusha na kupakia tena, hivyo kuathiri zaidi pato la mkulima huyu na dhana nzima ya kupambana na umaskini, kama inavyobainishwa kwenye Ilani ya CCM.

Kimsingi matokeo ya wakulima kutonunuliwa pamba yao hadi sasa, yanakwamisha jitihada za kuboresha maisha yao.

Muungwana anasema hivyo akiwa ni mtu anayetoka Kanda ya Ziwa na hivyo anaelewa maendeleo ambayo hupatikana kwa mtu binafsi, kaya na maeneo mbalimbali ya Kanda hiyo, pale msimu wa pamba unapozinduliwa na wakulima kuuza pamba yao.

Mbali na kutimiza majukumu yao kama ya kulipia ada na mahitaji ya shule kwa watoto, kipindi hiki huwa ni cha kuboresha makazi, kununua vyombo vya usafiri, mifugo na rasilimali zingine.

Muungwana anaendelea kutoa rai kwa serikali yetu sikivu kuwasaidia wakulima hawa kwa sababu kampuni za ununuzi wa pamba zinaonekana kama ‘zina kamgomo’ ambako sababu zake hazijawa wazi.

Nimesema kupambana na umaskini ni moja ya vipaumbele vya Ilani ya CCM, na kwa maana hiyo kununua pamba ya wakulima hawa ni muhimu katika dhima nzima ya kupambana na adui huyo.