Sijaelewa nini hatima ya bonde la Mkwajuni?

05Jan 2017
Mary Geofrey
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Sijaelewa nini hatima ya bonde la Mkwajuni?

MWAKA mmoja umeisha tangu serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba Maendeleo ya Makazi kwa kushirikia na Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), zibomoe nyumba 250 za wakazi wa Bonde la Mkwajuni, katika wilaya ya Kinondoni, Jijini Dar es Salaam.

Katika ubomoaji huo, wastani wa watu 2,000 walikosa makazi, katika azma ya serikali ni kuokoa maisha ya wananchi wanaokumbwa na mafuriko kila msimu wa mvua.

Hatua ya ubomoaji nyumba, ilitekelezwa miezi michache baada ya aliyekuwa Rais wakati huo, Jakaya Kikwete, kufanya ziara ya kuwatembelea waathirika wa mafuriko, wakiwamo wa bonde hilo na kuagiza nyumba zilizoko huko zibomolewe.

Rais Kikwete wakati huo, aliagiza kuwa nyumba za wakazi zibomolewe na serikali iwapatie maeneo ya mbadala wa kuishi, kabla ya kufanya hivyo. Lengo ni kupisha njia za maji.

Mnamo Novemba 17 mwaka juzi, serikali mpya iliyoko madarakani sasa, ilianza kutekeleza agizo hilo kwa kuvunja nyumba za wakazi wa bonde la Mkwajuni.

Mara baada ya nyumba kuvunjwa na wakazi wengine wakiendelea kutafuta hifadhi kwingineko, wako waliojikimu kwa kujenga vibanda 186 kwenye vifusi vilivyobomolewa, lakini serikali ilirudi tena na kuvibomoa.

Wakati hayo yakiendelea, wakazi hao walilalamika kutolipwa fidia ya makazi, huku waliokosa hifadhi wakiendelea kurandaranda katika eneo hilo.

Sasa ni mwaka mmoja tangu wakazi hao wabomolewe nyumba zao. Jumla ya vibanda 95 vimejengwa kwa mfumo wa maisha, kila kibanda inaishi kaya moja.

Kwa mujibu wa Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kawawa katika bonde hilo, Kikozile Abdallah, wakazi hao ni waliokosa mbadala wa mahali pa kuishi ama kwa ndugu jamaa na marafiki. Hadi sasa wana mwaka mmoja mahali hapo.

Ukiviona kwa nje, unaweza kudhani wanaoishi vibandani hapo ni waliokosa shughuli za kufanya na wanajihifadhi kusogeza siku za maisha yao.

Lakini ukiingia ndani, hali ni tofauti. Utakutana na wanawake, watoto wadogo na wanafunzi, ambao wote wana mahitaji muhimu ya kibinadamu, ambayo kimsingi yanafahamika vyema.

Ndani ya vibanda kuna maisha magumu. Wenyeji wanalazimika kudumu humo kwa kukosa mbadala wa pa kwenda.

Wakazi hao, watoto kwa wakubwa, wanatumia vyoo vitatu pekee kwa ajili ya kupata huduma za kujihifadhi.

Jambo la hatari zaidi ni kwamba eneo hilo limezungukwa na mbu wengi na kuna wadudu hatari kwa maisha yao ya kila siku.

Pia, huduma za maji na usalama wa afya wakati wa jua kali na mvua ni ndogo sana, hali inayowafanya waishi katika mazingira yenye hatari kubwa.

Malalamiko yaliyoko ni kwamba, fidia za makazi hawajawahi kulipwa na serikali, isipokuwa kwa baadhi yao ambao si wakazi wa eneo hilo. Sijui ukweli huo una hakika gani?

Jambo lingine wanaoililia serikali iwasaidie ni kwamba, wapatiwe eneo la kuishi na familia zao ili kuyaendeleza, badala ya kuendelea kufumbia macho yanayoendelea katika bonde hilo.

Serikali ilipobomoa nyumba, waliopata hifadhi na waliokuwa na uwezo waliondoka. Wapo waliobaki hawana mbele wala nyuma.

Bado wanahitaji msaada wa serikali kwa sababu wanaonyesha kabisa wana uhitaji ukizingatia eneo wanaloishi, siyo rafiki kwa afya ya binadamu.

Serikali inaweza ikaona namna ya kuwasaidia wakazi ambao si wengi, ikilinganishwa na waliokuwapo awali.

Pia, serikali ikihisi haiwezi kuwasaidia, hakuna sababu ya kuwaacha waendelee kuishi katika eneo hilo, hatari ambalo kila wiki watu hao wanaugua malaria na maradhi mengine ya kuambukiza.

Wakati serikali ikipambana na malaria, kuna watu walioko katika maeneo hatarishi na inakaribisha magonjwa.

Nadhani, wakazi hao wanaendelea kuishi katika eneo hatari, kwa sababu tu wameona serikali ipo kimya katika suala la kupaendeleza.

Mwaka jana umeisha, hakuna kilichoendelea. Kuna shaka wataongezeka watu bondeni hapo na makazi mapya hayo yatarudia zama zake za kabla ya bomoabomoa kufanyika.

Binafasi naona, hakukuwapo sababu za kuvunja nyumba za wakazi hao tena kwa ghafla na kutumia nguvu kubwa, iliyowaingiza kwenye matatizo na eneo hilo likiendelea kubaki kama ilivyo.

Hadi sasa sioni dalili zozote kufanyika kuhusu kukamilisha azma ya kusafisha bonde la Mkwajuni na kama itakuwa hivyo, bomoabomoa ilikuwa kutwanga maji kwenye kinu?