Serikali sikivu imewasikia, sasa visizingizio visiwepo Ligi Kuu

08Jun 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Serikali sikivu imewasikia, sasa visizingizio visiwepo Ligi Kuu

WIKI kadhaa zilizopita klabu mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara, hasa zile zilizoonekana zipo chini ya msimamo zilikuwa zikipinga ligi hiyo kuchezwa kwa vituo.

Ikumbukwe baada ya serikali kuruhusu michezo kurejea, awali ilitangaza Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara kuchezwa kwa vituo.

Na Ligi Kuu inayotarajiwa kuanza kupigwa Jumamosi ilitakiwa kuchezwa Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar ers Salaam, Uhuru na Azam Complex na Ligi Daraja la Kwanza na la Pili ilipangwa Kituo cha Mwanza, katika Uwanja wa CCM Kirumba na Nyamagana.

Viongozi wa klabu za Ndanda, Mbeya City, Mbao FC, Ruvu Shooting, Singida United na nyingine ambazo ukiangalia kwenye msimamo wa ligi haziko nafasi nzuri, walionekana kupinga mfumo huo, wakitaka urejeshwe ule ule wa zamani wa nyumbani na ugenini.

Nakumbuka wakati huo, serikali ilikuwa bado haijatangaza ruhusa ya mashabiki kuingia uwanjani, lakini bado viongozi hao wakataka timu zao zicheze nyumbani na ugenini, ili zipate faida ya kucheza nyumbani, hata kama uwanja utakuwa ni mtupu.

Nakumbuka msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire alikuja na mahesabu ya kuishi Dar kwa siku 30, matumizi ya hoteli, chakula na usafiri wa ndani.

Katika kukokotoa mahesabu yake, ikaonekana kuwa kuishi Dar itakuwa ghali zaidi tofauti na timu kusafiri kwenda mikoani kucheza mechi zao zilizosalia kwa sababu huko, zitakuwa zikikaa siku moja na kurejea makwao.

Serikali sikivu ikasikia kilio chao. ikaruhusu mechi kuchezwa nyumbani na ugenini, lakini kizuri zaidi ikaruhusu na mashabiki kuingia japo ni lazima tahadhari zote za ugonjwa wa Covid-19, unaosababishwa na virusi ya corona, lazima zizingatiwe.

Kwa uzoefu wangu wa masuala ya michezo, nilielewa ni kwa nini viongozi wengi walikuwa wakipinga mechi zilizobaki za Ligi Kuu msimu wa 2019/20 uliosimama tangu Machi 17, mwaka huu kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19.

Ni kwamba timu nyingi ambazo ziko kwenye ukanda wa hatari, zilikuwa zinaogopa kucheza Dar, badala yake zilikuwa zinataka kucheza nyumbani ili kupata sapoti kwa ajili ya kuhakikisha hazishuki daraja.

Hofu ya kurudi Ligi Daraja la Kwanza ndiyo iliyokuwa ikizikumba timu hizo kiasi cha kutaka ligi iendelee kwa mtindo ule ule, zikitegemea kufanya vema kwenye mechi zao zitakazocheza nyumbani.

Mimi sitaki kujua, ni kitu gani ambacho wanategemea zaidi, au wana uhakika kuwa timu zao zitakuwa zikipata ushindi zinapokuwa nyumbani, lakini tayari zimeshapata faida hiyo.

Kila timu sasa itacheza nyumbani na ugenini. Kila moja inatakiwa kuchanga karata zake vizuri na kushinda mechi, si za nyumbani tu, bali hata ugenini.

Tumeona msimu huu baadhi ya timu zikishinda hata ugenini. Mfano Coastal Union, iliichapa Namungo FC mabao 3-1 Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.

Naipongeza serikali kwa kurudisha mfumo ule ule kwa sababu baadhi ya timu zingepata visingizio kama zingepoteza mechi zake, au kushuka daraja.

Lakini kwa sasa hakuna visingizio tena. Mtindo ni ule ule, nyumbani na ugenini. Timu inayojiweza ishinde ugenini na nyumbani. Hata zile timu zinazoshinda nyumbani tu, haina tatizo, lakini mwisho wa siku pointi ndizo zitaamua.

Kwa sasa hatuhitaji visingizio tena, timu zitakazobaki zitakuwa zimebaki kwa uwezo wao na zile zitakazoshuka zitashuka kwa sababu hazikuwa na uwezo wa kushindana na si kwa sababu mechi zake zimechezea Dar es Salaam, au nje ya mkoa wao.