Serikali iwezeshe vyama ushirika kununua mazao ya wakulima

06Aug 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Serikali iwezeshe vyama ushirika kununua mazao ya wakulima

NILITAKA nisiendeleze ajenda ya kusuasua kwa ununuzi wa pamba ya wakulima wiki hii, nikiwa na imani kwamba suluhisho lake lingemalizwa kesho kutwa, siku ya Nanenane na Rais John Magufuli mkoani Simiyu.

Rais Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maonyesho na Maadhimisho ya Nanenane mwaka huu, yanayoendelea kwenye viwanja vya Nyakabindi, wilayani Bariadi mkoani Simiyu, moja ya mikoa inayolima kwa wingi zao la pamba.

Nilitaka nisizungumzie lolote juu ya kadhia hiyo kwa wiki hii ili nikiwa na imani kwamba kuna ambacho atasema juu ya kero hii ambayo bado ni adha kwa wakulima ambao hawajalipwa fedha baada ya kuuza pamba yao.

Lakini si kwa hao tu ambao tayari wameshauza pamba yao ambayo bado imehifadhiwa kwenye maghala ya Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS), pia kwa wakulima ambao bado hawajaiuza kabisa.

Kuna wakulima wengi wenye pamba majumbani, wakisubiri iliyo tayari kwenye maghala ya AMCOS isafirishwe, ili nafasi ipatikane ya kuhifadhi pamba nyingine na fedha za kutosha zipelekwe.

Hata hivyo, Muungwana amelazimika aendeleze ajenda hii ya kusuasua ununuzi wa zao hili, akichagizwa na hatua ya serikali kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ya kuendelea kulishughulikia kwa dhati suala hili.

Ikumbukwe kuwa tangu msimu wa uuzaji wa zao hili ulipoanza Mei 2, mwaka huu, serikali imekuwa ikichukua kila jitihada za kuhakikisha wakulima wanauza pamba yao, tena kwa bei yenye tija.

Ilichukua hatua ya kusimamia bila ya ‘kupepesa macho’ bei elekezi ya Sh. 1,200 kwa kilo kinyume na zilizokuwa zinatolewa na wanunuzi binafsi za kati ya Sh. 500 hadi Sh. 800 kwa kilo.

Lakini ikatoa pia dhamana kwenye benki mbalimbali kuwezesha kampuni za ununuzi kukopa fedha ili zinunue pamba ya wakulima.

Hatua hiyo ilifuatia madai ya kampuni za  ununuzi kwamba benki zinasita kutoa mikopo kwao kwa madai kuwa bei ya pamba kwenye soko la dunia imeshuka na hivyo kukosekana uhakika wa mikopo kurejeshwa.

Aidha, serikali ikatoa maelekezo ili kufikia Julai 30, pamba yote iwe imenunuliwa kutoka kwa wakulima, ingawaje elekezo hili halikutekelezwa ipasavyo.

Katika kuhakikisha suluhu ya changamoto hii inapatikana, wiki iliyopita Agosti 2, Waziri Mkuu alikutana kwa mara nyingine na wanunuzi wa pamba, wamiliki wa benki na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Vilevile Agosti 3, akazungumza na Wakuu wa Mikoa minane inayolima pamba ya Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Geita, Kagera, Mara, Tabora na Singida, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB.

Katika mikutano hiyo, Majaliwa ameagiza benki zilizoko katika maeneo yanayolima pamba zihakikishe taratibu zimekamilika ili kampuni za ununuzi zipate mikopo na ununuzi uwe umeanza kwa nguvu kuanzia jana Jumatatu.

Ni bahati nzuri kwamba mikutano hiyo ya Majaliwa ilihudhuriwa pia na mwenyekiti wa wanunuzi wa zao hilo Christopher Gachuma, ambaye aliagizwa kuweka utaratibu madhubuti wa ufuatiliaji ili kujua kiasi cha pamba iliyonunuliwa, kutoka kwa nani na wapi.

Muungwana ana imani kwamba kwa agizo hili la sasa la serikali pamba yote ya wakulima itanunuliwa na hivyo kuondoa kero hiyo kwao.

Pamoja na juhudi hizo zote za serikali, Muungwana anaona wakati umefika sasa kwa serikali kuwezesha vyama vya ushirika vya mikoa kushiriki kwenye ununuzi wa mazao ya wakulima ili kuepusha adha kama hizi zinazoendelea kwenye zao la pamba.

Anasema hivyo kutokana na somo lililopatikana kwenye kadhia ya zao la korosho na sasa pamba.

Kwamba hata kama wanunuzi binafsi wataendelea kuwapo, lakini hatua hiyo itatoa uhakika wa mazao ya wakulima kununuliwa kwa hali yoyote zikiwamo za  wanunuzi binafsi kusuasua kama ilivyo sasa.