Siasa safi ni muhimu kwa ajili ya umoja wa Watanzania

11Jan 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Siasa safi ni muhimu kwa ajili ya umoja wa Watanzania

TANGU nchi hii iingie kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa zaidi ya miaka 20 iliyopita, Watanzania wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kuanzisha vyama vya siasa na wengine kujiunga na vyama hivyo kwa lengo la kupanua wigo wa demokrasia.

Walifanya hivyo kwa sababu siasa siyo uadui bali ni kushindanisha hoja mbele ya wananchi ili hatimaye waamue ni chama kipi wanaweza kujiunga nacho ama wabaki bila chama au wahame kutoka kimoja kwenda kingine.

Ninasema hivyo kwa sababu kuna Watanzania wengi wasiokuwa wanachama wa chama chochote cha siasa ila wana mapenzi na vyama vya siasa, ambavyo wenyewe huvutiwa navyo na kuamua kuvishabikia.

Lakini wamekuwa wakiogopa kuingia kwenye siasa kwa kuogopa chuki, uadui na fitina, ambazo wanasiasa wamekuwa wakizitumia ili kujihakikishia uhalali wa kuongoza vyama vyao.

Kwa maana hiyo ni vyema vyama vya siasa vikajitahidi kufanya siasa safi ili wale ambao hawataki kushiriki siasa kwa kuogopa chuki na uadui waweze kushiriki na kuongeza wigo wa nani anaweza kuwa kiongozi kwenye vyama husika.

Ikumbukwe kuwa wapo baadhi ya Watanzania ambao bado hawajajiingiza kwenye siasa kwa sababu wanaogopa kitu kinachoitwa 'mchezo mchafu' ambao chimbuko lake ndiyo hizo fitina chuki, ambazo huzaa uadui.

Inapofikia hatua hiyo maana yake ni kwamba hata umoja wa Watanzania unayumba kwa sababu tu ya siasa, ndiyo maana ninasema siasa ni muhimu kwa ajili ya umoja wa Watanzania.

Tunaweza kuendelea na umoja wetu wa kuepuka chuki, fitina kwenye siasa kwa wanasiasa kuzingatia zaidi kushindanisha hoja ili Watanzania wenyewe waamue ni upande gani wa chama cha siasa wanaweza kuegemea.

Lakini vinginevyo itakuwa ni uadui, kwani wapo baadhi ya Watanzania waliojiingiza kwenye siasa, lakini sasa wamejiweka pembani baada ya kukumbana na kadhia hiyo na hata kushambuliwa na watu wasiojulikana na kuumizwa vibaya.

Mmojawapo ni aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chadema Wilaya yaTemeke, Joseph Yona, ambaye aliamua kubwaga manyanga kwa kuacha kujihusisha na masuala ya siasa na kusema kuwa siasa ni mchezo mchafu.

Kiongozi huyo aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari baada ya kukutana navyo na kuelezea uamuzi wake huo kwamba hataki tena kusikia kitu kinachoitwa siasa na badala yake sasa anaendesha maisha nje ya siasa baada ya kunusurika kufa.

Akasema kuwa hawezi kuhatarisha maisha yake huku akiwa na mifano hai ya mambo ya kutisha yaliyomkumba akaachwa akapambana pekee yake na kunusurika kufa bila kupata msaada wowote.

Akaweka msimamo kwamba hawezi kujihusisha na kitu kinachoitwa siasa na kamwe hawezi kurudi Chadema ama kuhamia CCM na kwamba atabaki kuwa raia wa kawaida ili aweze kufanya shughuli zake binafsi.

Ninadhani Baraza la Vyama vya Siasa halina budi kumulika hali hii ili kuondoa uadui, chuki, fitina kwenye siasa za Tanzania ili Watanzania waendelee kuwa kitu kimoja bila kujali itikadi zao za vyama.

Wanasiasa wanajua majukumu ya baraza hilo kuwa mojawapo ni kumshauri Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu migogoro baina ya vyama vya siasa, kumshauri kuhusu masuala yenye masilahi ya kitaifa yanayohusu vyama vya siasa na hali ya siasa nchini.

Kuishauri serikali kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu kutungwa ama marekebisho na utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa na sheria nyingine zinazohusu vyama hivyo, kushauri kuhusu uratibu wa shughuli za vyama vya siasa na kumtaarifu kuhusu masuala yoyote yanayohusu utendaji wa chama chochote cha siasa.

Katika majukumu hayo ya baraza ninadhani wanaweza kuzungumzia jinsi ya kuendesha siasa bora na zenye ustawi kwa taifa hili kwa kuacha fitina ndani ya vyama ama kati chama kimoja na kingine.

Katika mazingira hayo hakutakuwa na mchezo mchafu na itakuwa ni rahisi kuifanya Tanzania kuwa ya kwanza na siasa baadaye, hasa kwa kila jambo ambalo lina maslahi kwa umma.