Sifa za kuwa mbunge zimepitwa na wakati

09Nov 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Sifa za kuwa mbunge zimepitwa na wakati

KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Ibara ya 67- (1) inasema: Bila kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa ama kuteuliwa kuwa mbunge endapo;

(a) ni raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja, na ambaye anajua kusoma na kuandika katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza (b) ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa.

Ibara hiyo na vifungu vyake inaelekeza pia kwenye Sheria ya mwaka 1984 Na 15 ibara ya 13 na Sheria ya mwaka 1992 Na 4 ibara ya 19 ambazo zote kimsingi zinagusia usawa mbele ya sheria bila kubagua.

Nimejaribu kugusia kidogo jinsi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyobainisha sifa za mtu kuwa mbunge huku sheria nazo zikisisitiza usawa wa kupata haki bila ubaguzi.

Lengo langu ni kutaka kuzungumzia sifa hizi za mtu kuchaguliwa kuwa mbunge, ambazo binafsi ninaona kwamba zimepitwa na wakati, hivyo kuna umuhimu wa kuachana nazo ili kwenda na mazingira ya sasa.

Ninasema hivyo kwa sababu Tanzania ni nchi, ambayo inakuwa na kubadilika kiuchumi, kisiasa, kijamii na kitamaduni, kwa kuwa sio siri kwamba nchi imepiga hatua kubwa tangu kupata uhuru mwaka 1961.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa wakati huo nchi inapata uhuru, kulikuwa na wasomi wachache kutokana na uhaba wa shule za sekondari, lakini sasa kuanzisha shule za msingi, sekondari hadi vyuo ni vingi.

Maana yake ni kwamba kwa sasa wasomi wapo wengi, ambao wanatakiwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi ukiwamo ubunge kwa sababu wana sifa zinazotakiwa badala ya kuendelea kuwa na sifa zilizopitwa na wakati.

Kwa mtazamo wangu ni kwamba kilichochangia kuwapo kwa sifa za mtu kuchaguliwa ubunge kuwa za kujua kusoma na kuandika katika lugha ya Kiswahili au Kiingereza ni uhaba wa wasomi uliokuwapo wakati huo.

Kujua kusoma na kuandika lugha hizo mbili hakupaswi kuendelea kuwa kigezo cha mtu kuwa mbunge, kwa sababu sio kujua kusoma na kuandika tu bali mtu anatakiwa kuwa na uelewa zaidi wa kupambanua mambo kama msomi hasa kutokana na ukweli kwamba kuna hoja nzito za kisomi, ambazo huwasilishwa bungeni na hutakiwa kujadiliwa.

Haiingii akilini kuona mtu anayejua tu kusoma na kuandika anapewa jukumu kubwa la kutunga sheria ingawa ubunge sio taaluma, lakini linapokuja suala la kutunga sheria halihitaji mbunge wa aina hiyo.

Hata Muswada wa Huduma za Vyombo vya Habari uliopitishwa na Bunge wiki hii pamoja na mambo mengine, unagusia viwango vya elimu kwa waandishi, lakini itakuwaje kama miongoni mwa waliopitisha muswada huo ni wale waonajua kusoma na kuandika Kiswahiili au Kiingereza tu!

Ni kweli kila mtu ana haki ya kikatiba ya kuwa kiongozi, lakini pia kuna haja ya kuangalia ni nafasi gani anayotaka kama ana uwezo nayo kielimu badala ya kuendelea kung'ang'ania tu kwamba sifa za kujua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili au Kiingereza.

Nafasi za uongozi nyingi kuanzia kazi za chini kwenye vitongoji, vijiji, mitaa na kata, lakini ajabu ni kwamba mtu mwenye sifa za kuwania huko anakimbilia kwenye ubunge kwa sababu katiba inamruhusu!

Huku ni sawa na kutoitendea haki nafasi hiyo kwa sababu mchango wa mhusika hautakuwa mkubwa kama ambavyo angekuwa na elimu ya kutosha ya kuweza kupambanua mambo makubwa yanayohitaji uelewa mpana.

Lakini ajabu ni kwamba hata pendekezo la rasimu ya Katiba mpya kuwa wabunge walau wawe na elimu ya kidato cha nne lilitupiliwa mbali na wajumbe wa Bunge la Maalum la Katiba baada ya kamati karibu zote kuliweka pembeni.

Hii ilikuwa ni mwaka 2014, baadhi ya wajumbe walisikika wakisema kuwa kuweka kigezo cha elimu ya kidato cha nne ni ubaguzi, hivyo sifa zilizomo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ziendelee kutumika.

Walifanya hivyo wakiwa wamesahau kwamba wakati wa sasa sio ule wa mwaka 47, mambo yanakwenda kisomi zaidi ndio maana ikapendekezwa angalau sifa ziwe ni elimu ya kuanzia kidato cha nne.

Sasa hapo ubaguzi unakuwa wapi? Kwani hakuna nafasi nyingine ambazo watu wanaojua kusoma na kuandika lugha za Kiswahili na Kiingereza wanaweza kuzifanya hadi ubunge tu?

Inawezekana kweli kwamba wapo wenye elimu ya chini wanaoweza kuongeza na pia wapo wasomi wasio na uwezo wa kuongoza, lakini cha msingi hapa ni kuwa na wabunge wanaoweza kukabiliana na changamoto za sasa.

Kwa ujumla ni kwamba kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na wabunge ambao angalau wamefika sekondari wanaweza kuwa na uwezo wa kujadili na kutoa ushauri wanapojadili ama kupitisha bajeti mbalimbali.