Serikali izungumzie kusuasua ununuzi pamba ya wakulima

25Jun 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Serikali izungumzie kusuasua ununuzi pamba ya wakulima

MSIMU mpya wa ununuzi wa pamba ulizinduliwa rasmi Mei 2, mwaka huu mkoani Katavi, huku serikali ikitangaza bei mpya ya zao hilo kuwa Sh. 1,200 kwa kilo.

Hilo ni ongezeko la Sh. 100 kwa kulinganisha na bei ya msimu uliopita ambayo ilikuwa ni Sh. 1,100 kwa kilo.

Kuzinduliwa kwa msimu huo kulifungua rasmi ununuzi wa zao hilo karibu katika maeneo yote yanayolima, ukianzia na Kanda ya Ziwa inayoundwa na mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara, Geita, Mwanza na Kagera.

Ipo pia mikoa katika baadhi ya kanda inayolima zao hilo, kama Tabora ulio Kanda ya Magharibi na Singida ulio Kanda ya Kati.

Katika mlolongo huo unaingia mkoa wa Katavi, ambao kimsingi uko katika msimu wake wa pili wa kilimo hicho tangu kianzishwe mkoani humo.

Pamoja na changamoto mbalimbali ambazo wakulima wamekuwa wakikumbana nazo, rekodi zinaonyesha kwamba katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, wakulima wamehamasika kuongeza uzalishaji.

Kwamba changamoto za upatikanaji usio wa uhakika wa pembejeo kwa wakati na huduma za ugani unaotokana na uchache wa maofisa ugani kwa kutaja baadhi, hazikukwamisha juhudi zao.

Na ndiyo maana kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba (TCB), Marko Mtunga, uzalishaji wa zao hilo kwa mwaka huu unatarajiwa kuongezeka hadi kufikia zaidi ya tani 400,000 kutoka takribani tani 200, 000 za msimu uliopita.

Hii inathibitisha namna wakulima wa zao hilo la kibiashara linalotegemewa na wengi walivyohamasika kuongeza tija katika uzalishaji, japokuwa bado ekari moja ya pamba kwa wastani inatoa kilo 300 kwa sasa.

Kuna uwezekano hata hivyo wa ekari moja kutoa kilo 1000, iwapo changamoto zilizopo zitatatuliwa.

Pamoja na juhudi hizo za wakulima za kuongeza tija wakiamini watapata kipato cha kuonekana katika dhima nzima ya kupambana na umaskini kwa ujumla wake, kuna taarifa kwamba ununuzi wa zao hilo ni wa kusuasua.

Bado kuna pamba nyingi ya wakulima haijanunuliwa kabisa hadi sasa karibu miezi miwili tangu kuzinduliwa kwa msimu na kampuni za ununuzi zikionekana kutotoa kipaumbele kinachostahili.

Kwamba wakulima wa zao hilo wamebaki wameduwaa wakisikilizia kampuni za ununuzi ziinunue pamba yao!

Muungwana akiwa ni miongoni mwa watu wanaotoka Kanda ya Ziwa anadhani kuna haja ya serikali kuingilia kati suala hili sasa.

Anasema hivyo kwa sababu inaonekana kwenye kadhia hii ya pamba ni kama vile inataka kufanana na sakata lililotokea kwenye zao la korosho.

Ikumbukwe kuwa kabla ya serikali kuingilia kati suala la ununuzi wa korosho, wanunuzi wa zao hilo walitaka kuinunua korosho kwa bei ya chini ya shilingi 3,000, ambayo ilikuwa haiwalipi wakulima.

Kuna maeneo ambayo tayari baadhi ya wanunuaji wa pamba walikuwa wameshaanza kununua kwa bei ya chini ya shilingi 1,000 kwa kilo, hali iliyowafanya baadhi ya wakuu wa wilaya kuingilia kati na kupiga marufuku kitendo hicho.

Kilio cha kusuasua kwa ununuzi wa zao hili kimeibuliwa pia bungeni na Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa ambaye ameitaka serikali iingilie kati suala hili kwani hali ya kiuchumi ya wakulima wa pamba walio wengi si nzuri.

Si nzuri katika mantiki ya kawaida tu kwamba wanategemea pamba ili waishi na kwamba pamba kwao ni siasa vilevile, sasa kama pamba yao hainunuliwi, maendeleo yao ya kimaisha yatakuwa ndiyo yanakwamishwa hivyo.

Pengine wakati umefika kwa serikali kuchukua uamuzi sasa kuhakikisha pamba ya wakulima inanunuliwa, tena kwa bei iliyotangazwa ili kuboresha maisha ya wakulima hawa.

Ieleweke kwamba wakulima hawa wametumia raslimali zao, nguvu zao na muda kuzalisha pamba wakitarajia waiuze ili watatue matatizo yao ya kiuchumi.

Sasa danadana zinapoanza kutoka kwa wanunuaji inakuwa haieleweki, hivyo ni vyema serikali ikasema katika hili.