Si Mafisango tu, Tindwa pia akumbukwe Simba

20May 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Mjadala
Si Mafisango tu, Tindwa pia akumbukwe Simba

ITAKUWA ni Mei 30, klabu ya Simba itakapofanya hafla ya utoaji tuzo kwa wachezaji, viongozi, wanachama na mashabiki wake kwenye Hoteli ya Hyatt Regency iliyopo jijini Dar es Salaam.

Huu utakuwa ni msimu wa pili kwa tuzo hizo zinazojulikana kama Tuzo za Mo, zilizoanza kufanyika mwaka jana.

Zilianzishwa kwa lengo moja la klabu kutambua mchango wa watu wote wa familia ya soka kwenye klabu hiyo kongwe ya Simba.

Kwa upande wa wachezaji wanaowania ni James Kotei, Mzamiru Yassin na Jonas Mkude kwa kipengele cha kiungo bora wa mwaka 2019, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi wao wakishindana kwenye kipengele cha Mshambuliaji Bora wa Mwaka, pia kwenye kipengele cha Mchezaji Bora wa Mwaka wamo John Bocco, Meddie Kagere na Clatous Chama.

Upande wa makipa, Aishi Manula anashindana na msaidizi wake Deogratius Munishi 'Dida', wanaoshindana kwenye Beki Bora wa Mwaka ni Erasto Nyoni, majeruhi Shomari Kapombe na Paschal Wawa na kwenye kipengele cha Mchezaji Chipukizi wameshindanishwa Rashid Juma, Adam Salamba na Paul Bukaba.

Kuna wachezaji pia wanaowania tuzo la Goli Bora la Mwaka, ambao ni Claotus Chama, Meddie Kagere na John Bocco.

Tuzo zikitoka huko zinahamia kwa viongozi wa klabu pamoja na wadau wengine, hizo zinaitwa tuzo za heshima.

Hizo hupatiwa watu walioifanyia makubwa klabu hiyo huko nyuma, waliojitolea jasho, nguvu na hata uhai wao kwa ajili ya klabu. Tuzo hizi zinawajumuisha wachezaji, viongozi, wanachama au mashabiki, wawe hai au wamefariki dunia. Mwaka jana tuliona tuzo ya shabiki bora wa mwaka ikienda kwa shabiki mwanamama marehemu Fihi Salehe Kambi ambayo ilichukuliwa na mwakilishi wake.

Wakati zimebaki siku chache kabla ya tuzo hizo kutolewa, klabu ya Simba inapaswa iwe na kumbukumbu ya baadhi ya wachezaji na mashabiki wake wa nyuma ambao wameshawahi kufanya mambo makubwa kiasi cha kupoteza uhai wao kwa sababu ya klabu hiyo.

Ni kwa sababu tu Watanzania, hasa kwenye tasnia ya michezo, si Shirikisho la Soka nchini (TFF), wala klabu zenye tabia ya kutunza kumbukumbu za wachezaji au matukio ya miaka ya nyuma ili kuwa kama kielelezo au funzo kwa kizazi kijacho.

Mfano kwa sasa wengi wanasema kuwa aliyekuwa kiungo mahiri wa klabu hiyo marehemu Patrick Mafisango apewe tuzo maalum ya heshima, lakini Simba wanapaswa warudi nyuma wakumbuke kuwa kulikuwa na mchezaji aliyeitwa Hussein Tindwa aliyefia uwanjani akiwa amevaa jezi ya klabu hiyo.

Mafisango alifariki Mei 17, mwaka 2012 jijini Dar es Salaam kwa ajali ya gari akiwa mchezaji wa Simba, Tindwa alianguka akiwa uwanjani mwaka 1979 wakati Simba ikicheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Racca Rovers ya Nigeria jijini Dar es Salaam, akafariki dunia akiwa na jezi ya Simba mwilini.

Hawa ndiyo mashujaa wa kukumbukwa ambao hawasemwi wala habari zao kutajwa na naishauri Kamati ya Tuzo angalau ingalie ni jinsi gani na kufanya ili Tindwa naye apate tuzo yake kwa sababu afadhali Mafisango anazungumzwa na kizazi cha sasa, lakini beki huyo wa kati aliyekuwa akiinukia ni kama historia na Simba yenye kama vile haimtendei haki.

Kwenye upande wa shabiki bora, pamoja na kuwa na shabiki bora wa mwaka, lakini tuzo nyingine maalum ingekwenda kwa shabiki ambaye, ingawa wenye Simba huwa hawaielezei, sana, lakini mitaani inazungumzwa sana na mashabiki wa soka hasa wa miaka ya nyuma.

Mwaka 1974, baada ya Simba kufungwa mabao 2-1 na Yanga, Uwanja wa Nyamagana, mechi ambayo ilikuwa inaelekea Simba kupata ushindi, lakini mahasimu wao walisawazisha dakika ya majeruhi na baadaye kupata bao la pili, simulizi zinadai kuwa kuna shabiki mmoja huko Mwanza alijirusha kwenye pipa la maji na kufariki.

Viongozi wa Simba walipaswa wawe wanafanya utafiti na kujua alikuwa ni nani na familia yake au ndugu zake wako wapi kwa sasa.

Simba ikitoa tuzo kwa shabiki kama huyu, itakuwa ni faraja hata kwa familia au ndugu zake na kuona kuwa alichofanya ndugu yao enzi zile ni kitu cha kishujaa kwani amekumbukwa na kuenziwa.

Kwa haya yote, ni kwamba kuanzia sasa klabu zetu zianze kukusanya rekodi na historia ya matukio yote yaliyotokea huko nyuma na kuyaweka kwenye maandishi na pia ziwe na maktaba ya kuonyesha matukio na watu muhimu waliofanya makubwa na kusababisha klabu hizi zisimame hadi leo hii kuwa kubwa na kupendwa na watu wengi nchini.