Sifa hizi zaweza kuihadaa Yanga

11Jun 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Sifa hizi zaweza kuihadaa Yanga

SIFA ikizidi sana si sifa tena bali ni hadaa (kitendo cha kumlaghai mtu). Mtu huvimbishwa kichwa kwa sifa hata asizokuwa nazo naye akaishia kubweteka.

Viongozi na wachezaji wa Yanga wasikubali kuhadaika kwa sifa wanazopewa na magazeti kwani waandishi huchagua vichwa vinavyowashawishi wasomaji wanunue kazi zao.

Vichwa vya magazeti mengi ya michezo huwa tofauti kabisa na habari zake. Soma hii: “Yanga hii haitaki hasira *Ngoma awalaza Al-Ahly na viatu.” Nani aliyewaona wakilala na viatu kama si hadaa? Hao wanaosemwa walilazwa na viatu ndio walioitoa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika!

*“Waangola waweseka.” Jijini Dar es Salaam, kweli Waangola walifungwa mabao 2-0 lakini kwao waliishinda Yanga bao 1-0. ‘Weweseka’ ni kitendo cha mtu kusema akiwa usingizini. Nani aliyewaona Waangola wakiweweseka?

“Yanga hii wataikoma.” Sijui onyo hilo lilizihusu timu zipi. Hata hivyo Yanga itakomwa kwa lipi? Timu zote zinazoingia uwanjani kupambana, hucheza kwa lengo la kupata ushindi. Hazichezi ili zifungwe.

Mara nyingi timu kongwe huhangaishwa sana zinapokutana na timu zinazoitwa ‘ndogo’ ingawa kila moja huwa na wachezaji 11 uwanjani. ‘Udogo’ wa timu hizo sijui hupimwaje kwani mara nyingi huzitoa kamasi jembamba hizo kongwe.

Vichwa vingine vya magazeti: “Mnaibishia Yanga?” Kina nani wanaoibishia na kinachobishiwa ni kitu gani? “Yanga yatisha vigogo Afrika.”

Vigogo hao watishwa kwa jipya lipi wasilolijua katika kandanda? “Ndiyo mtaijua Yanga sasa.” Kwani ilikuwa haijulikani tangu ilipoundwa mwaka 1935?

Vichwa kama hivi ndivyo vinavyowapotosha wachezaji kwa kujiona wao ni wao hakuna kama wao kumbe wanachotwa akili! Sifa za aina hiyo ndizo zinazofanya timu zinazodharauliwa zicheze kwa ari, nguvu na kasi zaidi ili kupata ushindi; na hutokea kuwa hivyo.

Simba na Yanga zinaposhindwa na timu ziitwazo ‘ndogo’ (ingawa zote zacheza Ligi Kuu ya Bara), huwa mwanzo wa chokochoko. Wachezaji hulaumiwa, eti kwa kucheza ‘chini ya kiwango,’ au baadhi ya viongozi kuhusishwa na kipigo hicho!

Kama timu zote zimo daraja moja na idadi ya wachezaji ni sawa kila upande, vipi iwe ajabu Yanga na Simba kushindwa na hao wanaodharauliwa? Hakuna timu inayoingia uwanjani kupambana na Yanga au Simba kwa lengo la kushindwa.

Kama Manchester United/City, Arsenal, Liverpool, Chelsea na timu nyingine maarufu za Ureno, Hispania, Ujerumani, Ufaransa, Italia, Brazil, Argentina n.k. hufungwa, sembuse Yanga na Simba?

Katika hatua nyingine, Yanga wasihadaishwe na sifa za magazeti. Wafanye mazoezi ya nguvu na kuzingatia maelekezo ya walimu wao kwa makini.

Pia ni muhimu kuwa na nidhamu ya hali ya juu, ndani na nje ya uwanja.

Timu watakazopambana nazo si rahisi kama wanavyodanganywa na magazeti. Ni timu ngumu tena zenye uzoefu wa mechi za kimataifa kuliko Yanga.

Kadiri watakavyocheza kwa bidii, ustadi na nidhamu ndivyo watakavyouza majina yao kwa timu za Ulaya. Hapa walipofika si mwisho kwani bado kuna safari ndefu kufika kileleni yaani kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika.

Wakumbuke wanaziwakilisha nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani timu zingine zilitolewa kwenye michuano hii.

Watumie fursa hii adimu kulitangaza jina la Tanzania kutoka ‘kichwa cha mwenda wazimu’ na ‘Shamba la Bibi’ ili Tanzania iwe bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika Inshaallah!

Jambo lingine lawahusu wanachama wa Yanga. Leo Jumamosi wanafanya uchaguzi wa viongozi wa klabu yao. Wanapaswa kutuliza akili zao na kuchagua si bora viongozi, bali viongozi wenye uwezo wa kuiletea Yanga mafanikio na maendeleo ya kweli.

Viwanja vya michezo, shule ya kukuza vipaji na mambo mengi kama yafanywayo na vilabu vya nchi zilizoendelea. Azam FC iliundwa takribani miaka saba iliyopita na imeweza.

Ni aibu kwa timu kongwe kama Yanga kupitwa na Azam ambayo sasa ni mfano wa kuigwa katika Afrika Mashariki na bado inaendelea kuwekeza zaidi katika mchezo huo.

Hapana shaka walioomba uongozi wa ngazi zote wamepimwa uwezo, hekima, weledi wa kujua kiu ya maendeleo ya klabu.

Watakaoshindwa wakubali badala ya kuleta chokochoko.
[email protected]
0715/0784 33 40 96