Serikali za mitaa zihusishwe kikamilifu kupambana na magonjwa ya mlipo

28May 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Serikali za mitaa zihusishwe kikamilifu kupambana na magonjwa ya mlipo

‘MTU ni Afya’ ni moja ya kampeni kubwa iliyoendeshwa na serikali ya awamu ya kwanza kwenye miaka ya 1970, ambayo kama zilivyo kampeni zingine za kiafya ililenga kuboresha ustawi wa wananchi.

Ni katika dhamira ileile ya kupambana na maradhi, moja ya maadui wakubwa watatu waliotangazwa na serikali chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, wengine wakiwa umaskini na ujinga.

Kampeni hii ya ‘Mtu ni Afya’ ilikuwa na malengo matatu mahsusi lakini mawili kwa minajili ya Muungwana leo ilikuwa ni pamoja na kuongeza ufahamu kwa watu.

Ufahamu wa namna ya kuwa na maisha yenye afya kwa kuhamasisha vikundi na watu binafsi kuchukua hatua stahiki zinazotakiwa ili kulifikia lengo hilo.

Hatua za kutunza mazingira katika makazi wanayoishi kwa kuyaweka katika hali ya usafi, kuwa na vyoo bora, kunawa mikono kwa kutumia sabuni kabla na baada ya kula, mtu anapotoka msalani, mambo yaliyo ya msingi katika suala zima la kuzuia magonjwa.

Lengo lingine lilikuwa kutoa taarifa wazi na rahisi kuhusiana na dalili za magonjwa maalumu yakiwamo ya mlipuko na namna ya kuyazuia.

Kampeni hiyo iliyoendeshwa kwa njia mbalimbali kama vile kupitia kwenye vyombo vya habari, mikutano na vipindi vya darasani shuleni na kwenye mafunzo ya elimu ya watu wazima ilikuwa na mafanikio makubwa.

Pamoja na kwamba bado adui maradhi anaendelea kuwapo miongo kadhaa sasa ikiwa imepita, lakini Muungwana anadiriki kusema ushirikiano wa Watanzania wa wakati huo uliwezesha kampeni hiyo kufanikiwa.

Na ndiyo maana Tanzania ikawa mfano kwa mataifa mengine kupitia kampeni hii kama ilivyo kwa kampeni zingine ilizozizindua nyakati hizo, ikiwamo ya ‘Elimu kwa Wote-UPE.’

Hata hivyo, Muungwana anashangaa kwa nini ushirikiano kama huo wa kampeni ya ‘Mtu ni Afya’ haupo zama hizi akiangalia namna baadhi ya wananchi wanavyozembea kuchukua hatua zinazoelekezwa na mamlaka kwa faida ya afya zao.

Kuna mlipuko wa homa ya dengue katika baadhi ya mikoa nchini kwa hivi sasa, Dar es Salaam ikiongoza na elimu ya kujikinga na ugonjwa huo tayari inaendelea kutolewa na serikali kupitia wizara ya Afya nchini.

Na katika hili serikali imeelekeza mikoa na halmashauri zote kuchukua hatua za kudhibiti ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kunyunyizia dawa ya kuua viluwiluwi, kufukia madimbwi ya maji, kufyeka vichaka na kufunika mashimo ya maji taka.

Muungwana alitarajia wananchi kutoa ushirikiano kwa kufuata maelekezo ya mamlaka kwa ustawi wa afya zao kama ilivyokuwa nyakati za kampeni ya ‘Mtu ni Afya.’

Katikati ya janga hili la homa ya dengue na ikionyesha namna baadhi ya wananchi wasivyofuata maelekezo ya serikali, kumeripotiwa kuibuka tena ugonjwa wa kipindupindu katika Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Naibu Meya wa manispaa hiyo Omari Kumbilamoto, sababu ya mlipuko huo ni baadhi ya wakazi kutiririsha majitaka kutoka katika vyoo vyao kwenye maji yanayotumiwa na wananchi.

Sasa kama hali ndiyo hii katika zama hizi ambapo kampeni ya ‘Mtu ni Afya’ ina miongo kadhaa, adui maradhi atafutika lini?

Ni rai ya Muungwana kwa serikali kupitia kwa maofisa afya katika halmashauri kutoa mamlaka ya kutosha kwa wenyeviti wa serikali za mitaa kusimamia ipasavyo suala la usafi wa mazingira.

Na hiyo si kwa kuwatoza faini tu wale wanaofungulia maji taka ya vyooni kwenda kwenye maji yanayotumiwa na wananchi, bali kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Zama hizi za Watanzania takribani milioni 55 waliopiga hatua kubwa kielimu huku karibu kila kata ikiwa na shule ya sekondari, si za mlipuko tena wa kipindupindu kila mwaka na magonjwa mengine kama homa ya dengue.