Sichoki wala sitochoka kusahihisha

05Sep 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Sichoki wala sitochoka kusahihisha

MOJA ya magazeti ya michezo yanayochapishwa humu nchini, liliandika kwa herufi kubwa, nyeusi ti: “TUNALIAMSHA DUDE UPYA.”

“Salaam. Hali yako. Kwanza nakuuliza: hizi makala zinakuwa mali ya gazeti au waweza kuzitumia tena? Kama waweza, kwa nini zisikusanywe zikatoka kama kitabu kwa faida ya kudumu?” Ananiuliza mwalimu na rafiki yangu Mohamed Sharif wa Tanga.

Akaendeleza ujumbe wake: “Upondo ni mti mrefu mgumu unaotumiwa kusogezea dau kwenye maji machache kwa kukita chini. Kuna msemo wa watu wachache wa mambo au elimu: ‘huyo ni maji ya upondo tu.’

2. “Kasia hutumika kwenye maji mengi (au marefu). 3. Fito ni miti myembamba sana hutumika kwenye ujenzi wa nyumba. Msemo: ‘Mbona twagombea fito nasi twajenga nyumba moja?’

“Kama kabila haiuzwi lakini yanunuliwa. Hapo zamani watu walinunua kabila nyingine hasa za watawala wao. Kama kwa Wareno akipewa cheti kwamba yeye sasa si Mmakonde tena bali ni Mreno halafu wanamwita ‘assimilado.’

“Kuhusu ‘Sports Extra’ hii ni habari ya ziada ya michezo’ si michezo ya ziada kwani michezo ya ziada itakuwa mingine ya zaidi ya tuliyonayo. Jioni njema.”

Alijibu makala niliyoandika kuhusu kuchanganya Kiswahili na Kiingereza kwenye magazeti yetu.

Turudi kwenye ‘dude.’ Kwa mujibu wa Kamusi la Kiswahili Fasaha, ‘dude’ ni dubwana yaani mtu anayedharauliwa; lakabu ya kuonesha dharau kwa mtu mwingine.

Kamusi ya Karne ya 21na Kamusi Kamili ya Kiswahili zaeleza maana ya ‘dude’ kuwa ni kitu kikubwa kisichojulikana; dubwana.

Kamusi ya Kiswahili Sanifu yaeleza maana ya ‘dude’ kuwa ni dubwana, nyangarika. Pia neno hilo hutumiwa kuitia kitu au mtu unayemdharau au usiyetaka kumwita jina. Kamusi ya Visawe (maneno yenye maana zinazokaribiana) yasema ‘dude’ ni dubwana, nyangarika, mbwedu, jitu, dubwana.

Kwa lugha ya Kiingereza, ‘dude’ ni unknown massive thing. 2 despicable thing/person, contemptible thing/person.

Baada ya kueleza hayo kwa kunukuu kamusi mbalimbali zinavyoeleza maana ya ‘dude,’ sasa nauliza: Je, neno hilo latumiwa kwa maana yake? Ni moja ya visawe au ni mwendelezo wa upotoshaji lugha?

Tusonge mbele: “Nyota huyo, katika michezo mitano aliyoshuka uwanjani kipindi akiwa Azam FC kuwania taji hilo, ameingia kimiani mara nne.

Najua mtaniita mhafidhina (mtu anayeshikilia na kuifuata falsafa na mfumo maalumu wa kuendesha jambo) lakini sichoki kukosoa. Hebu nambieni kati ya mchezaji na mpira kinachoingia kimiani ni mtu au mpira unaochezewa?
‘Kimia’ ni wavu wa nyuzi ndogondogo. ‘Kimiani’ ni ndani ya goli la soka, ndani ya kimia. “Alipiga mpira wa kona hadi kimiani.”

Ingeandikwa: “Katika michezo mitano aliyokuwa mchezaji wa Azam FC, alifunga mabao manne” au “ … alitumbukiza mabao manne kimiani.”

Katika mtange huo, kama Bocco atakuwa amerejea kikosini na kutumiwa na Kocha wake, Joseph Omog, huenda itakuwa ahueni kwa mashabiki wake wa Simba kuendeleza rekodi yake hiyo.”

Sentensi hii ina neno moja lililo tofauti na habari yenyewe. Pia baadhi ya maneno yaliyotumiwa hayakuwa na umuhimu wowote.

Mwandishi kaandika: “Katika mtange huo …” Maana ya ‘mtange’ ni chuma cha mizani kilicho katikati ya sahani za mizani. Kwa nini “ … mashabiki wake wa Simba?” Ingetosha kuandikwa ‘mashabiki wake

Kwa faida ya wasomaji, ‘mizani’ haina umoja wala wingi. Kwa hiyo kusema ‘mzani’ kama walivyozoea wengi ni kosa.

Nimeeleza mara nyingi kuwa kusema kutokukula, kutokusema, kutokulia, kutokucheka n.k. ni makosa ingawa bado waandishi wanaendelea kufanya kosa hilo. Soma sentensi ifuatayo:

“Gazeti … lilielezwa kwamba, Bulaya alikamatwa kwa mahojiano katika Ofisi ya Mkuu wa Makosa ya Jinai wa kanda hiyo akituhumiwa kutokutii amri ya Serikali iliyozuia mbunge mwingine kwenda kuhutubia mkutano jimbo jingine.”

Badala ya kuandikwa ‘kutokutii,’ ingeandikwa ‘kutotii’ bila ‘ku’ katikati ya herufi ‘o’ na ‘t.’ Kwa hiyo maelezo yangu ya paragrafu ya tatu kwenda juu kutoka hii ingekuwa kutolala, kutosema, kutolia, kutocheka n.k.

“Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga aliliambia gazeti hili” (si hili unalosoma sasa) “jana kwamba baada ya kutokea kwa vurugu …”

Waandishi wa leo hutumia maneno ‘kwa,’ ‘huyo,’ ‘hao,’ bila sababu za msingi. Hivi kweli ni sahihi kuandika au kusema “… kutokea kwa vurugu” badala ya “kutokea vurugu?”

Pia imeandikwa: “Alisema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na baada ya kumalizika kwa mahojiano watapandishwa kizimbani kujibu tuhuma zao.” (Maneno 16 yaliyopangwa ovyo).

Ingeandikwa: “Alisema watuhumiwa watakapomaliza kuhojiwa watapelekwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.” (Maneno tisa yanayoeleweka haraka).

Methali: Wanja wa manga si dawa ya chongo.

[email protected]
0715/0784 33 40 96