Sheria inavyomshika mzazi, mlezi wajibu wa matibabu

01Jun 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Sheria inavyomshika mzazi, mlezi wajibu wa matibabu

MTU unapoulizwa mtoto ni nani, unaweza kujibu vipi? Kwa mujibu wa Kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto wa Mwaka 1989; huyo ni kila binadamu aliye chini ya umri wa miaka 18.

Haki za msingi za mtoto zinatajwa kwa ujumla wake, ni zinazolindwa na mkataba tajwa juu, ambao Tanzania ni mshirika tangu Julai 10, mwaka 1991.

Ni haki zilizogawanyika katika makundi makuu manne, ambayo ni: Haki ya kuishi kwenye mazingira mazuri ikiwemo kupata lishe bora; haki ya kuendelea, kukua ikiwemo haki ya kupata elimu na haki ya kucheza.

Pia, inatajwa kujumuisha haki ya kulindwa na wazazi, walezi, jamii na serikali dhidi ya madhara, ikienda sanjari na haki ya kushiriki katika masuala yanayomgusa. Sehemu ya II, katika kifungu cha 5-7 na Sheria ya Mtoto, ya Mwaka 2009 ndiko inakoangukia.

Katika kuendelea jambo mahsusi, kuna suala la: “Wajibu wa kumlea Mtoto.” Hapo kuna haki yake ya msingi ya kupatiwa matibabu pale inapohitajika kufanya hivyo. Hiyo ni kwa mujibu wa Kifungu cha 8 (3) cha Sheria ya Mtoto, 2009.

Baadhi ya nukuu:“Mtu yeyote haruhusiwi kumkatalia, kukataza, kuzuia huduma za uangalizi wa kimatibabu kwa Mtoto, kwa sababu za imani za kidini au imani nyingine zozote zile.”

Mwongozo wa Sheria hiyo unagusa kifungu cha 206 na kile cha 207, vyote vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, kwa maana ya kuipatia maana au mantiki sahihi. Katika hilo inagusa kinachoitwa “Wajibu husika ambao upo kwa mujibu wa Sheria.”

Nyingine inasema:“Itakuwa ni wajibu wa kila mtu mwenye uangalizi juu ya mtu mwingine (ikiwemo/ kujumuisha na watoto) ambaye kwa sababu ya umri, maradhi, upungufu wa akili, kuwekwa kizuizini au kwa sababu nyingine yoyote itakayomfanya asiweze kujiangalia nafsi yake na ambaye hawezi kujipatia mahitaji ya maisha.

“Ama, uangalizi huo ni kwa kuajiriwa au kutokana na sheria au kutokana na kitendo chochote cha halali au kisichokuwa cha halali cha muangalizi huyo, kumpatia mtu huyo mwingine mahitaji ya maisha na atahesabiwa kusababisha matokeo yoyote yanayoweza kudhuru maisha au afya ya mtu huyo mwingine, kwa sababu ya kuacha kufanya wajibu wake huo.

“Pia, ni wajibu wa kila mtu ambaye kama mkuu wa familia, ana uangalizi wa mtoto aliye na umri wa chini ya miaka 18 akiwa ni mmoja wa watu wa nyumbani kwake, kumpatia mtoto huyo mahitaji ya lazima ya maisha, (ikiwemo na matibabu) na atahesabiwa kusababisha matokeo yoyote yenye kudhuru maisha au afya ya mtoto huyo, kwa sababu ya kuacha kutekeleza wajibu wake huo,” inaeleza.

Kwa mujibu wa elekezo la Kifungu cha 229 na sheria hiyo, mtu yeyote anayepewa wajibu wa kutoa mahitaji ya lazima ya maisha ya mtu mwingine na bila sababu ya msingi, anashindwa kufanya hivyo, anasababisha maisha ya mtu mwingine huyo kuwa hatarini au huenda yakawa hatarini au afya yake kudhurika au huenda ikadhurika daima, atakuwa anatenda kosa na atahukumiwa kifungo cha miaka mitatu.

Kwa hiyo, kwa wale wenye utamaduni wa kukwepa kuwapeleka watoto hospitalini kupata huduma za afya, wafahamu sheria inawaelekezea jicho la kuwaadhibu.!

Sababu za kuwapo ulinzi wa haki za mtoto, ni kuwapatia uzito stahiki wa haki zao za kibinadamu.

 Watoto ni binadamu, wana haki sawa; watoto hawana sauti ya kujisemea au uwezo wa kupigania haki binafsi.

Pia, kuna ongezeko la wimbi kubwa la ukiukwaji haki za watoto, mfano hai ukatili dhidi ya mtoto, mateso, kupuuzia hali za afya zao kwa uzembe na makusudi bila ya kuwa na sababu za msingi. Naomba kuwasilisha.